loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wajumbe wa Ukawa rejeeni Bungeni

Katika salamu zao kwa Watanzania, hususani Waislamu, viongozi wa dini hiyo nchini kote, walitoa mwito kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuhakikisha kuwa wanaendelea na mchakato wa uandaaji wa Katiba ili kuwapatia Watanzania Katiba mpya na bora.

Kupitia fursa hiyo, viongozi hao wa dini ya Kiislamu, waliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliosusa Bunge hilo, kurejea bungeni ili kukamilisha mchakato wa Katiba mpya.

Mathalani, akisoma salamu za Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) katika sherehe za Baraza la Idd jijini Dar es Salaam juzi, Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaji Suleiman Lolila aliwaomba Ukawa kurejea bungeni na kuwapatia wananchi Katiba mpya.

Mbali na salamu hizo za Baraza la Idd, mwito huo ulitolewa pia na mashekhe wa mikoa tofauti nchini, ambao nao waliwasihi mno Ukawa kurejea bungeni.

Alhaji Lolila alisema Bunge Maalumu la Katiba, limepata pigo kwa baadhi ya wajumbe wake (Ukawa), kuamua kususa Bunge hilo.

Alisema Baraza Kuu la Waislamu Tanzania linawasihi wajumbe wote waliotoka nje ya Bunge, warejee mara Bunge litakapoanza shughuli zake ili kuwawezesha Watanzania kupata Katiba yao mpya.

Ukiondoa viongozi hao wa dini ya Kiislamu, viongozi mbalimbali wa dini nyingine, viongozi wa serikali na hata viongozi wa kimila, pia wamekuwa wakitoa mwito kwa Ukawa kurejea bungeni, wakati Bunge hilo litakapoanza vikao vyake mapema mwezi ujao.

Sauti hizi za watu wengi za kuwaomba Ukawa kurejea bungeni, si za kupuuza hata kidogo, bali ni sauti zinazopaswa kupewa uzito na heshima ya aina yake na wajumbe wa Ukawa, kwani kama inavyoaminika mara zote sauti ya wengi hutafsiriwa kama ni sauti ya Mungu.

Ni kweli kwamba yapo baadhi ya mambo ya msingi, ambayo Ukawa wanayajengea hoja, kama kiini cha wao kususa Bunge hilo.

Lakini, kwa namna yoyote ile, madai hayo hayawezi kushughulikiwa, endapo Ukawa wataendelea kuyajengea hoja nje ya Bunge Maalumu la Katiba.

Kwa vile zipo kanuni, ni vema Ukawa wakazichambua kanuni hizo ili kuziwekea mikakati kanuni zinazotoa mwanya kwa madai yao kupatiwa ufumbuzi ili mara tu baada ya Bunge hilo kurejea, wazitumie kanuni hizo kushinikiza kutekelezwa kwa matakwa yao.

Inawezekana Ukawa wakatamani kusikia sauti ya kiongozi mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete akiwaasa kurejea, kama ambavyo wamekuwa wakisisitiza.

Lakini, ni imani yetu kwamba kwa vile viongozi wa dini wana nafasi kubwa zaidi katika kuiasa jamii, ni vema Ukawa wakasikiliza busara za viongozi hao katika kufanya uamuzi, juu ya mgomo wao, badala ya kuendelea kusubiri kauli ya Rais Kikwete wanayoitaka.

Hima hima wajumbe wa Ukawa, rejeeni bungeni ili muweze kuwaandikia Watanzania Katiba mpya, inayosubiriwa kwa hamu kubwa.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi