loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanawake: Wadau wa elimu walioathiriwa na mfumo dume

Ghairi ya changamoto za kijinsia wanazokumbana nazo, bado wanawake tunaweza kuwaweka kwenye daraja la juu la viwango vya ushiriki wa jamii yetu, katika kujiletea maendeleo.

Haina maana kwamba sitambui mchango wa wanaume katika kuliletea taifa letu maendeleo, isipokuwa katika makala haya nitajaribu kutoa mchango wangu wa mawazo juu ya ushiriki wa wanawake katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora, huku nikihusisha athari za mfumo dume dhidi ya wanawake.

Lengo la kufanya hivi ni kutaka jamii yetu kuchukua hatua za kujirekebisha. Awali ya yote, ninakubaliana na kauli ya siku hizi isemayo ukimwelimisha mwanamke, umeelimisha Taifa na hata Waarabu wanasema ‘mwanamke ni shule’. Kauli hizi zinabeba ujumbe mzito unaotokana na nafasi ya mwanamke katika jamii, unaokinzana na nafasi ya mwanaume katika ushiriki wao kwenye shughuli za maendeleo kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Tangu mwanzo hata sasa, historia inatufunza kwamba, kutokana na mila na desturi zetu wanawake wamekuwa hawapati fursa ya kupata elimu kama ilivyo kwa wanaume. Hiyo ni sehemu ya makali ya mfumo dume katika eneo hilo.

Ingawa taratibu jamii inabadilika, lakini kasumba hii mbaya ndani ya jamii yetu bado ipo na inapaswa kupigwa vita kwani inavyoonekana wanawake wanajitahidi sana, pengine hata kuliko wanaume walio wengi katika kusimamia maendeleo ya shule ya watoto wa kike na watoto wa kiume bila ubaguzi wa kijinsia.

Tunapotafakari kidogo, tunaona kuwa mwanamke kama mzazi amebebeshwa mzigo mzito wa kuilea na kuiangalia familia bila kujali uwezo wa kiuchumi uliopo kwenye familia husika. Kadhalika wapo wanawake wengi wanaolea watoto peke yao bila wanaume, tena baadhi yao wakiwa wamekimbiwa na wanaume hao baada ya kuwapa mimba.

Na pia zipo familia ambazo akina baba wamezitelekeza. Hata hivyo, uzoefu unaonesha zipo familia zilizo na nafasi nzuri kiuchumi lakini mwanamke ndiye anayeachiwa majukumu yote ya kulea watoto. Iwe mjini au kijijini, mwanamke amezongwa na makali ya mfumo dume.

Tangu kuzaliwa hadi kukua kwa mtoto, mwanamke ndiye sehemu kubwa anayelazimika kumlea mpaka anapofikisha umri wa kwenda shule pasipo usaidizi wowote wa maana kutoka kwa mwenzi wake. Akipata usaidizi kutoka kwa baba hilo ni jambo lingine, lakini wanaume walio wengi hawashiriki kikamilifu katika malezi ya watoto.

Wengine huthubutu kuzikimbia familia zao kama nilivyodokeza hapo juu. Ikitokea hivyo waathirika wakubwa huwa ni wanawake na watoto. Wanawake hufedheheka na watoto hukosa elimu bora. Kunywa pombe kupindukia huenda ikawa chanzo kikuu cha haya yote.

Tumeshuhudia au kusikia mama mjamzito akibeba mtoto mgongoni na jembe begani akielekea shambani kulima ilhali baba wa familia anachapa tembo (pombe) kilabuni. Mama atalima na mwanawe mgongoni huku jua likimchoma na kazi nyingine humsubiri nyumbani. Anaporudi nyumbani, licha ya mtoto mgongoni, pia hubeba shehena ya kuni kichwani, kifurushi cha mboga za majani za mlo wa siku hiyo, lita tano za maji na jembe lake mkononi.

Mfumo wa maisha ya aina hii licha ya kumkandamiza na kumdhalilisha mwanamke, pia huzorotesha ustawi wa familia. Kumbe kwa hali hii, watoto huenda shuleni wakiwa hawajala chochote kwani mama hakuwa na muda wa kuandaa chakula. Baba hurudi usiku wa manane akiwa amevaa miwani (kalewa pombe), anakataa kula ugali kwa tembele huku akimtaka mkewe amtengee wali kwa nyama, ilhali anafahamu hakuacha fedha za kugharamia mlo huo.

Jambo likitokea kuhusu maendeleo ya mtoto shuleni, mama (mwanamke) huwajibika kwenda kuzungumza na walimu. Mkuu wa kaya (mwanaume) hubaki kupunga upepo ama yuko kwenye kibanda cha pombe. Elimu bora ya mtoto huchochewa na ushirikiano wa kimalezi baina ya mzazi/mlezi wa mtoto, walimu, wanafunzi, jamii na wadau wengine wa elimu kwa ujumla.

Watoto wa jinsia zote wanayo haki yao ya msingi ya kupata elimu bora. Baba kama mkuu wa kaya awe mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wa kike na kiume wanakwenda shule. Mfumo dume unakinzana na haki ya watoto wa kike ya kupata elimu, kuanzia anapozaliwa hadi anapofikia umri wa mtu mzima.

Ipo haja ya kujirekebisha. Ndoa za wake wengi nazo ni tatizo. Mara nyingi wanaume wamekuwa wakisitisha huduma kwa familia ya mke wa kwanza baada ya kupata mke wa pili. Athari zake ni kubwa. Licha ya watoto kukosa elimu ya uhakika, ndoa za mitala huweza kusababisha kutokea kwa ndoa za utotoni, mimba za utotoni, maambukizi ya VVU na ajira za watoto.

Tamaa za kimwili za wanaume hupelekea kutafuta mke mwingine bila kujali uwezo alionao wa kutunza familia. Zama za kumfanya mwanamke kuwa chombo cha starehe zimepitwa na wakati. Wanawake wakipata ushirikiano wa kulea familia kutoka kwa wenzi wao, hali ya mfumo dume na unyanyasaji wa kijinsia utatoweka hivyo mahitaji ya kuwapeleka watoto wao shule yatapatikana.

Mwanamke atapunguziwa mzigo wa kulea familia peke yake uliomuelemea kwa miongo mingi sasa. Inavyoonekana wanawake wamekosa wa kuwasemea kama wapo ni wachache, wao huishia kulalamika. Lakini katika jamii yetu na hata katika medani za kimataifa wapo wanawake wa kupigiwa mfano, waliovivuka vikwazo vyote vinavyotokana na mfumo dume.

Sasa yapasa wapaze sauti zao kuwasemea wenzao. Ipo wizara inayoshughulikia wanawake na watoto. Ifanye kazi yake kwa kuhakikisha hakuna ukandamizaji wa wanawake na watoto. Watoto wapate haki yao ya kuelimishwa. Wanaoendelea kushikilia kuwa mfumo dume ni mfumo sahihi wa maisha wawekewe adhabu kali zaidi ili iwe fundisho.

Lengo letu liwe kuutokomeza huu mfumo kandamizi unaowanyima watoto fursa ya kupata elimu pamoja na kuwanyanyasa na kuwakandamiza wanawake. Jamii ielimishwe. Tutafika! Mwandishi wa makala haya ni mkazi wa Dodoma na msomaji wa HabariLeo.

benedictbnkumbi@ yahoo.com

Simu;0756308038 au 0717770088.

“MTU niliyefanya naye mahojiano alikuwa anafanya kazi kwenye ...

foto
Mwandishi: Benedict Nkumbi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi