loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Viongozi wa Vicoba miungu-watu waepukwe

Miongoni mwao ni waroho wa fedha kiasi kwamba wamekuwa wakikodolea macho fedha za wakopaji na kutaka kupewa chochote, kwa madai kwamba wao ndio waliofanikisha mikopo hiyo.

Mratibu wa Taasisi inayojishughulisha na Malezi ya Vijana, Ukimwi na Maendeleo ya Jamii (UYACODE), ambayo inatoa mafunzo kwa vikundi vya Vicoba, Aldo Mfinde, amekemea tabia hiyo ya viongozi hao na kuwataka waache mara moja.

Amekemea vitendo hivyo wakati wa mkutano wa kufungua mwaka wa wenyeviti, makatibu na watunza hazina wa vikundi vya Vicoba katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulioshirikisha viongozi zaidi ya 400, ulikuwa wa kukumbushana majukumu ya viongozi hao, namna ya kujaza vitabu, fomu, kumbukumbu za wanachama na kuweka mikakati mipya kwa mwaka huu.

Mfinde ambaye taasisi yake imefundisha zaidi ya vikundi 600 vinavyounda Vicoba katika Jiji la Dar es Salaam na Pwani, anawataka viongozi wawe waaminifu. Mfinde pia imeshafungua Vicoba katika mikoa mingine 12 na kuifikia jumla ya mikoa 14.

Anasema viongozi miungu-watu, wanatakiwa kuachana na mtindo huo kwani unachangia katika kuleta vurugu kwenye Vicoba na kutoelewana baina ya viongozi na wanachama.

“Baadhi ya viongozi miungu-watu, wanaotaka kuabudiwa na kusujudiwa, na kukodolea macho fedha za wakopaji, watatakiwa kuogopwa kama ukoma na waache mara moja,” anasema Mfinde.

Anasema baadhi ya viongozi wakipata madaraka wanajisahau, hawatekelezi wajibu wao wa kuitisha mikutano ili wanachama wajue historia ya vikundi vyao, mafanikio na changamoto zinazovikabili na mbaya zaidi hawasomi hata taarifa za fedha.

Viongozi hao wanachoangalia ni kufukuzia fedha za wanaokopa mikopo ili wapewe, vitendo ambavyo vinaleta vurugu tupu ndani ya vikundi hivyo.

Anasema katika vikundi vingine viongozi wake wanaingiliana madaraka hasa kati ya wenyeviti na makatibu, kila mmoja anajiona mkubwa, jambo ambalo limekuwa kama kirusi ndani ya Vicoba.

Anasema imefikia hatua baadhi ya viongozi hawasalimiani na kusababisha kurudisha nyuma maendeleo ya kikundi. Taasisi ya Uyacode, imefanya ukaguzi kwenye baadhi ya vikundi na kubaini madudu mengi.

Katika utafiti huo imegunduliwa pia kwamba baadhi ya viongozi ni wazembe kujaza vitabu, wanafutafuta, hawatunzi kumbukumbu za wanachama na kwamba wakati umefika ambapo si Uyacode pekee itakayofanya ukaguzi bali Serikali kupitia dawati la Uwezeshaji Biashara kutoka katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Fedha inayosimamia vikundi vya ujasiriamali vikiwamo Vicoba kukagua.

Mfinde anasema, taasisi ya Uyacode imefanya kazi ya ukaguzi kwa miaka 12 tangu kuanzisha kwake Ukonga, Dar es Salaam, lakini tangu 2006, kampeni ilikuwa kutafuta vikundi hivyo vipo wapi na sasa inajulikana vipo chini ya Wizara ya Fedha. Anasema kwa sasa wizara hiyo inataka kujiridhisha kujua kuna nini kwenye vikundi hivyo.

Mfinde amesema Wizara ya Fedha imefanya ukaguzi wa majaribio kwenye baadhi ya vikundi na kubaini kwamba mahesabu ya Vicoba hayajakaa sawa, hivyo imeamua kufanya ukaguzi rasmi kwa kuanzia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga.

Mratibu huyo anasema, ukweli ni kwamba baadhi ya viongozi wamekuwa hawaweki kumbukumbu vizuri na wanathubutu hata kuidanganya benki ya Twiga ambayo ndiyo inayotunza fedha za vikundi kwa kupeleka kiwango kidogo cha fedha benki na nyingine kufanyia shughuli zao.

Mfinde ametoa mifano michache kuonesha namna baadhi ya viongozi ambavyo wamekuwa wakiwadanganya wanachama kwamba wamepeleka fedha benki kiwango kikubwa, kumbe hawajapeleka. Wamekuwa wakifanya hivyo kwa kufoji nyaraka.

Mgeni rasmi katika mkutano huo, Kaimu Msimamizi wa Shughuli za Wateja katika Benki ya Twiga, Joseph Ndunguru ameungana na Mfinde kwa kuwataka viongozi wa Vicoba waliopewa dhamana ya kuweka na kutoa fedha benki kuwa waaminifu kwa kutoa na kuweka kile ambacho wametumwa na vikundi vyao badala ya kwenda kinyume na walichopangiwa.

“Wakati mwingine baadhi ya viongozi wasio waaminifu wametumia nafasi hii na kuthubutu kufoji hata nyaraka za fedha na kuandika kiwango ambacho hawajatumwa na wana vikundi wao, jambo ambalo si jema kwani linahatarisha maisha kwa wahusika,” anasema Ndunguru.

Ameviasa vikundi hivyo kuzingatia kanuni walizojiwekea kwani Serikali kwa upande wake, imeamua kuweka mkazo kwenye mpango wa Vicoba na ndio maana mwaka huu imeamua kufuatilia mwenendo wa fedha wa vikundi hivyo kwa karibu.

Serikali itaratibu ili kuwajengea uwezo na kuwapa fursa ya kuviwezesha ili vikue kwa lengo la kujipatia maendeleo na kwa Taifa lao.

Ndunguru amesema, kazi ya benki hiyo ni kuhakikisha Vicoba vinasimamia kwa uhakika miradi inayopata mikopo kutoka katika benki mbalimbali nchini ikiwamo yao na kuirejesha kwa wakati ili vijenge imani kwenye taasisi za fedha kwamba Vicoba vinakopesheka na vinarudisha mikopo kwa wakati.

Ngunduru ameahidi kwamba benki yake itaendelea kuwa bega kwa bega na wana-Vicoba popote nchini, ili kuhakikisha vikundi hivyo vinapata tija kubwa katika kumiliki mtaji na riba kutokana na kujiwekea akiba.

Benki hiyo imekuwa bega kwa bega katika kuanzishwa kwa Vicoba pote nchini na tayari inahudumia vikundi hivyo katika mikoa 14 na mkakati wake ni kuhudumia vikundi vingine katika mikoa 11 iliyobaki.

Mwanzoni mwa mwaka huu Mratibu Mfinde akiwa na benki hiyo wamefika mkoani Ruvuma katika Wilaya ya Nyasa na sasa wanakwenda mkoani Kigoma, kuhamasisha wananchi kuanzisha Vicoba na kuweka akiba katika Benki ya Twiga ambayo inaviamini na kuvisaidia ili kuhakikisha vinakua na baadaye kuwa taasisi za fedha.

Mkutano huo uliokuwa chini ya uenyekiti wa Agnes Mangula umekuwa chachu ya kuwakutanisha wenyeviti, makatibu na watunza hazina wengi zaidi kuliko makisio ya watu wastani wa watu 300.

Katibu wa mkutano alikuwa Shaban Mwasa huku wajumbe wakiwa ni Egidius Kamara, Shaweji Koroboi, Mariam Magafu, Elizabeth Tossi na Arabi Najumbwe. Mkutano huo wa siku moja pia umetumika katika kupeana mbinu baina ya viongozi wakongwe na wapya waliochaguliwa mwaka jana.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi