Rai hiyo imetolewa leo Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Maria Bilia wakati wa ufunguzi wa mkutano kwa watendaji wa wizara hiyo kuhusu masuala ya ushindani kwa lengo la kumlinda mlaji na mapambano dhidi ya bidhaa bandia.
Alisema masuala ya ushindani wa kibiashara ni wigo mpana unaopaswa kupata ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali na kwamba kwa kuitegemea Tume ya Ushindani peke yake hakutosaidia kumaliza tatizo hilo kutokana na uchache wa watendaji wa tume ukilinganisha na idadi ya wafanyabiashara suala alilosema linahitaji jitihada za wafanyabiashara hao.
“Tume peke yake haiwezi kusimamia ushindani bila kushirikiana na wadau wengine, ni vyema kwa nafasi yao wafanyabiashara wakajenga tabia ya kutoa taarifa katika tume pale wanapoona kuna kasoro za kisheria katika maeneo ya shughuli zao hatua itakayoirahisishia tume kufanya kazi yake,” alisema Bilia.
Aidha aliwataka watendaji wote wa tume hiyo kufanya kazi yao kwa weledi na umakini utakaowezesha mapambano ya kiushindani licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya rasilimali fedha.
Awali akizungumzia utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya tume hiyo ya ushindani, Makamu Mwenyekiti wake Kanali mstaafu Abihudi Nalingirwa, alisema ipo haja ya msingi ya kuhakikisha masuala ya utoaji elimu kwa walaji wa Tanzania pamoja na utanzuaji wa malalamiko yao unafanyika kwa haraka kwa lengo la kutomgharimu mlalamikaji.