loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Viongozi wanaoshindwa kusimamia sheria wabanwe

Tunasema wabanwe kwa kuwa Rais Kikwete alikerwa na uharibifu wa mazingira, ikiwamo kuharibu vyanzo vya maji katika mlima wa Uluguru huku viongozi wa Manispaa wakishindwa kuchukua hatua stahiki.

Rais Kikwete alisema woga wa viongozi hao unawapa mwanya wananchi kukiuka sheria na kufanya wanavyotaka, kwa kuwa wasimamizi wa sheria hiyo hawafanyi kazi yao.

Tunajiuliza, hivi hawa viongozi wanasubiri kukemewa ndio wafanye kazi wakati wakijua wapo pale kusimamia sheria?

Kwa kuwa sheria zipo, wasimamizi wapo na wanalipwa mishahara, ni jambo la kushangaza kwa kuwa, waliotoa kilio hicho ni baadhi ya wananchi ambao hawataki kuona uharibifu ukiendelea kufanyika huku viongozi waliopewa dhamana nao wakiangalia bila kuchukua hatua yoyote.

Kwa mujibu wa wananchi hao waliotoa kilio cha muda mrefu kwa Rais Kikwete, wapo watu ambao wamegeuza vyanzo vya maji katika mlima huo kulima, kupeleka mifugo na wengine kudiriki kujenga kandokando ya vyanzo hivi.

Hii ni ubinafsi wa makusudi kwa kuwa watu wachache wanaamini wao ndio wao na wengine hawana chao katika rasilimali ambazo ni mali ya Watanzania wote.

Tunaamini yapo maeneo mengi hapa nchini ambayo yana sura kama hiyo na wanaohusika hawachukui hatua yoyote hadi viongozi wa ngazi ya kitaifa wafike na kukemea au kutoa agizo.

Sheria ni msumeno, pale ambapo viongozi wanazembea kuchukua hatua, ina maana nao wanawajibika kupewa adhabu stahiki. Kuharibu vyanzo vya maji kwa makusudi na ubinafsi ni kuua taifa kwani wachache wanataka kufaidi wakiacha walio wengi wakiumia.

Hii haiwezi kuvumiliwa kwa aina yoyote na tunadhani, agizo hilo lisiishie kwa viongozi wa Manispaa ya Morogoro bali na wengine wapime uadilifu wao mahali walipo na kutumia sheria zilizopo kuhakikisha wanalinda mazingira vikiwamo vyanzo vya maji.

Tuna milima mingi ambayo kwa njia moja ama nyingine, mazingira yanayozunguka milima hiyo ambayo kwa kawaida huwa ardhi yenye rutuba ikiwa na miti yenye kulinda udongo uendelee kuwa wa rutuba na kuwezesha kutunza vyanzo vya mito inayoanzia katika milima hiyo hukatwa na hakuna kiongozi anayechukua hatua.

Rais ametaja woga na udhaifu bila kutafuna maneno kwa kuwa viongozi wengi wana nasaba na wahalifu, hivyo wanakuwa woga kutumia nafasi zao kwa sheria zilizopo kuwabana, matokeo yake wahalifu wanatumia nafasi hizo kufanya watakavyo.

Huo ni udhaifu mkubwa na woga usikubalike kwani kama sheria zilipo hazitumiwi, tunakaribisha majangwa ya kujitakia.

Agizo la Rais linahitajika kufanyiwa kazi na kila kiongozi katika eneo alipo ili kurudisha hali ya hewa katika nyakati zile za nyuma ambapo mila na desturi zilizokuwapo zilizuia watu kukata miti kwenye vyanzo vya maji huku vikikingiwa vifua kwamba kuna matambiko ya mizimu.

Hivi kweli tunahitaji kutumia njia hiyo badala ya sheria kuwabana watu wanaofanya uhalifu?

Tuache woga. Kwa kiongozi makini kuitwa dhaifu na mwoga mbele ya kadamnasi, ni adhabu tosha na tuamini wahusika watalichukulia agizo hilo kwa umakini mkubwa huku tukishauri na wengine katika maeneo yao kuhakikisha wanatumia sheria kulinda mazingira yanayowazunguka hasa vyanzo vya maji.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi