loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

WASAGARA: Wanavyozingatia mila katika malezi ya watoto

Kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa na John Mwakipesile kuhusu utamaduni wa Wasagara, mila na desturi hizo zinatumika pia katika malezi ya mtoto angali tumboni mwa mama yake hadi anapotimiza umri wa miaka 15. Kwa mujibu wa mila na desturi za Wasagara, mama mjamzito anakuwa katika uangalizi maalum ili mtoto aweze kukua vizuri.

Mwakipesile anasema Wasagara walikuwa na mila nzuri kuhusu uzazi salama kwa sababu mwanamke mwenye ujauzito aliruhusiwa kula chochote kile na kama alisema anatamani kitu fulani basi kilitafutwa. Hata hivyo, mama mjamzito hakuruhusiwa kula vyakula vilivyohisiwa kuwa ni hatari kwa afya ya mama na mtoto.

Hali hiyo iliwafanya wajawazito kuwa na afya njema na kujifungua watoto wenye afya pia. Ni mwiko kwa mume kumpiga mke wake wakati wa ujauzito. Pia mjamzito hakuruhusiwa kutembea umbali mrefu wala kushiriki katika kazi ngumu. Pia ni mwiko wa mwanamke mjamzito kuwa na uhusiano wa mapenzi na mume mwingine.

Hali kadhalika mwanamume ambaye ana mke mjamzito hakuruhusiwa kuwa na uhusiano na mwanamke au wanawake wengine. Mwiko huo unasaidia kuzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa ambayo ni hatari kwa afya ya mama mjamzito na mtoto anayetarajiwa kuzaliwa.

Ili kudhibiti wanawake wajawazito kupunguza kutembea mwendo mrefu Wasagara ‘walizua’ uvumi kuwa katika jamii yao kuna watu wanaochanja wajawazito kwa lengo la kudhuru watoto. Uvumi huo uliwafanya wanawake wajawazito kutembea kwa tahadhari pale walipolazimika kwenda safari ya mbali.

Hata hivyo, wengi wao walikaa nyumbani na kufanyakazi ndogo ndogo kitendo kilichosaidia kuboresha afya ya mama na mtoto. Wasagara wanasifiwa kwa kuwa na tabia ya upole na wema uliotukuka hivyo walihakikisha kuwa watoto wao wanarithi maadili na tabia njema ili kudumisha mila na utamaduni wao.

Mara mtoto anapozaliwa katika jamii ya Wasagara hupimwa afya kwa kunyweshwa maji kisha uji. Endapo mtoto atashindwa kumeza maji waliamini kuwa mtoto huo atakufa au amezaliwa kabla ya kukomaa hivyo anahitaji uangalizi maalum. Kitendo cha kumpa mtoto maji na uji mara baada ya kuzaliwa kinakwenda kinyume na ushauri wa wataalamu wa afya ambao wanahimiza kuwa mtoto anapaswa kupewa maziwa ya mama peke yake kwa muda wa miezi sita.

Kwa mujibu wa utafiti wa kitaalamu, mtoto mchanga chini ya mienzi sita hapaswi kupewa maji wala uji kwa kuwa maziwa ya mama yenye virutubisho vingi vinavyofaa kwa mtoto yanatosheleza. Mtoto anapofikia umri wa kutembea huimbiwa nyimbo mbalimbali zenye ujumbe mzito ili kumwezesha kujenga hulka ya kupenda kazi na kujitegemea badala ya kusubiri wazazi wake.

Mfano mtoto wa Kisagara anapofundishwa kutembea huimbiwa wimbi, “Do yaya do, Maikoka do.” Maana ya maneno hayo ni “pengine mimi (mama yako) nitaondoka, afadhali ujisaidie.” Wimbo huo ulihimiza watoto kukaza miguu na kutembea ili waweze kufikia vitu mbalimbali badala ya kutegemea wazazi kuwaletea.

Wazazi na hasa mama katika kabila la Wasagara ana jukumu kubwa la kuhakikisha mtoto anajifunza lugha ya Kisagara na kutamka maneno yote kwa ufasaha. Pia mama ana kazi ya kuhakikisha kuwa mtoto anakuwa mtiifu kwa kuitikia mwito, kuheshimu wakubwa na kutofanya mambo yasiostahili katika jamii.

Akinamama walifundishwa jinsi ya kuchukua tahadhari endapo mtoto atakutwa na hali ya hatari. Miaka ya nyuma Morogoro kulikuwa na nyoka wengi na yapo masimulizi kwamba wakati mwingine nyoka hao waliwazunguka watoto na kucheza nao. Mwakipesile anasema wanawake wa Kisagara walifundishwa kuwa na ujasiri na uvumilivu pale walipokuta mtoto amezungukwa na nyoka mwenye sumu anayejulikana kama kifutu.

Wasagara waliamini kuwa njia pekee ya kuokoa mtoto aliyezungukwa na nyoka huyo ni kutulia na kuvuta subira hadi nyoka huyo atakapoondoka mwenyewe bila kubudhudhiwa. Endapo mama atapata hofu na kupiga kelele, nyoka huyo hushtuka na kumng’ata mtoto na hivyo ilikuwa ni mwiko kwa mwanamke wa Kisagara kupiga kelele wakati mtoto wake akiwa katika hali ya hatari.

Miaka ya nyuma watoto wa Kisagara walipelekwa jandoni baada ya kutimiza umri wa miaka 10 ili kujifunza stadi za maisha. Maandalizi ya kwenda jando yalifanywa kwa ushirikiano na wanakijiji wote wenye watoto wa rika linalopaswa kwenda jandoni. Watoto hao hukaa jandoni kwa mwezi mmoja au zaidi ambapo pamoja na kufanyiwa tohara hufundishwa jinsi ya kukabiliana na changamoto katika maisha.

Pia hufundishwa jinsi ya kudumisha mila na desturi za Wasagara hasa maadili mema kwa watoto na vijana. Mafunzo yaliyotolewa wakiwa jandoni ni pamoja na watoto kufundishwa kuwa kutukana watu ni makosa, kutukana wakubwa ni mwiko, marufuku kupita mahali ambapo akinamama wamekaa kwa ajili ya mazungumzo au sehemu yoyote ambayo wakubwa wamekaa.

Mtoto wa kiume anapoamkia wakubwa lazima kwanza apige magoti, akishapiga magoti yake, aondoe kofia yake, halafu ndipo aseme “shikamoo”. Anapotaka kuingia ndani ya nyumba ya mama yake lazima abishe hodi na kusubiri hadi aambiwe ‘karibu’ ndipo aingie ndani. Kama hataambiwa karibu anapaswa kuendea kusimama ukumbini hadi atakaporuhusiwa kuingia ndani.

Endapo mtoto aliyehitimu mafunzo ya jando atavunja sheria au kanuni, baba anaweza kumchukulia hatua kali au kumrudisha kwa mwalimu wake wa jando.

Mtoto anayerudishwa kwa mwalimu huapishwa kabla ya kupigwa tena msasa kuhusiana na maadili mema. Katika kiapo hicho, mtoto hutakiwa kusema, “Lusimbi nitamwona tena,” huku akitia alama vumbini kwa kutumia kidole cha shahada cha mkono wake wa kulia kisha hufanya alama kuzunguka shingo yake na kuapa.

Neno “Lusimbi” maana yake ni dawa ya vidonda iliyotumika kuponyesha vidonda baada ya kutahiriwa. Dawa yenyewe ilikuwa vumbi la udongo ambalo ndiyo ilikuwa dawa ambalo lilipakwa kwenye vidonda vya mtoto aliyetahiriwa. Baada ya kiapo hicho mtoto hurudishwa darasani na kujifunza na wanafunzi wapya na akihitimu hutangazwa kuwa alirudia kwenda jando kwa ajili ya mafunzo.

Kitendo hicho huonekana kama aibu kwa kuwa mwanamume hatahiriwi mara mbili hivyo vijana hujitahidi kuzingatia mafunzo ili kuepuka aibu ya kurudi jandoni akiwa ameshatahiriwa. Watoto wanapohitimu mafunzo akinamama huandaa vyakula kwa kutumia mtama kwa ajili ya sherehe ya kupokea watoto wao.

Watoto hao hutoka jandoni siku ya Jumapili na kukaa uwanjani sehemu ambayo hukutana na mama zao tu na hukaa hapo kwa wiki nzima kabla ya kutawanyika. Kila mwanamke mwenye mtoto aliyekwenda jandoni hufika uwanjani na kuita jina la mtoto wake kwa lengo la kumlaki.

Inaelezwa kuwa endapo mtoto atafariki dunia akiwa jandoni, baba yake hujulishwa na maziko kufanyika kimya kimya bila kumjulisha mama mzazi wa mtoto huyo. Siku ya sherehe mama asipomuona mtoto wake hapaswi kuuliza yuko wapi bali aliendelea kuhudumia watoto wengine pasipo kuonesha huzuni.

Ilikuwa ni mwiko kwa mama kulia au kuhuzunika kwa kitendo cha mtoto wake kufa akiwa mafunzoni. Sherehe kubwa hufanyika wiki moja baada ya watoto kutoka jandoni. Siku ya sherehe kubwa mama aliyefiwa na mtoto hulazimika kuandaa chakula na kujumuika na wanawake wengine katika sherehe bila kugusia kifo cha mwanawe.

Mila hiyo kandamizi dhidi ya wanawake ilidumishwa kwa kuzingatia imani kuwa watoto ni wa watu wote hivyo mama hana haja ya kulia wakati kijiji kimejaa watoto wengine wenye rika sawa na mtoto wake aliyekufa akiwa jandoni. Wasagara waliamini kuwa watoto ni mali ya kijiji hivyo mzazi yeyote aliweza kumtuma mtoto wa mwingine na kama mtoto huyo atakataa kwenda basi atapewa adhabu kali.

Watoto walifundishwa kuheshimu na kuwatii watu wote wakubwa. Wakati wa kula wanaume walikusanyika katika kundi na kula kwa pamoja wakiwa wamekaa upande wa kulia na wanawake upande wa kushoto na watoto walikaa katikati. Wakati wa kula ilikuwa marufuku kuvuta sahani, kila mtu alijitahidi kula kwa ustaarabu ili wasipunjane.

Wakati wa kula walizingatia kanuni kwani walikuwa na desturi ya kula ugali kuanzia chini kwenye kitako cha sahani. Ilikuwa ni mwiko kwa Msagara kula ugali kutoka juu na hata watoto walifundishwa kuzingatia kanuni za kula kwa ustaarabu. Hata hivyo, mabadiliko ya mfumo wa maisha yamesababisha Wasagara kuacha kula kwa pamoja na hivi sasa kila familia kujitegemea.

Ilikuwa mwiko kwa Mwanamume kufunua chakula. Hata kama ana njaa atasubiri hadi mama au mtoto afunue chakula hivyo ilikuwa ni lazima mke au mtoto kukaa karibu ili kumfunulia baba chakula. Pia utaratibu huo umetoweka ingawa kama wanafamilia wote wanapata fursa ya kula kwa pamoja basi mama au mtoto anamfunulia baba chakula ili kuenzi mila na desturi za Wasagara.

Wasagara wa kale walikuwa na mfumo wa maisha ambao uliwalazimu watoto kurithi mali kutoka kwa wajomba zao. Mjomba alikuwa na mamlaka makubwa na aliogopwa na kuheshimiwa sana na watoto wa dada zao kwa kuwa mjomba alikuwa na nguvu kuliko baba mzazi.

Mjomba aliweza hata kumchukua mtoto wa dada yake na kumuweka rehani na hakuna ambaye angalimwuliza kisa cha kufanya hivyo. Baba wa mtoto hakuwa na sauti ya kutoa maamuzi mbele ya mjomba. Kazi ya baba ilikuwa ni kuzaa na kusaidia kulea. Hata hivyo, Wasagara wa sasa wameipa kisogo mila hiyo na hivi sasa kila mzazi ana uwezo wa kutoa maamuzi dhidi ya mwanawe isipokuwa mjomba bado anaheshimiwa.

MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Godwin ...

foto
Mwandishi: Kaanaeli Kaale

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi