loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanaume Mwanza wafundwa kushiriki afya ya uzazi

Suala la afya ya uzazi kwa muda mrefu limekuwa likifanywa na wanawake pekee huku wanaume wakibaki kuwa kama watazamaji ingawa ni haki ya kila mmoja katika ndoa kushiriki na kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii.

Hali hiyo ya wanaume kujiweka kando na masuala ya afya ya uzazi imesababisha madhara makubwa kwani baadhi ya maamuzi yao yameathiri afya ya uzazi, ikiwa ni pamoja na vifo vya wajawazito pamoja na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Taasisi mbalimbali zimeiona changamoto ya ushiriki mdogo wa wanaume katika masuala ya huduma za uzazi wa mpango na hivyo kuamua kutoa elimu kwa wataalamu itakayowawezesha kuifikia jamii hasa wanaume na kuielimisha ili waweze kubadilika na kushiriki kwenye masuala ya afya ya uzazi.

Winlady Boniface ni miongoni mwa washiriki wa programu ya mafunzo ya kubadili tabia ya jamii katika masuala ya afya inayotekelezwa na Shirika la John Hopkins University (JHU) kwa msaada wa watu wa Marekani (USAID).

Anasema amenufaika na mafunzo hayo na tayari ameanza kutekeleza kwa vitendo katika kata ya Usagara na Fela wilayani Misungwi.

Anasema mafunzo hayo ni sehemu ya mawasiliano ya afya kwa ajili ya kubadili tabia ya wanajamii kuendana na mabadiliko ya kiafya na kunufaika na huduma za afya zinazotolewa na wizara ya afya, wadau na mashirika yasiyo ya kiserikali.

“Mafunzo hayo ya miezi sita yameniongezea ujuzi kwenye upande wa mawasiliano ya afya ya jamii na sasa naweza kwenda mstari wa mbele kuielimisha jamii ili iweze kuondokana na uvumi na mtazamo potofu juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango,” anasema.

Anasema amepata elimu ya kutengeneza programu ya matangazo ya afya ya kubadili tabia katika jamii na njia ya kushirikisha jamii hasa wanaume katika masuala ya afya.

“Tayari nimepata mradi utakaonisaidia kufanya kazi kwa vitendo katika kata za Usagara na Fela wilayani Misungwi kwa kutumia elimu niliyoipata.

“Nimefurahi sana kwa sababu nimeona jinsi jamii ilivyofaidika na elimu niliyoipata kwani tayari nimeendesha mdahalo wa kubadili tabia ya jamii hasa ushiriki wa wanaume katika huduma za uzazi wa mpango," anasema.

Katika kata ya Usagara na Fela wilayani Misungwi anasema mafunzo hayo yamemwezesha kutoa elimu ya ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya huduma ya afya katika uzazi wa mpango, eneo lenye changamoto lukuki katika jamii.

Anasema jamii ina mitazamo hasi kuhusu ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya uzazi wa mpango, lakini inaweza kubadilika baada ya kupatiwa elimu na kuwa kichocheo cha kuboresha uzazi wa mpango.

Nalifika katika kata ya Usagara ili kushuhudia namna jamii ilivyoipokea elimu hiyo na kama italeta mabadiliko chanya kwenye jamii kwa maana ya wanaume kuanza kushiriki katika afya ya uzazi, hususani uzazi wa mpango.

Japhet Ngereja wa kata ya Usagara ni miongoni mwa wadau walioshiriki katika mafunzo ya ushiriki wa wanaume katika huduma za uzazi wa mpango. Yeye anasema wanaume wengi wamekuwa waoga kufunga uzazi kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha na kuwepo kwa uvumi mitaani juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

Anasema kumekuwepo na uvumi mbalimbali mitaani juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango na hivyo kuwatia hofu kuzitumia, lakini wakipata elimu ya kutosha kutoka kwa wataalamu wa afya wanaweza kuhamasika kuzitumia.

Anasema mbali na uvumi wa njia hizo kuwa na madhara mengi zaidi ya faida kiafya, ilikuwepo pia dhana kwamba anayeshiriki uzazi wa mpango anaweza kuwa malaya.

“Sasa ndio tumepatiwa elimu na ufahamu wa matumizi ya njia za uzazi wa mpango lakini huko nyuma tumekuwa tukisikia vitu vingi tofauti na tulivyojifunza, sasa tumeelimika na tutaelimisha wengine,” anasema.

Moses Ayo, mchungaji wa kanisa la FGBF katika kata ya Usagara, anasema mada zilizowasilishwa katika mafunzo kuhusu ushiriki wa wanaume katika afya ya uzazi zinamshirikisha Mungu kwani hata Biblia inafundisha kwamba baba ni kama kichwa cha familia hivyo hana budi kuitunza na asipoitunza ni dhambi.

Yeye anaona ni mpango wa Mungu kuwa na utaratibu wa kuzaa sambamba na kuelimisha njia za uzazi wa mpango za asili na za kisasa. Mchungaji Ayo anasema amekuwa akiwatia moyo waumini wake kuonana na wataalamu wa afya kujua ni njia gani za uzazi wa mpango wanazoweza kutumia.

Anasema kanisa la FGBF limekuwa likiendesha semina za wanandoa wakielimishwa masuala mbalimbali yahusuyo ndoa, lakini bado mkazo bado ulikuwa haujawekwa kwa wanaume.

Anasema ni vyema watu wakubali elimu ya afya hususani ya uzazi wa mpango na kuweza kushiriki ipasavyo kuliko kuendelea kusikiliza maneno ya mitaani ambayo hutofautiana na yanayofundishwa na wataalamu.

Daktari wa zahanati ya Idetemya, kata ya Usagara, Joseph Muyande anasema wanaume wachache wamekuwa wakijitokeza katika masuala ya huduma za uzazi wa mpango ambapo kwa mwezi anaweza kujitokeza mmoja ama asiwepo kabisa.

Sababu zinazochangia wanaume kutojitokeza kwa wingi anasema ni pamoja na mila na desturi ambapo wanaume hawaoni sababu za wao kushiriki katika masuala hayo wakati anayebeba mimba na kuzaa ni mwanamke.

Anashauri elimu kutolewa vya kutosha kwani suala hilo bado ni geni kwa jamii hasa za vijijini na waliopata elimu hiyo ni wachache, hivyo anawataka wahusika wa program hiyo kujikita zaidi vijiji.

Jamii imekuwa ikiwaamini zaidi wasio wataalamu kuliko wataalamu wa afya na hii inatokana na uvumi ambao ni mwingi kuliko ukweli halisi wa huduma za uzazi wa mpango.

Mfano, watu wamekuwa wakijadili na kukubaliana kuwa njia za uzazi wa mpango zinaleta kansa kwa wanawake lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kudhibitisha pasipo shaka kuwa alimuona mgonjwa wa kansa iliyotokana na matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

Mratibu Msaidizi wa Afya ya Uzazi katika wilaya ya Misungwi, Grace Masunga anasema, ofisi yake imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) ambapo wameteka kata nne za Lubili, Shilalo, Nunduru na Kasololo kwa ajili ya kutoa elimu kwa viongozi na wanavijiji ili waendelee kuelimisha juu ya mila potofu zinazowafanya wanaume washindwe kushiriki katika suala zima la afya ya uzazi.

Uamuzi huo anasema ulifikiwa baada ya kugundulika kwamba baadhi ya wanawake hushiriki katika suala la uzazi wa mpango kwa kificho wakihofia waume zao kujua.

Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa uzazi wa mpango nchini hupunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 44.

Aidha takwimu zinaonesha pia kwamba matumizi ya njia za uzazi wa mpango siku za nyuma zilikuwa mwaka 1991/92 asilimia 7, mwaka 1996 asilimia 13, 1999 asilimia 17, 2004/5 asilimia 20 na mwaka 2010 ilikuwa asilimia 27 na kwamba ifikapo 2015 mkakati ni kufika asilimia 60.

“WANAOFANYA shughuli za maendeleo katika vyanzo vinavyotiririsha maji ...

foto
Mwandishi: Grace Chilongola

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi