loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wajitosa kutoa taarifa za hali ya hewa, soko kwa wakulima

Ni kutokana na umuhimu wa kilimo katika kuongeza ukuaji wa uchumi, serikali iliamua kuanzisha mpango wa Kilimo Kwanza kama njia ya kuongeza kasi ya kilimo. Hata hivyo, bado kuna changamoto kadhaa ambazo zinawaandama wakulima katika kufanikisha kilimo chao, moja wapo ikiwa ni elimu inayohitajika kwa kilimo cha kisasa.

Elimu hii ni pamoja na kujua hali ya hewa, na hasa kwa vile kilimo chetu bado kinategemea mvua pamoja na ardhi inayofaa kwa kulima zao fulani. Changamoto nyingine ambayo wakulima wamekuwa wakikutana nayo ni soko la kuuza bidhaa zao kwa bei nzuri. Sambamba na hilo, inaaminika kwamba soko linaweza kuwepo lakini tatizo likawa taarifa, kwa maana ya kujua ni wapi wapeleke mazao yao na kuyauza kwa bei gani.

Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo Tanzania ina fahamu tatizo la wakulima kujua taarifa kuhusu soko na hivyo imeona haja ya kujikita katika kuwasaidia wakulima hapa nchini katika eneo la utafutaji wa soko la bidhaa zao na namna ya kuuza. Kwa mantiki hiyo, huduma ya Tigo Kilimo imeanzishwa kwa kampuni hiyo, lengo ikiwa ni kutoa elimu zaidi kwa ajili ya kilimo bora na pia namna ya kufikisha mazao sokoni.

“Tigo Kilimo kama zilivyo huduma zingine za Tigo, inalenga kuhamasisha maendeleo ya wateja wake kupitia ubunifu wa teknolojia ya simu za mkononi. Mkulima ambaye ni mteja wa Tigo ataweza kuelimika juu ya kilimo cha kisasa kupitia simu yake ya kiganjani popote alipo,” anasema Meneja wa Programu Maalumu za Tigo, Yaya N’djore.

Anasema Tigo imeamua kutazama maendeleo ya mkulima na kuona eneo ambalo inaweza kuchangia katika kampeni za Kilimo Kwanza, katika harakati za kuisaidia Serikali kuwainua wakulima nchini. N’djore anasema huduma hiyo imeanza kutumika katika baadhi ya mikoa nchini kuwasaidia zaidi wakulima katika mahitaji yao makuu ambayo ni namna ya kulima kilimo bora na cha kisasa na pia kujua bei ya soko la bidhaa zao kila wanapohitaji.

“Wakulima ni jamii ambayo ni kama imetengwa kwa sababu wakulima wako vijijini na hivyo sio watu wengi wanawafikiria moja kwa moja kama ambavyo Tigo imeamua kuwatupia macho,” anasema N’djore. Mikoa ambayo inaweza kunufaika na huduma hiyo kwa sasa anaitaja kuwa ni mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Shinyanga, Mwanza na Kigoma.

N’djore anasema ili kujiunga na huduma hiyo, mteja wa Tigo atatakiwa kujiunga katika huduma ya kila wiki, ambayo itamuwezesha kupata taarifa muhimu kwa kupiga *148*14#. Anasema kupitia huduma hii mkulima ataingiziwa taarifa za kilimo mara tatu kwa wiki na huduma hii gharama yake ni sh. 259 kwa wiki.

Taarifa zitakazopatikana ni pamoja na taarifa za hali ya hewa ya kila eneo husika, ambapo mkulima anaweza kutaja eneo alilopo na kupata taarifa hizo, taarifa ya ardhi ya eneo mkulima alipo na aina gani ya mbolea itafaa kwa ardhi yake. “Taarifa hizi mteja atapewa kila atakapotuma ujumbe wa kuuliza baada ya kujiunga na taarifa ambazo Tigo inapokea kutoka kwa wataalamu wa kilimo mara tatu kwa wiki,” anasema N’djore.

N’djore anasema hali hii inawafanya wakulima wengi zaidi kutumia huduma hata katika maeneo ambayo hawajafikiwa na mawasiliano ya Tigo. “Tumeshangaa katika kufuatilia namna watu wanaotumia huduma hii, kuna maeneo hakuna mawasiliano ya Tigo lakini watu wana laini zao za Tigo wanakwenda kufata mawasiliano yanakopatikana wanaweka laini zao na kupata huduma hii ya taarifa muhimu za kilimo.”

Anasema alipowahoji wakulima hao kwa nini wanakuwa na laini za Tigo wakati mawasiliano hayajawafikia katika kijiji chao walieleza kuwa huwa wanafuata minara ya Tigo kwa ajili ya kupata taarifa za kilimo.

“Inapendeza kuona kuna watu wanaohitaji kupata huduma zetu hata kama wako katika mazingira magumu kiasi gani,” anasema N’djore. N’djore anasema Tigo kilimo inatoa taarifa za kilimo kutoka kwa watu wa Idara ya Hali ya Hewa (TMA) na kwamba kampuni hiyo kwa kushirikiana na TMA watakuwa wakiwapa elimu wakulima kwa Tigo Kilimo kuhusu hali ya hewa kwa siku tatu kwa wiki jinsi itakavyokuwa ikibadilika.

Hata hivyo, N’djore anakiri kuwa changamoto kubwa ambayo inaikabili huduma ya Tigo Kilimo ni baadhi ya vijiji kukoa mawasiliano ya mtandao huo na kwamba wana kazi kubwa ya kufikia wakulima wengi zaidi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa huduma hiyo inawafikia watu wengi zaidi.

“Kadiri siku zinavyokwenda tutanunua huduma zetu, kwa sasa Tigo iko katika mikoa yote 30 Tanzania bara na Zanzibar ambapo tuna minara isiyopungua 1603, hii haitoshi kwetu,” anasema. Anasema Tigo ina mpango wa kuongeza minara 1500 na kuisambaa sehemu kubwa zaidi ya nchi ili kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini.

Akifafanua anasema katika maboresho zaidi, Tigo Kilimo, huduma ya kutaka kujua soko la bidhaa za mteja wa Tigo na atauzaje bidhaa zake wao na namna atakavyosafirisha itakuwa ikipatikana kwenye Tigo Kilimo.

“Kwa utafiti tulioufanya wakulima wengi wanahitaji huduma hii kutanuka hasa kuweza kufahamu bei za bidhaa zao sokoni,” anasema. Serikali ikiwa mdau mkubwa, anasema imekuwa ikijitahidi kuweka mazingira ya kilimo katika mfumo ambao utamfanya mkulima anufaike.

Hakuna asiyejua kama kilimo ndiyo uti wa mgongo wa taifa, uchumi hauwezi kukua bila kuwa na kilimo cha kisasa na chenye tija kwa kuona hilo, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo inasambaza huduma hii ya Tigo Kilimo kutoa mchango katika sekta hiyo nyeti.

Zipo changamoto nyingi Serikali imekuwa ikiwashauri wadau mbalimbali kuunga mkono kampeni ya kukuza kilimo lengo likiwa ni kuinua uchumi wa nchi na pia kuboresha maisha ya wananchi na hasa wakulima.

“MTU niliyefanya naye mahojiano alikuwa anafanya kazi kwenye ...

foto
Mwandishi: Regina Kumba

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi