loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanawake wanavyouzwa dola 10 sokoni

Inadaiwa kuwa, watu hao ni familia za Kituruki zilizokuwa zinaishi Kobane na sasa zimekwama katika mji huo ambao, hadi naandika makala haya, ulikuwa kwenye mapambano makali kati ya ISIS na wapiganaji Wakurdi waliokuwa wakiwazuia wasiingie na kuuteka mji huo.

Inadaiwa kwamba, wanawake wakiwemo wazee, wasichana na watoto wameamua kuchukua bunduki zikiwemo za AK-47 kwa sababu si rahisi kuondoka Kobane, hivyo imewalazimu kupambana kujilinda kwa kuwa ISIS walikuwa kwenye maeneo ya mji huo.

Hadi Oktoba 15 mwaka huu kulikuwa na taarifa kwamba, mashambulizi ya anga ya majeshi ya ushirika yalikuwa yameshindwa kuizuia ISIS kusonga mbele kuingia Kobane na huenda hadi makala haya yanatoka wanaweza kuwa wamefika katikati ya mji huo.

Kwa mujibu wa mitandao ya kimagharibi, ikiwemo ya CNN na BBC, maofisa wa Kikurdi waliwataka maelfu ya wakazi mjini humo waondoke kwa sababu wasingeweza tena kuwalinda, na kwamba, ilikuwa dhahiri ISIS wangeuteka mji huo unaodaiwa kuwa muhimu kwa kundi hilo la ISIS, Uturuki na majeshi ya ushirika.

Kwa mujibu wa habari ambazo hazikuthibitishwa, hadi Oktoba saba, asilimia 80 ya wakazi wa Kobane walikuwa wamekimbilia Uturuki, na kuna watu wengi wakiwemo wazee bado wapo Kobane na sasa hawawezi kuondoka huko.

Sina uhakika kama wanawake walioonekana kwenye picha hizo ni sehemu ya mamia ya wanawake waliojitolea kupambana na ISIS.

Inakadiriwa kwamba theluthi moja ya wapiganaji Wakurdi wanaopambana na ISIS ni wanawake wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 40.

Kuna madai kwamba, kuwepo kwa wanawake katika mapambano hayo kunaongeza hofu kwa ISIS kutokana na imani iliyopo huko kuwa, mwanamke akikuua unakwenda moja kwa moja jehanamu. Kwenye mpaka wa Syria na Iraki kuna bataliani ya wanawake inayopambana na ISIS iitwayo YPG.

Wanawake hao wana jukumu la kufanya doria katika vituo vya mipakani, hivyo wanaweza kufuatilia nyendo zote za ISIS Iraq na Syria. Mmoja wa wanawake hao ni binti Rosarine (19) ambaye amekiri kwamba, kabla ya mapambano dhidi ya ISIS hakuwahi kufyatua risasi.

“Nilivyofyatua mara ya kwanza niliogopa lakini upendo kwa nchi yangu ulikuwa mkubwa kuliko hofu yangu,” anasema na kubainisha kwamba sasa anafyatua risasi wakati wowote anapoona kitu kinatembea walipo ISIS.

“ISIS walifikiri wanawake hawawezi kupigana nao lakini tupo hapa, hatuogopi kwa sababu tunajua tunachokipigania,” anasema msichana huyo aliyeacha shule akaenda kujiunga kikosi hicho maalumu chenye jukumu la kuwalinda Wakurdi.

Kwa mujibu wa msichana huyo, wanawake wote kwenye batalioni hiyo wanajitolea, na wanakwenda kupambana wakiwa na kauli mbiu isemayo ‘Hava’ ikimaanisha urafiki.

Anasema, wanawake hao waitwao ‘Dada wenye silaha’, wanaungwa mkono na kupewa moyo na familia zao kwa kuwa wanapigana kulinda ardhi ya Wakurdi na watu wake.

Kamanda wa wapiganaji wanawake Wakurdi, Dalil Derki anasema, jeshi hilo linashambulia wapiganaji wa ISIS ambao baadhi ya itikadi zao haziendani na mafundisho sahihi ya Uislamu.

“Kwenye filosofia yao mwanamke hana nafasi yoyote kwenye jamii, filosofia na utamaduni wao wanaamini kuwa, mwanamke akiwaua hawaendi peponi badala yake watakwenda jehanamu,” anasema Derki na kusisitiza:

“Kama wanataka kwenda jenahamu waendelee kupigana na sisi.” Derki anajivunia mafanikio waliyopata kwenye uwanja wa mapambano na kwamba, yatakuwa mfano kwa wanawake kote duniani.

Mamia ya wanawake kutoka mataifa mbalimbali duniani wapo vitani wakiunga mkono ISIS. Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti na Tathmini kuhusu Ugaidi (TRAC), takribani asilimia 15 ya wapiganaji wa nje wa ISIS ni wanawake, wanaokadiriwa kuwa 200 kutoka zaidi ya nchi 14 zikiwemo za Afrika.

Inadaiwa kuwa, hadi mwanzoni mwa mwezi huu, ISIS walikuwa wamewateka zaidi ya wasichana na wanawake 2,500 Wakurdi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wao kutaka kupata wafuasi, wakawauza wawe watumwa, na wanaume waliotekwa wameuawa.

Kwa mujibu wa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa (UN), kuna masoko ya watumwa ya ISIS nchini Iraki, wanawake na watoto Wakristu na Wayazidi wanauzwa. UN inadai kuwa, ISIS wakiteka wanawake wanawafanya watumwa, wanawadhalilisha kijinsia, na kila mmoja anauzwa kwa dola 10 za Marekani.

Umoja wa Mataifa unasema, kwa mujibu wa jarida la International Business Times, masoko ya watumwa yaliyopo kwenye kitongoji cha al-Quds mjini Mosul nchini Iraki na kwenye Raqqa nchini Syria yanatumiwa kupata wafuasi wapya wa ISIS. Inadaiwa kwamba, wanawake waliotekwa Agosti mwaka huu walificha simu zao za mkononi na walifanikiwa kuwasiliana na UN kutoa taarifa kwamba walikuwa wanadhalilishwa kijinsia.

Mmoja wa wanawake hao ni mtoto Myazidi aliyetekwa kijijini kwao Agosti tatu. Kwa mujibu wa mtoto huyo mwenye miaka 13, ISIS waliteka mamia ya wanawake ambao hawakuweza kukimbilia kwenye milima ya Jabal Sinjar.

Mtoto huyo anadai kuwa, wapiganaji kadhaa wa ISIS walimbaka mara kadhaa, na kisha akauzwa sokoni.

Inadaiwa kuwa, wapiganaji 10 wa ISIS walimbaka mmoja wa wanawake hao.

“Tuliuzwa kwa bei ya dola 10 hadi 12 (za Marekani), nani angekubali hiyo tabia? Mungu anaweza kulikubali hilo?” anasema mmoja wanawake hao mwenye miaka 17.

“Ni aibu kumbaka mwanamke lakini anapobakwa na wanaume 10 hii ni nini? Ni wanyama, wale si binadamu na kwa sababu yao, kila wakati naogopa,” anasema mwanamke huyo aliyefanikiwa kutoroka utumwani baada ya mwananchi kumsaidia na akakimbilia Mosul.

Kwa mujibu wa mwanamke huyo, alikuwa mateka na wanawake wengine 40 wa jamii ya Yazidi ya nchini Iraki. Mwanamke huyo alihojiwa kwa simu ya mkononi baada ya wazazi wake waliopo kwenye kambi ya wakimbizi nchini humo kumpa namba mwandishi wa habari.

“Naomba msiandike jina langu kwa sababu naona aibu kwa wanayonifanyia. Kuna sehemu ya mwili wangu inataka kufa, lakini sehemu yangu nyingine ambayo bado inatumaini kwamba nitaokolewa na kwamba, nitaweza kuwakumbatia tena wazazi wangu,” anasema msichana huyo.

“Tumewaomba waliotuteka watupige risasi tufe, watuue, lakini wanatuhitaji sana. Wanaendelea kutuambia kwamba hatuna imani kwa sababu sisi si Waislamu na kwamba, sisi ni bidhaa kama kitu cha starehe vitani, wanasema sisi ni kama mbuzi walionunuliwa sokoni,” anasema. Imeandikwa kutoka vyanzo kwenye mtandao wa intaneti.

TANZANIA na dunia nzima kwa sasa ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi