loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wabunge walivyomlilia Mandela

Wabunge walivyomlilia Mandela

Taarifa za kifo hicho zimepatikana wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likiendelea na mkutano wa kumi na nne, ambapo kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge siku ya Ijumaa, Spika wa Bunge aliomba kusimama kwa dakika tano kumuombea kiongozi huyo.

Baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu alisimama na kuomba mwongozo na kuhoji kutokana na kifo hicho cha kiongozi huyo muhimu kwa bara la Afrika, kwanini Bunge bado linaendelea na shughuli zake badala ya kuahirisha?

Ndipo, Spika wa Bunge akasema kwa kufuata sheria na kanuni za nchi siyo rahisi Bunge kuamua kuahirisha vikao lakini kwa kutambua umuhimu wa Mandela watatoa azimio rasmi la Bunge. Siku ya pili ya vikao hivyo vya Bunge, liliamua kusitisha shughuli zote na kutoa azimio kufuatia kifo cha Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela kwa kumuenzi kwa kudumisha umoja, amani na mshikamano ili kuleta maendeleo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Edward Lowassa aliwasilisha azimio hilo la kuungana na Nchi ya Afrika Kusini kuomboleza kifo cha muasisi, mpinga ubaguzi wa rangi na Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini.

Anasema Mzee Mandela aliyatoa maisha yake kupigania uhuru wa Waafrika na kupinga ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiendeshwa na utawala wa wazungu wachache nchini Afrika Kusini hali iliyofanya kufungwa katika Gereza la Robben tangu mwaka 1964,” anasema.

Anatoa historia ya Mzee Mandela aliyezaliwa mwaka 1918 na kufungwa kwa miaka 27 akitetea haki za watu weusi kwa kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo.

Anasema baada ya kutangazwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 1990, alionesha ukomavu wa uongozi kwa kusamehe wote waliomtesa gerezani na kuwaunganisha watu wa nchi hiyo weusi na weupe. Lowassa anasema mwaka 1999 alistaafu mwenyewe urais na kurithisha madaraka kidemokrasia hivyo kwa azimio hilo Bunge litamuenzi kwa utu na kuthamini wengine.

Anasema Bunge linaazimia kuungana na familia yake, wananchi wa Afrika Kusini na dunia nzima katika kuomboleza msiba wa Hayati Nelson Mandela kwani amekufa lakini ataendelea kuishi katika mioyo yetu kwa miaka mingi. “Tuendelee kumuenzi kwa kuiga na kufuata nyayo zake za kuwa kiongozi mzalendo aliyeithibitishia dunia kujali utu na kuthamini wengine, mpigania haki na usawa kwa binadamu na kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi,” anasema.

Wakichangia na kuunga mkono azimio hilo, lililopitishwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye alitangaza kulipeleka katika Bunge la nchini Afrika Kusini, wabunge waliungana katika kuomboleza na kusema bara limepoteza mtu muhimu. Wakichangia azimio hilo, wabunge wametaka kufuatia kifo cha mpigania uhuru huyo kujifunza kwa kutolipiza kisasi kwa kusameheana na kuvumiliana katika kila jambo hususan suala la Katiba na mijadala mbalimbali.

Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni, Injinia Habibu Mnyaa, (CUF) anasema kufuatia kifo cha Mandela, amefaulu kwa kuunganisha mataifa yote duniani hasa waliochukia unyanyasaji bila kujali wapo umbali gani. “Hata baada ya kifo pia ameunganisha dunia kwa nchi zote hata zenye mitazamo tofauti kupeperusha bendera nusu mlingoti na kuungana kuomboleza,” anasema Mnyaa.

Anasema pia Mandela alikuwa mwanamichezo na aliyependa michezo jambo ambalo wanamichezo wote wanaomboleza kifo hicho. Anasisitiza kuwa pia alikuwa mtu wa misamaha kwa watu wote jambo ambalo viongozi wengi hawana jambo ambalo ni karama ya pekee kwani viongozi wengi hawawezi.

Anasema kuna baadhi ya Wazanzibari ambao katika kipindi cha miaka 50 iliyopita bado hawajasamehe huku akitaka wabunge nao kusamehe wapinzania wao majimboni na kuungana kufanya kazi za maendeleo.

“Ni vema kuwa na moyo kama Mandela kuondoa migogoro na kutokuelewana miongoni mwa jamii na kusimamia Umoja wa Kiafrika.” Amesema. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Mahadhi Juma Maalim anasema Mandela ataendelea kukumbukwa daima kwani urafiki wa nchi mbili uliimarishwa naye pamoja na Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere.

Anasema kwa azimio hilo la Bunge ni kielelezo cha kuthamini ukaribu baina ya nchi hizo mbili kwa kuthamini ushirikiano wa nchi hizo mbili Serikali itamuenzi kwa kuendeleza ushirikiano wa nchi hizo mbili . Naye, Mbunge wa Viti Maalum, Magreth Mkanga, (CCM) anasema hajui kama katika miaka 20 atatokea mtu kama Mandela Afrika mwenye ushupavu na ujasiri huku akiweka msisitizo katika kusamehe.

Mbunge wa Nyamagana, Hezekiah Wenje (Chadema) alianza kwa kusema Tanzania imempoteza rafiki wa kweli, shujaa na mwenye upendo wa kweli. Anasema msamaha wa Mandela unafundisha kuwa mtu akiingia madarakani sio vita na kulipiza visasi bali kusamehe na kuunganisha watu na kutoa mafunzo kuwa kuingia madarakani siyo vita bali kuwaunganisha na kutumikia watu.

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, (NCCR-Mageuzi) anasema alikuwa nyota pekee na hakuna aliyeunganisha dunia kama yeye na kutaka wasiasa vijana kusoma ili kuwa kama Mandela na zaidi. Anasema kwa kumuenzi mwanamapinduzi huyo taifa linatakiwa kuondoa chokochoko za ubaguzi wa kidini kwa kutumia hekima na kusoma maisha yake ili kuondoa ubaguzi huo.

“Kwa kweli Afrika simuoni mtu mwingine mwenye karama za pekee kama Mandela na ikiwa watu wote vijana na wazee tukiungana kumuenzi kwa uongozi na matendo yake , Afrika itakuwa nchi ya amani na upendo,” anasema Kafulila.

Jambo lililoungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) anayesema hata waliowahi kumuita gaidi sasa wanamlilia kwani aliunganisha dunia nzima wakiwemo hao hasa mataifa ya Magharibi.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi