loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vijana: Wafe wangapi?

Wasalimie wadau hapo, hongera kwa kuiona siku ya leo, kuna walioiona jana, leo hawapo, wamemaliza safari yao, wametangulia, Mungu awarehemu.

Poleni mliopoteza wazazi, walezi, ndugu, jamaa, marafiki katika ajali za barabarani na kwingineko, naamini nyingi zimetokea si kwa sababu ni mipango ya Mungu ilani uzembe wa wanadamu.

Inasikitisha, inauma sana kuwapoteza wapendwa wetu katika mazingira kama yale, tumshukuru Mungu kwa sababu waliishi miongoni mwetu, tuliwapenda, wamekwenda, wapumzike kwa amani.

Ajali hasa za bodaboda na magari zimekuwa kama wimbo, siku hizi ukimwambia mtu kuna ajali swali la kwanza anauliza wamekufa wangapi ikiwa na maana vifo kutokana ajali sasa limekuwa jambo la kawaida, vimezoeleka.

Ajali nyingi si bahati mbaya, mifano ipo na wahusika wanalifahamu hilo ila tunashawishiwa tuamini kwamba eti ni mipango ya Mungu’. Sina uhakika kama Mungu yule yule aliyekuumba na kukupa uhai na mwili, na tunayeamini kuwa anatupenda anaweza kupanga ufe kikatili kwa ajali.

Ipo mifano hai, ni nani leo anaweza kujenga hoja yenye mantiki kwamba, meli ya mv Bukoba ilizama kwa kuwa ilikuwa ni mipango ya Mungu?, Meli ya mv Spice Islanders ilizama kwa bahati mbaya Zanzibar?

Mabasi, magari mengine yanayoua kila mara, na ajali za bodaboda ni bahati mbaya au mipango ya Mungu? Tunasubiri wafe wangapi ndipo tuseme inatosha? Au tunajisikia fahari kutoa rambirambi kwa wafiwa na kuwatembela majeruhi hospitali?

Kila zinapotokea ajali wananchi wanaelezwa kwa Polisi wanachunguza vyanzo vya ajali hizo, lakini sijaona faida ya uchunguzi huo kwa sababu haujasaidia kuzuia nyingine zisitokee.

Mimi, wewe, yule na wale wote tunafahamu vyanzo vya ajali, hicho kinachodaiwa kuwa ni uchunguzi ni danganya toto tu, tuwe wakweli, Polisi wameshindwa kuzuia ajali za barabarani, zinatokea na huenda zitaendelea kukatisha maisha ya Watanzania wasio na hatia.

Japo hili halizungumzwi, ajali hasa za barabarani na majini zimekuwa chanzo kikubwa cha hasara za kiuchumi kwa makundi mbalimbali, zinasambaratisha familia kwa kuua na kusababisha ulemavu, zimekatisha ndoto, malengo na matuamini ya wananchi wengi, zimekuwa kichocheo kikubwa cha umasikini kwa Watanzania na utafika wakati, watu wengi watakufa kwa ajali kuliko kwa Ukimwi na malaria.

bmsongo@gmail.com

Waziri Mkuu Mstaafu, ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi