loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vijana 60 wafundishwa kuhudumia watalii

Mafunzo hayo ya wiki moja yamefadhiliwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa lengo la kuwawezesha vijana hao kutoa huduma bora kuchocheo kuvutia watalii zaidi kuja kwa wingi nchini.

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kaskazini, Angelus Ngonyani aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kufunga mafunzo hayo na kuongeza kuwa kabla ya kutoa mafunzo hayo walifanya utafiti na kubaini asilimia kubwa ya vijana hao hawana elimu kuhusu kazi hiyo na wanaifanya kwa mazoea kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Ngonyani alisema baada ya kugundua hilo waliamua kufadhili mafunzo hayo ambapo awamu ya kwanza walianza na wabeba mizigo (wapagazi) ikiwa ni jukumu la Veta kupanua wigo katika sekta isiyo rasmi.

Alisema mafunzo waliyopatiwa vijana hao ni pamoja kuwajali wateja, kutoa huduma ya kwanza kwa mteja, ujasiriamali na jinsi ya kuwa na matumizi bora ya fedha wanazozipata.

Naye mmoja wa wapagazi hao, John Isonda alisema mafunzo hayo yatawasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na changamoto walizonazo za kuwahudumia wateja kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu sekta hiyo.

Alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kutodhaminiwa na makampuni wanayofanyia kazi kama wanavyodhaminiwa waongoza watalii wa mbugani na hali hiyo imesababisha kukwamisha mipango yao.

Walitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kutokuwa na mikataba ya kudumu ya ajira na kampuni wanazofanyia kazi, kutokuwa na chombo maalumu cha Serikali ambacho kitadhibiti ubora wa waongoza watalii nchini.

Mgeni rasmi katika ufungaji wa mafunzo hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Arumeru, Evalilian Boma kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Nyirembe Munasa aliwataka vijana hao kutumia vizuri elimu waliyopata kuwa chachu ya kuongeza watalii nchini.

foto
Mwandishi: Veronica Mheta

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi