loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vijana: Usomi vyeti au maarifa?

Namshukuru Mungu sijambo, mambo si mabaya, nazidi ‘kuzichanga’, kama wao walishindana na wakashinda kwa nini nisiweze? Naamini mimi na wewe tunaweza kufika tulipokusudia, jambo la msingi ni dhamira, mipango, na mikakati ya kutekeleza tuliyokusudia.

Tutumie elimu tuliyonayo, maarifa na vipaji vyetu kuboresha maisha yetu. Wakati najiandaa kuandika haya nilikuwa najiuliza, msomi ni nani?

Ni mhitimu wa chuo cha elimu ya juu, chuo kikuu, sekondari au hata yule aliyehitimu ngazi ya cheti katika chuo cha ufundi lakini mwenye maarifa makubwa kwenye jambo fulani analofanya?

Najiuliza hayo kwa sababu kwenye jamii yetu kuna wanaoitwa wasomi na wasiosoma kwa vigezo vya ngazi ipi ya elimu amefika mhusika.

Waliohitimu vyuo vya elimu ya juu wanaitwa wasomi kwa sababu wana Shahada, Stashahada au vyeti, hata kama hawana maarifa ya jambo au mambo fulani kuwawezesha kuendesha maisha yao.

Kwa hali ilivyo sasa kwenye jamii si vibaya ukijiuliza msomi ni nani? Ni sahihi kuitwa msomi kwa sababu tu una Shahada au Stashahada hata kama huwezi kuitumia elimu yako kuendesha maisha yako?

Usomi unapimwa kwa ngazi uliyofika kulingana na mfumo wetu wa elimu au maarifa uliyonayo kwa jambo unalolifanya? Kuna wanaoamini kuwa kusoma si kupanda kidato, si sahihi kuamini hivyo?

Ni sahihi kuendelea kuamini usomi wa mtu kwa sababu tu kahitimu chuo kikuu? Kwa nini tunaendelea kuthamini yaliyoandikwa kwenye vyeti kuliko maarifa ya mhusika katika kufanya jambo fulani?

Wapo waliohitimu darasa la saba lakini wana uwezo mkubwa wa kufanya biashara kuliko mwenye Stashahada ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

Kuna mkulima kijijini asiyejua kusoma au kuandika mwenye uelewa mkubwa katika ufugaji wa samaki kuliko mhitimu katika Chuo cha Uvuvi Mbegani.

Kwa mifano hiyo, tunatumia vigezo vipi kusema fulani ni msomi na yule siye? Ninaamini kuwa kufeli darasani si kufeli maisha, na si kila aliyefanikiwa katika maisha ‘amesoma’, mifano ipo mingi ya watu ambao hawapo kwenye kundi la ‘wasomi’ lakini wamefanikiwa sana katika maisha yao hasa kupitia biashara.

Unaweza kuwa ‘kilaza’ darasani lakini ukawa fundi mzuri wa nguo, umeme, magari, mbao, au ukafanya biashara hadi watu wakashangaa, ili utoke si lazima uwe na diploma au shahada, na si wote wenye elimu hiyo wametoka.

Usikatishwe tamaa kwa kujiona wewe si miongoni mwa wasomi, kila mtu ana kipaji fulani, ni bahati mbaya kwamba wengi hawavitambui vipaji vyao na hawaoni kwamba hilo ni tatizo.

Itumie siku ya leo kutambua kipaji chako na ujiulize kwa nini usikitumie kikutoe, siku njema. bmsongo@hotmail.com

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi