loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Viongozi wa dini waaswa kuombea amani

Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilalalisema hayo juzijijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Huduma cha Mwadhama Laurean Kadinali Rugambwa kilichopo katika Kanisa la Mtakatifu Petro. Dk Bilal alisema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kufanya waumini wao kutambua umuhimu wa tunu iliyoletwa kwa wanadamu waweze kukabiliana na majukumu ya maisha yao.

“Viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa ya kuwafanya waumini wenu kutambua umuhimu wa tunu hii,”alisema DkBilal hivi karibuni jijini Dar es Salaam.Kituo hicho kimegharimu Sh bilioni tatu. Alisema mafanikio ya kukamilika kwa Kituo cha Kadinali Rugambwa ni matokeo ya mshikamano na upendo uliojengeka ndani ya nchi.

“Nawakumbusha Watanzania wenzangu wote kuendeleza moyo huu wa kuchangia maendeleo yetu katika sekta mbalimbali,”alisema Makamu wa Rais.

Alisema kufunguliwa kwa kituo hicho ni kielelezo tosha cha kukumbuka historia ya Kadinali Rugambwa ya unyenyekevu uliotukuka, kwani kiongozi huyo wa dini alipenda Tanzania na watu wake na alihubiri amani ndani na nje ya nchi.

“Nawapongeza kwa kuchagua jina hili, Kadinali Rugambwa alikuwa kiongozi wa kipekee katika kueneza suala la amani kwa Watanzania na hii ndio njia bora ya kuwaenzi viongozi hawa,”alisema.

Aidha alisema kuzinduliwa kwa kituo hicho Oktoba 14, mwaka huu,ni kielelezo cha kuenzi amani, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania kwa kuwa hiyo ni siku ambayo Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere anatimiza miaka 15 tangu kufa kwake.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo mbali na kumshukuru Makamu wa Rais alisema ameamua kuita kituo hicho jina la Kadinali Rugambwa kutokana na kiongozi huyo kuipenda nchi yake na kuunganisha Watanzania.

“Nilipofuatwa na wazee wa Kanisa la Mtakatifu Petro kutoa jina la kituo hiki niliwaambia kituo kitaitwa Kadinali Rugambwa Social Center,” alisema.

Mwenyekiti wa Parokia ya Mtakatifu Petro, Dk Adelhelm Meru alisema hatua kubwa iliyofikiwa mpaka kukamilisha kituo hicho ni kutokana na mshikamano uliooneshwa na waumini wa kanisa hilo kujitoa kwa hali na mali.

Uzinduzi wa kituo hicho chenye ofisi, maduka na kumbi mbili za mikutano, ulitanguliwa na ibada ya misa takatifu iliyoongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi