loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wakulima na hofu ya kushuka ufanisi wa soko la mahindi

Wakulima na hofu ya kushuka ufanisi wa soko la mahindi

Jambo hilo linafuatia taarifa iliyotolewa na viongozi wa Mkoa wa Manyara kwa kutoa siku 30 kuanzia Desemba mosi mwaka jana, kuwa wakulima wanaolima maeneo yanayodaiwa kuwa ni hifadhi ya msitu kuondoka maeneo hayo mara moja. Jambo hilo limezua hofu ambapo wakulima wengi hawakukubaliana nalo kutokana na kulima kwenye maeneo hayo kwa miaka mingi.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima Josephat Mponda anasema ni muhimu kama Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai ambaye pia ni Naibu Spika kupeleka suala hilo serikalini ili watambue jinsi wakulima wanavyonyanyasika.

Anasema wakulima wa Wilaya ya Kongwa waliingia Kiteto mwaka 1991 kwa kanuni na sheria za Tanzania na walifika kwa viongozi wa Serikali wa Vijiji na Wilaya ya Kiteto na wakaomba maeneo ya kilimo na walipewa kihalali. Mponda anasema mpaka sasa zaidi ya miaka wanalima maeneo hayo kwa kushirikiana na halmashauri ya Wilaya ya Kiteto na wanalipa ushuru wa mazao na wanashiriki pamoja kujenga shule.

Anasema ilipofika mwaka 2002 ndipo mgogoro ulianza na halmashauri ya Kiteto iliwataka kuondoka kwenye maeneo hayo ili watenge hifadhi bila kushirikisha wananchi pamoja na serikali za vijiji. Kutokana na kauli hiyo, wakulima walitakiwa waache mashamba yao na kuondoka bila kuambiwa waende wapi kwa ajili ya kuishi na kulima.

Kufuatia hilo wakulima waliamua kwenda kwa viongozi wa kitaifa wa serikali kutafuta msaada ili wasinyang’anywe mashamba yao ndipo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, aliingilia na kuagiza suala hilo lirudi vijijini.

Pia vijiji viitishe mkutano wapange matumizi ya ardhi ambapo vijiji vyenye mgogoro viko saba ambapo vitano vimekataa habari ya hifadhi, viwili havikufanya mkutano kwa kuwa ardhi ni mali za kijiji na vijiji ninashangaa havina mgogoro na wakulima.

Aidha anasema halmashauri ya Kiteto inachangisha fedha kwa wafugaji ili kuwaondoa wakulima jambo ambalo linaonesha ana nia ya kugawa wakulima na wafugaji na iwapo jambo hilo halitaangaliwa kwa makini linaweza kuleta machafuko. Mkulima wa Kiteto, Jackson Mtango anasema kuanzia mwaka 2000 kumekuwa na matatizo sana kati ya wakulima na wafugaji.

Anasema licha ya juhudi za mara kwa mara kumaliza mgogoro huo kufanyika lakini kinachoonekana ni wafugaji kupendelewa zaidi kuliko wakulima, jambo ambalo watu wengi hawakubaliani nalo. Kulingana na mkulima huyo kuna matukio ya wakulima kuuawa na wafugaji wa Kimasai, jambo ambalo limekuwa likizua hofu kubwa ya kuzuka machafuko kwenye eneo hilo ambapo mpaka sasa zaidi ya wakulima nane wameuawa na wafugaji.

“Kilio chetu kifikishwe kwa Rais Jakaya Kikwete juu ya wananchi kunyanyaswa na halmashauri ya Wilaya ya Kiteto,” anasema Mtango. Anasema kuanzia mwaka 2000 kumekuwa na matatizo sana na mgogoro huo unachochewa sana na viongozi wachache. “Sisi ni Watanzania tuliajiriwa na ardhi kwani tunategemea ardhi tulime tupate mavuno ambayo ndiyo yanaendesha maisha yetu, lazima serikali itusikilize katika hili na kupatia ufumbuzi jambo hili,” anasema.

Mkulima mwingine, Machite Mgulamba anasema ni muhimu Serikali ikaingilia kati suala hilo kufuatia mkuu wa mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo ambaye ametangaza kuwapa wakulima siku 30 kuondoka maeneo hayo ambayo wamekuwa wakitumia kwa ajili ya kulia kwa miaka mingi sasa.

Anasema kilimo kinachoendeshwa Kiteto ni kikubwa na juhudi hizo zinatakiwa kuungwa mkono na Serikali kwa kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa mapema kabla ya madhara kutokea. Mgulamba anasema wakulima wa Kiteto ndiyo wanaoongoza kwa kupeleka mazao kwenye soko la kimataifa la Kibaigwa hivyo ni bora kuliangalia hilo ambapo kuna matrekta zaidi ya 2,000 katika eneo hilo ambayo yamekuwa yakitumika kwa ajili ya kilimo.

“Tusipolima matrekta yatafanya kazi gani wakati matrekta mengi ni mikopo na watu wanatakiwa kulima ili waweze kurejesha fedha wanazodaiwa,” anasema. Dominic John anasema alianza kulima Kiteto mwaka 1998 ambapo ana shamba la ekari 150 na amekuwa akipata kuanzia gunia 800 hadi 1000 za mahindi ambayo huuza katika soko la kimataifa la Mahindi la Kibaigwa.

“Serikali imeamua kutufukuza wakati tunaendesha kilimo cha kujitegemea na hatujawahi kuomba kusaidiwa fedha au kitu chochote ili tuendeshe kilimo chetu.” Anasema eneo hilo wanalotakiwa kuondoka lina wakulima zaidi ya 40,000 na wanafahamu wakulima hao watakwenda wapi kwani wakulima wote hao wamekuwa wakilima kwa ufanisi mazao ya mahindi na alizeti.

Mkulima mwingine, Abdi Mussa anasema alianza kulima Wilaya ya Kiteto mwaka 2004 na ardhi anayotumia kwa ajili ya kulima alipewa na mkutano mkuu wa kijiji mwaka 2004 ambapo amekuwa akimiliki ekari 150 ambazo ndizo hutumia kwa ajili ya kilimo. Anasema amekuwa akiuza magunia 800 hadi 1,000 kwa msimu katika soko la Kibaigwa.

“Tuko karibu wakulima 40,000 na wananchi walioshtaki kwenye kesi ya kukataa kuondolewa maeneo hayo walikuwa 50 tu, awali wananchi walishinda kesi kisha halmashauri ikakata rufaa ikashinda kesi na hivyo kkutakiwa wakulima wote kuondoka katika eneo hilo kitu ambacho si sawa,” anasema.

Anasema eneo lililohusishwa na kesi sio eneo ambalo wakulima wanatakiwa kuondolewa. Akizungumza na wananchi, Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai anasema mgogoro wa wakulima na wafugaji katika wilaya ya Kiteto mkoani Manyara kwa kiwango kikubwa unachangiwa na viongozi wa serikali ambao wanaendeleza dhana ya ubaguzi.

Anasema hilo linajidhihirisha kutokana na ukweli kuwa baadhi ya viongozi kuendelea kuchochea mgogoro huo kwani wamekuwa wakichukua rushwa ya ng’ombe kwenye kila boma la mfugaji kwa ajili ya kuwafukuza wakulima katika maeneo ambayo wamekuwa wakilima. Ndugai anasema ni muhimu kwa Rais Jakaya Kikwete kutazama suala hilo.

“Tatizo lililopo ni ubaguzi kwa kisingizio cha hifadhi na uharibifu wa mazingira, baadhi ya viongozi wanaendeleza ukabila na mara nyingi ugomvi huo unatengenezwa na baadhi ya viongozi,” anasema.

Mbunge huyo anasema jambo hili liangaliwe kwa makini ili wakulima waweze kulima katika msimu huu wa kilimo. “Kinachoonekana sasa ni viongozi ambao wamekuwa wakiwakumbatia wafugaji na kuwafukuza wakulima kwa madai kuwa wanaharibu mazingira. Watendaji hawabadiliki na kama hawabadiliki basi kuna haja ya kuchukua hatua itakuwaje itangazwe hifadhi mkulima aondolewe halafu mfugaji abaki kama si ubaguzi.” “Wafugaji wamekuwa wakichangishana fedha kwa ajili ya kuwakomoa wakulima huku wakulima wakiambia wako kwenye eneo la hifadhi, hivi ni sheria gani imesajili kuwa hifadhi eneo,” akahoji Ndugai.

Aidha anawataka wakulima kuendelea na kilimo katika eneo hilo na kamwe wasikubali kunyanyaswa kwa kisingizio kuwa ni eneo la hifadhi wakati halijawekwa kisheria. Ndugai anasema kilimo kinachoendesha eneo la Kiteto ni kilimo kikubwa ambacho kina matrekta zaidi ya 1,000 huku matrekta mengine yakiwa yamepatikana kwa mkopo.

“Hata chakula kinachozalishwa ni kingi mno ambacho kinalisha nchi nzima na nje ya nchi na sehemu kubwa ya mahindi yanayozalishwa yanauzwa katika soko la kimataifa la Kibaigwa. Anasema hata hati ya hifadhi hiyo haipo na mara kadhaa amefanya jitihada za kuitafuta lakini hajafanikiwa mpaka sasa na sasa kinachosubiriwa ni kauli ya serikali kuhusiana na mgogoro huo.

Hata hivyo, Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia anasema miaka ya nyuma tatizo kama hilo liliwahi kutokea na watu 14 walipoteza maisha. Anasema kutokana na kadhia hiyo kuanza tena viongozi wakae chini na kutafuta suluhu ya kudumu kwani hata Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi ana wajibu wa kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Nkamia anasema hata baadhi ya viongozi wa Kiteto ni tatizo hali ambayo imekuwa ikichochea mgogoro huo. Diwani wa Kata ya Kibaigwa, Richard Kapinye anasema wakulima wamekuwa wakinyanyasika na watendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kutokana na kuwafukuza katika maeneo yao.

Anasema hata vitendo vya wafugaji kuwaua wakulima vimekuwa vikifumbiwa macho kwani hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na tahadhari isipochukuliwa mapema suala hilo linaweza kuleta maafa hapo baadaye. Ni dhahiri kinachosubiriwa ni kauli ya serikali kuhusiana na mgogoro huo ili wakulima wajue mipaka yao.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi