loader
Picha

Waajiri, waajiriwa wajipime Mei Mosi hii

Viongozi pia wajibu wenu mkubwa ni kulinda heshima na kudumisha nidhamu ya kazi.” Ninaukumbuka wimbo huo leo wafanyakazi nchini wanapoungana na wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi maarufu kama Mei Mosi inayoadhimishwa kitaifa Iringa ambapo mgeni rasmi ni Rais John Magufuli.

Wimbo huo unanirejesha kwenye moja ya mashairi ya mtunzi Egyne Emmanuel (Simba wa Yuda), lililopo uk. 14 wa gazeti hili, liitwalo, ‘Mei Mosi Tujipime’ pale mshairi anaposema:

“Tukafanye uchunguzi, Wenyewe tukajihoji, Wapi tulikuwa lezi, Ukashuka ukuaji? Tuzidishe mazoezi, Uongezeke mtaji, Tujipime utendaji, Siku ya Wafanyakazi.”

Kimsingi, Siku ya Wafanyakazi Duniani inatukumbusha kwamba uhusiano baina ya mwajiri na mwajiriwa ni sawa na haki na wajibu; chanda na pete; na kuku na yai yaani, bila kuku, hakuna yai na bila yai, hakuna kuku.

Kadhalika, bila haki hakuna wajibu na bila wajibu hakuna haki. Vivyo hivyo, bila mwajiri, hakuna mwajiriwa na bila mwajiriwa, hakuna mwajiri, hivyo uhusiano uliopo unapaswa kuimarika ili kuwapo tija na ufanisi pande zote.

Ndiyo maana ninasema kila Mtanzania ajipime; ajitafakari na kutathmini kazi aliyoifanya kwa mwaka mzima kujiwekea sera na mikakati ya kukuza mafanikio yaliyopo kwa ustawi wa umma. Kila mfanyakazi anapaswa ajiulize kama kweli anatenda haki kwa mwajiri wake na kadhalika mwajiri, awe mtu binafsi au taasisi, ajipime pia.

Kwangu, kumtendea haki mwajiri ni pamoja na kuhudhuria kazini, kuwahi eneo la kazi na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ukiepuka visingizio ili usifanye ipasavyo majukumu yako.

Kutomtendea haki mwajiri ni kutumia vibaya rasilimali za ofisi kama muda na vifaa, kukosa ubunifu na kuficha udhaifu wako katika majungu kuanzia ngazi moja kwenda nyingine.

Pia waajiri wanadaiwa wajibu wa kuwatendea haki waajiriwa wakiwamo wa sekta binafsi.

Wahakikishe waajiriwa wanapata haki zao ipasavyo kwani mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake.

Wasiwatumikishe waajiriwa wao kihuni kwa kazi zisizoendana na malipo ya kazi na usalama kazini na hata katika maisha yao. Sio siri, wapo baadhi ya waajiri wanaofanya maeneo ya kazi sehemu ya kunyonya waajiriwa na “kuwatapeli” kwa kutowalipa mishahara yao hadi walazimishwe na “sauti ya sheria za kazi.”

Kimsingi, mwajiri yeyote anatakiwa atende haki kwa kuweka mazingira rafiki kwa wafanyakazi kuonesha ubunifu wao na kufurahia kuwapo kazini ili watimize vema majukumu yao kazini.

Wakati tukijipima, tuzingatie ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika kuzalisha na kutoa huduma sambamba na kujenga mshikamano wa dhati kati ya vyama vya wafanyakazi na wanachama wao kwa kuzingatia kanuni, sheria na nidhamu; weledi, uadilifu na uwajibikaji; utawala bora, ulinzi na usalama wao kazini! Mara nyingi maadhimisho haya yamekuwa nafasi ya wafanyakazi kudai nyongeza ya mishahara, hali nzuri na mazingira bora ya kazi.

Yote haya yanaweza kufikiwa kama kutakuwa na tija na uzalishaji wa kutosha. Ufanisi kazini utatokana na mchango makini wa wafanyakazi kwani wizi, ufisadi, udanganyifu wa kiwango cha elimu, hujuma na tamaa huua ufanisi kazini.

UKOSEFU wa vibanda vya kujihifadhi wasafi ri wakati wa wakisubiri ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi