loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vijeba sasa basi soka la Tanzania

Mambo haya ambayo yapo kila kukicha kwenye soka la Tanzania, tena yamekuwa kama ya kawaida tu wakati hayastahili kuwepo kwenye soka letu hata kwenye nchi yeyote ile, lakini kwa Tanzania yamekuwa ni ya kawaida tu na wengi wakiyapigia chagizo au kuyakumbatia.

Kwanza kabisa uchawi (kwenda kwa waganga kuloga kwa ajili ya mechi) yaani viongozi wengi hasa wa klabu za Ligi Kuu ni ngumu kuwaepusha na hili suala la kwenda kwa waganga huku wenyewe wakiwabatiza jina la ‘Kamati ya Ufundi’ wakiamini ndio wanaoweza kuleta ushindi kwenye timu zao.

 

Pili udanganyifu au kuuza na kununua mechi, pia mwamuzi kuzibeba timu fulani baada ya kupewa kitu kidogo na baadhi ya vigogo wa timu fulani hasa zile kubwa na zenye ushawishi na uchumi mkubwa huku suala hii likiwa la siri. Na hadi sasa watu wengi wanaozungumzia suala hili, wamekuwa wakikosa ushahidi wa wazi na huku wenyewe wanaopenda hayo mambo wakizidi kulibomoa soka la Tanzania kwa kutumia mlungula.

Tatu, utumiaji wa dawa za kuongeza nguvu hasa bangi kwa wachezaji wetu, yaani hili ndilo limekuwa sugu kabisa au niseme ni donda ndugu kwa wachezaji wa Kitanzania hasa wanaocheza Ligi Kuu Tanzania Bara. Wengi wao wanaamini kuwa bila kupata pafu kama wanavyoita wenyewe, basi hawawezi kufanya chochote uwanjani.

Hili linawezeka kabisa kulikomesha kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakiamua kufanya hivyo, lakini inavyoelekea TFF hawataki. Basi tuendelee kuwa nao hao ‘mateja’ kwenye soka na tujue kabisa kuwa tukienda uwanjani kuangalia mechi, basi tunaenda kuwaangalia ‘mateja’ wakipambana.

Kazi kweli kweli. Na nne ni suala la kudanganya umri ambalo leo ndio nitalizungumzia kwa kina. Acha niwe mkweli ingawa wengi wao watachukizwa na mada hii ila ukweli ni ukweli tu huwezi kupingana nao.

Wachezaji wengi au niseme zaidi ya nusu wanaoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara hivi sasa, wawe wa Kitanzania au wale wa kigeni, wamedanganya umri na wengine waziwazi unajua kuwa huyu amedanganya umri maana sura zao zimeshuka na kuonesha umri wake umekwenda ila utasikia eti yeye ni ‘under 20’ (chini ya miaka 20).

Hili suala la kudanganya umri limefanywa kuwa la kawaida sana kama lilivyo suala la uvutaji bangi kwa wachezaji wetu. Katika hili, viongozi wa klabu mbalimbali kuanzia ngazi za chini hadi juu pamoja na wale wa shirikisho la soka kuanzia TFF Makao Makuu hadi kwenye vyama vya mikoa, wanahusika kwenye udanganyifu wa umri wa wachezaji wao.

Wachezaji wenyewe ndio wamekuwa vinara wa kufanya hivyo huku tukiwaachia tu na kuwabatiza jina la chipukizi wakati ni vijeba na ndio maana utaona mchezaji hadumu kwa muda mrefu kutokana na kudanganya umri.

Udanganyifu wa umri wa wachezaji ulishawahi kuligharimu soka la Tanzania wakati ilipogundulika kuwa kiungo Nurdin Bakari alidanganya umri kwenye timu ya Taifa ya chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ na kuzuiwa kushiriki michuano ya Afrika ya ngazi hiyo ingawa timu hiyo ilifuzu kwa fainali zilizofanyika Gambia, lakini hadi leo hatukomi tunaendelea kulikumbatia suala hilo huku tukijua madhara yake.

Yaani wachezaji wengi wa Kitanzania wenyewe baada ya umri wao kwenda mbele, basi wao umri wao huwa unaenda nyuma au unasimama pale pale miaka nenda miaka rudi. Kuna wengine ukiwauliza umri wao, watakujibu unataka umri gani wa kuchezea mpira au wa kwenye hati ya kusafiria au umri wangu halisi.

Na hapo ndipo utajua kiasi gani hili suala tumelichukulia kuwa ni la kawaida sana yaani mtu anapewa hati ya kusafiria ya nchi kwa umri bandia. Hatari sana.

Ninakumbuka kuna wakati baadhi ya wachezaji waliniambia kuwa kuna viongozi wa klabu na baadhi ya makocha wao, ndio wanalazimisha kurudisha umri wao nyuma na hata kuwapa huo umri wa bandia na wanafanya hivyo huku wakijua kabisa wanatenda kosa ambalo linaigharimu nchi na ndio maana hadi leo tunasuasua tu hatuendi kokote kwneye michuano ya kimataifa, maana tuna wachezaji wazee.

Ninakumbuka wakati fulani nikiwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), nilikutana na makocha wawili ambao walikuwa wanasimamia michuano ya Copa Coca-Cola wakiwa kama waratibu wa michuano hiyo. Walinieleza kituko kimoja ambacho sitokuja kukisahau.

Kwamba kulikuwa na mchezaji kutoka mkoa fulani alighushi cheti cha kuzaliwa ila alisahau kubadilisha sehemu ya jinsi yake maana yeye ni mvulana ilitakiwa cheti hicho kiandikwe ‘male,’ basi yeye sehemu hiyo ikawa imeandikwa ‘female’ kwamba yeye ni msichana.

Moja kwa moja wakajua kuwa mchezaji huyo amedanganya umri, wakachukua uamuzi wa kumfuta kushiriki mashindano hayo nadhani yalikuwa ni mashindano ya mwaka 2009. Sasa hapo utaona ni namna gani viongozi wa soka hadi wa ngazi ya mikoa wanavyohusika kwenye udanganyifu huu na hao hao utawaona wakiwa mbele ya vyombo vya habari eti wakijifanya ni wasafi kwenye harakati za kukuza soka kumbe ni uongo mtupu.

Kisa kingine, nakumbuka kuna mchezaji mmoja alikuwa akichezea moja ya timu kubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na timu ya Taifa ‘Taifa Stars,’ akihojiwa na chombo cha habari alianza kueleza historia yake ya soka katika kudanganya kwake ukipiga hesabu, basi ilionesha kuwa yeye alianza kucheza Ligi Kuu akiwa na umri wa chini ya miaka 16. Jambo ambalo kwa hakika halikuwa kweli.

Kitu kingine watu wanashindwa kutofautisha mchezaji chipukizi na yule aliyechelewa kuanza kucheza Ligi Kuu na hilo lipo sana maana wachezaji wengi wanaoitwa chipukizi, sio kweli ni chipukizi, bali wamechelewa tu kuanza kucheza michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na hilo lipo wazi na wengi tunalijua.

Wachezaji hao wengi wanaobatizwa jina la uchipuzi, tumekuwa tukiwaona wakiwa wanacheza mashindano mbalimbali kwenye mitaa yetu kama vile mashindano ya kuwania mbuzi au ng’ombe, tena kwa muda mrefu tu ila akianza kucheza Ligi Kuu mchezaji huyo hubatiwa jina la mchezaji chipukizi. Hapo ninashindwa kuelewa chipukizi au yoso ni yupi ni yule mwenye umri mdogo au yule aliyechelewa kuanza kucheza Ligi Kuu.

Mimi ninawasi wasi hata hao wachezaji walioteuliwa hivi karibuni kuandaa timu ya Taifa ambao wapo Tukuyu mkoani Mbeya, wengi wao watakuwa wamedanya umri tu maana kwa kuwa hawachezi Ligi Kuu, basi tunawachukulia kuwa ni wachezaji chipukizi wakati sio kweli kumbe umri umekwenda na huku wengine wakiwa na umbile dogo, basi tena wanaendelea kutudanganya tu.

Kwa ujumla, ufike wakati hili suala litazamwe kwa jicho la mbali na lisiwe jambo la kawaida wakati tunazidi kujipoteza na pia hili liwe somo kwa TFF na viongozi wote wa klabu hadi makocha wenyewe wapambane kupinga udanganyifu wa umri kwa wachezaji wetu maana kufanya hivyo ni kujimaliza.

Tumechoka na vijeba ambao wamebatizwa jina la chipukizi wakati ni vibabu. Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi Mtanzania anayesoma China. Anapatikana kwa anuani za evancemhando@gmail.com, mobile +8615180191494 au Instagram: Mo1188.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Mo van der Mhando

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi