loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vijana: Wajane, wagonjwa wanastahili furaha

Mungu ni mwema, namshukuru kwa zawadi ya uhai, tuzidi kumuomba atulinde na atuwezeshe kutimiza malengo yetu. Tusherehekee kwa amani, tustarehe kwa kiasi ili furaha isiwe chanzo cha matatizo, kero kwa wengine, majuto, migogoro, ajali, na mengine mabaya kwenye jamii.

Tuoneshe upendo kwa wenzetu wote bila kujali umri, rangi, dini, kabila, jinsi au uwezo wake kiuchumi, tusiwabague, tuwe nao, tufurahi nao, tule nao, tucheze nao, tunywe nao kwa kuwa vyovyote vile walivyo, wao ni binadamu kama mimi na wewe.

Pasaka ni sikukuu hii ni ya kidini lakini ubinadamu hauna dini. Ukristo, Uislamu au dini yoyote ni imani, ubinadamu ni jambo la asili, hauna mipaka na haubagui.

Kwa kuwa dini ni upendo, jitahidi kutumia fursa hii kuthibitisha upendo wako kwa sababu, naamini Mungu ndiye aliyetuumba kupitia wanadamu, hivyo huwezi kumpenda yeye kama unawachukia au huwathamini wanadamu wenzako.

Jitoe kwa ajili ya hao, walipenda na wanatamani kufurahi kama wewe, wana hamu ya kuwa na kipato kama chako, na wanahitaji faraja ambayo naamini wanaweza kuipata kwako.

Kutoa ni moyo na si utajiri, hata kama wewe si tajiri bado unaweza kujitoa kwa ajili ya wengine, msaada kwa wengine si lazima uwe wa fedha au vitu.

Hata usipowapa fedha au vitu, muda wako una thamani kubwa sana kwao kwa sababu faraja watakayoipata ni muhimu ili kuwapa moyo, kuwafariji, wasikate tamaa, waone thamani ya ubinadamu wao.

Hata kama huna ndugu, jamaa, jirani, au rafiki aliyelazwa nenda hospitali kawafariji wagonjwa, kawasalimie watoto wa mitaani, yatima, wajane na wengine wanaohitaji faraja.

Usisubiri uwe tajiri ili wengine wapate kwako, toa hata hicho kidogo ulichonacho kwa njia ya muda kwa kuwashauri wenye matatizo ili watumie busara kuyatatua badala ya pupa, hasira, au visasi.

Usijitoe kwa sababu wewe una madaraka au uwezo mkubwa kifedha, jambo la msingi , ni utayari wako kusaidia na thamani ya unachokifanya kwa wengine.

Jiulize utamsaidiaje jirani yako asiye matumaini kwa sababu ya ugumu wa maisha? Wafungwa na mahabusu magerezani watarajie nini kutoka kwako?

Usijitoe ili na wewe uje upewe, fanya hivyo kwa sababu unaowasaidia ni wanadamu kama wewe, wanastahili furaha, faraja, kupendwa, kuthaminiwa, wana hisia na matamanio kama yako ila hawawezi kuvipata wanavyovitamani au wanavyovihitaji. Pasaka njema, Mungu Ibariki Tanzania.

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi