loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Vishoka’ wasivuruge usambazaji umeme vijijini

Kitendo cha kuzuka matapeli kutumia mwanya wa wananchi kutokuelezwa vyema namna ya kupata huduma hiyo kunastahili kulaaniwe; na pande zinazohusika hazina budi kufanyia kazi habari hiyo ili vishoka hawa wanaowarubuni wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kuwadang'anya kwamba wanaweza kuwapatia huduma zinazotolewa na shirikia hilo watiwe mbaroni.

Habari hiyo ambayo imewanukuu wananchi mbalimbali wa kijiji cha Mkoja wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wakilalamika kutapeliwa na vishoka baada ya kuwarubuni kuwa wangeweza kuwaunganishia umeme kwa gharama kati ya Sh 100,000 na Sh 300,000 huku gharama halisi ya huduma hiyo ikiwa ni Sh 32,900 tu, ni njama za wazi za kuzuia juhudi za serikali kusambaza nishati.

Sisi tunasema kwamba hakuna ubishi vishoka hawa wanatibua mipango ya serikali ya kuwaleletea wananchi wake huduma endelevu ya kupata nishati ya umeme kwa maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini kama walivyo wenzao wa mijini.

Ni wazi kwamba uchu huu wa kujipatia kipato kwa njia ya udanganyifu ni hatari na si sahihi. Kutokana na ukweli huu, tunatoa mwito kwa Tanesco, kuchukua hatua za kuwasaka na kuwatia mbaroni vishoka hao kwa kushirikiana na vyombo vya dola, wakiwemo polisi ili wahusika hao wapatiwe adhabu wanayostahili kwa vitendo hivyo vya ambavyo ama hakika ni hujuma kwa maendeleo ya wananchi.

Lengo la serikali ni kuwapatia huduma hiyo wananchi kwa gharama nafuu, hivyo hatua yoyote ya kuongeza gharama ya huduma hiyo kutoka Sh 32,900 hadi kufikia kati ya Sh 100,000 hadi 300,000 ni wizi wa hali ya juu na haitakiwi kamwe kufumbiwa macho.

Lakini ni kweli kwamba Tanesco na polisi pekee hawataweza kudhibiti wahalifu hao ambao katika hali ya kawaida tunaishi nao katika maeneo yetu. Kwa hili tunaomba wananchi washirikiane kwa pamoja kwa maana ya kuwa wabia wa vita dhidi ya vishoka.

Tanesco, polisi na wananchi tuzungumze lugha moja ya kupambana na wahalifu na wahujumu hawa wa maendeleo ya wananchi wetu walipo vijijini.

Ni vizuri kukumbushana pia kwamba iwapo juhudi za kusambaza umeme vijijini zitafanikiwa ni wazi kwamba hata suala la uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji vitapungua kwa sababu kiwango cha ukataji miti kwa ajili ya kujipatia nishati inaweza kupungua na kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa kutakuwepo na vyanzo mbadala vya nishati kwa maana ya umeme.

Mabadiliko ya tabia nchi ambayo kila mmoja wetu hapa nchini, Afrika na duniani kwa ujumla anayashuhudia iwe ni kichocheo cha kuwadhibiti wenzetu wanaotaka tuendelee kuharibu mazingira kwa kutunyima fursa za kupata umeme. Hili tulikatae katakata kwa vitendo.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi