loader
Dstv Habarileo  Mobile
Waongozaji wanavyoharibu filamu

Waongozaji wanavyoharibu filamu

Lakini filamu nyingi za Kitanzania, au za Kibongo kama tulivyozoea kuziita zimekuwa zikiharibiwa na watu wawili. Wa kwanza ambaye amekuwa akiharibu filamu ni mwandishi wa mwongozo ‘Skript’, ambaye anaweza kusimuliwa na kujikuta akishindwa kupanga vizuri matukio kutokana na simulizi aliyopewa na kuepelekea filamu kuharibika.

Na mwingine anayeweza kuiharibu filamu ni mwongozaji ambaye kihalisi ndiye mtu pekee anayebeba lawama zote za filamu, iwe nzuri au mbaya. Yeye anaweza kupotoshwa na mwandishi wa skripti kwa kuandikiwa kitu ambayo inaweza kumchanganya zaidi, lakini ili kwenda sambamba na stori lazima arudi kwa mwenye simulizi, na amhadithie upya na hapo ndipo atakapopata maana ya stori na kuiongoza vizuri.

Hii imejitokeza katika filamu ya Last Step, labda ningeanza kuuliza maswali haya. Hivi kuna mtu anaweza kumuua mkewe, na kutembea mtaani, bila ya wasi wasi na hata kudiriki kuendelea kufanya mauaji mengine bila ya wasi wasi, huku jina lake na picha yake ikisambaa kwenye magazeti?

Najua wengi mtapata jibu kwamba ni kitu ambacho hakiwezekani, lakini kwenye filamu hii imewezekana. Labda ningeanza kwa upande wa stori ya filamu, ambayo naweza kusema msimulizi wa filamu alikuwa na simulizi nzuri. Tena nzuri ya kuvutia, lakini tatizo sijui lilikuja kwa mwandishi wa mwongozo ‘Script Writer’, au tatizo lilikuwa kwa mwongozaji mwenyewe.

Nasema hivyo kwa maana hao wawili ndio wenye jukumu zima la kufanya filamu inoge, yaani namaanisha mwongozaji filamu asipouelewa vizuri mwongozo basi hata filamu atakosea kuiongoza. Hapo ndipo kinakuja kilichotokeza kwenye filamu hii, baada ya mwongozaji kushindwa kuimudu filamu na kujikuta matukio yakikorogana na hata mengine kukuweka njia panda.

Mchanganyiko wa matukio, umempelekea hata Mhariri wa filamu, kutokuwa na muunganiko mzuri kati ya tukio moja na lingine ‘Bridge’. Filamu ya Last Step, simulizi yake ilitungwa na Jerry Cham, muandishi wa mwongozo ni Kismaty Ally, mwongozaji ni Jelly Chambilo, na mtarishaji au mzalishaji ‘Producer’ kazi iliyofanywa ni Consorose Shihumba.

Mchukua picha ni Sweabert Michael, na mwisho wa filamu ilihaririwa Florian Lawrence. Hao waliohusika katika utengenezaji wa filamu hii, lakini waigizaji hawakuwa wengi kwa kuwa kati yao walionekana mara moja na kupotea. Labda ningekupa kwa ufupi jinsi ilivyokuwa na kwanini nakwambia hivyo, Stori yenyewe ilikuwa ikihusu maisha ya kijana Pearson Samweli aliyeigiza kama Kessy, na Aunt Ezekiel aliyeigiza kama Zed.

Filamu ilianza wakati Zed akionekana akiuza matunda kwa kutembeza na kubeba kwenye beseni, ndipo anapokutana na Kessy dukani, ambaye naye alikuwa hapo kwaajili ya huduma nyingine. Kessy anamuita na kununua matunda na kumchombeza kwa maneno ya hapa na pale na hatimaye, wanakubaliana kuishi pamoja.

Hapo mengi kuna matukio yanashindwa kueleweka sababu sehemu kubwa inatumika sauti ya muziki wa nyuma ‘Back sound’, ambayo inafanya baadhi ya maongezi tusiyajue. Lakini ghafla tunaanza kuona wawili hao wakiishi pamoja, lakini kama vile kuna kitu kinakumbukwa zaidi kutokana na mwingiliano wa picha za matukio.

Nasema hivyo kwa maana kuna kipindi nilijua labda scene nyingine inakuja, ila ina sita sita, lakini baadaye nikaja kugundua kwamba, Kessy anavuta kumbukumbu ya tukio ambalo hatukuwahi kuliona mwanzoni. Mapenzi yao yanatawaliwa na ucheshi, na utani ili kuonesha jinsi wapenzi hawa walikuwa wamezama kwenye dimbwi la mahaba, ingawa Zed anaonesha wazi kutofurahia utani huo.

Kama unapenda kula basi kwenye filamu hii ndiyo mahala pake, kwani wametumia muda mrefu watu kuandaa chakula na kula. Siku moja Kessy anaporudi nyumbani kwake anamkuta, mkewe akiwa amelala kwenye kochi, simu yake ameiweka mezani. Bila ya kumshitua anachukua simu na kuchunguza nini kilichomo, lakini ghafla anabadilika uso kwa hasira ingawa hatujui nini alikiona kwenye simu hiyo.

Hapo ndipo inapokuja tena ile kumbukumbu ya tukio, ambayo baadhi yake anaonekana Kessy akiwa ameshika kisu chenye damu. Kessy anarudisha simu ya mkewe mezani, kisha anamwamsha na kama kawaida ya mapenzi yao, mwanamume anaanza kumtania mkewe lakini utani ambao mara nyingi mkewe huwa hafurahii hata kidogo.

Baada ya tukio hilo tunarushwa mpaka kwenye tukio lingine ambalo tunamuona Kessy, akiwa amekaa kwenye kochi, na kisu mkononi. Anaonekana mtu mwenye mawazo sana, huku akikishika kile kisu na kukizungusha zungusha. Baada ya kuwaza kwa muda mrefu, anainuka na kukichomeka kisu kiunoni, kisha tunarushwa kwenye tukio lingine.

Tukio ambalo tunamuona Kessy akiongea na mtu ambaye baadaye tunakuja kugundua ni dereva teksi, baada ya kuchukuana. Kessy anamchukua dereva huyo hadi nyumbani kwake, na wanaposhuka Kessy, anamwambia. “Kama kazi ikikamilika basi nitakuongezea laki moja nyingine na itakuwa laki mbili”.

Jambo ambalo dereva anakubali na kumtoa wasi wasi kwa hilo. Wanapoingia ndani Kessy anaenda kufunua maiti ya mkewe Zed, kisha anamwambia amsaidie kusogeza gari ili wautoe mwili na kwenda kuutupa. Lakini Kessy anakuja kushituka baada ya kuona yule dereva huenda akamsaliti, jambo ambalo aliamua kukimbia na kutoka ndani ya nyumba.

Muda mchache baadaye tunamuona dereva akiwa na polisi na kuja hadi katika nyumba hiyo, ambayo ilikuwa na maiti ya Zed, lakini Kessy akiwa tayari ameshakimbia. Baada ya kutoroka kwenye mauaji, anaonekana katika soko la Mwananyamala akinunua ndizi,na baada ya hapo aliondoka hadi kwenye hoteli aliyopanga.

Hapo ndipo anapoanza kukumbuka jinsi alivyokuwa akichomoa kisu kutoka tumboni kwa mkewe. Wacha niishie hapo, kwani linakuja timbwili la mtafute mtafute, kati ya polisi na Kessy juu ya Mauaji ambapo walifanikiwa kupata hadi picha yake. Lakini pia kuna mtafute mtafute ya Kessy na dereva taksi ambaye alishuhudia maiti kwa mara ya kwanza na kutoa taarifa polisi.

Huwezi amini lakini ndivyo hivyo, Kessy anapoamua kufanya mauaji zaidi ili kuficha siri yake, lakini kikubwa zaidi ni kuweza kutembea barabarani bila ya wasi wasi wakati tayari sura yake ipo kwenye magazeti.

Ushauri wangu kwa mwongozaji wa filamu, kama unahisi stori hujaielewa kupitia mwongozo ‘Script’, mfuate mtunzi wa hiyo simulizi atakuelezea lengo lake. Kukosea kwako, unaweza kusababisha mwigizaji akakosea, mpigapicha akakosea, na kila kitu kikaenda tofauti na filamu ikawa mbaya. Sababu haiwezekani filamu nzima watu wanakula masaa yote, utafikiri matangazo ya afya.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Mohamed Mussa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi