loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wasanii na Tuzo za Kili 2014

Tuzo hizo zinazofanyika kila mwaka, kwa mwaka huu zitafanyika mwezi ujao huku tayari mchakato wa upigaji wa kura ukiwa umeshafunguliwa. Upigaji wa kura ulianza mapema mwezi huu na wasanii mbalimbali wakiwa wameshaanza kujipigia chapuo kuomba kupigiwa kura.

Lakini pia wapo wasanii ambao wamekuwa na malalamiko kadhaa kuhusu tuzo hizo huku kubwa zaidi ikiwa ni kutolewa kwenye ushiriki wao kwenye tuzo hizo. Wasanii wengine wametolewa kushiriki kwenye tuzo hizo kutokana na nyimbo zao kuwa hazina maadili, hasa suala zima la video za wasanii wenyewe.

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) likiwa kama ndio waratibu wa tuzo hizo chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), katika kufafanua kero mbalimbali zilizotolewa na wasanii walikutana nao katika semina elekezi. Godfrey Mngereza ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, anawasihi wasanii wa muziki nchini kuwa na utaratibu wa kutengeneza nyimbo zitakazoishi miaka zaidi ya 50 ijayo bila ya kuathiri haiba zao.

Mngereza anasema wasanii wa muziki wengi wa sasa wanashindwa kubuni aina ya nyimbo na hata video ambazo zinatunza na kutetea maadili ya Kitanzania. Anasema wasanii wanatakiwa kutambua kuwa majukumu yao sio kuburudisha peke yake, bali kusimama kama kioo katika jamii na kuendeleza maadili ya Kitanzania.

Akiongeza hatua za Basata katika kuwaendeleza wasanii na kuhakikisha wanabakia katika mstari, anasema kuzuia wasanii waliotengeneza video za nyimbo zao zisizokuwa na maadili kushiriki katika Tuzo za Kili ni moja kati ya njia mwafaka za kuwarejesha kwenye mstari wasanii hao.

Anaongeza kuwa kwa upande wa nyimbo kama vile Tema Mate Tuwachape wa msanii Madee au ule wa Snura Mushi wa Nimevurugwa zimezuiliwa kutokana na kutozingatia maadili hayo. Lakini hata hivyo hoja hiyo inakumbana na upinzani kutoka kwa baadhi ya wasanii ambao wanasisitiza kuwa sio haki kuwatoa kwenye ushiriki wa kugombea tuzo kwa kuwa hata nyimbo za Ulaya zinaoneshwa na wasanii wamevaa nusu uchi.

Ni semina ambayo inaonekana kuwa imegusa wasanii pamoja na wadau wa Basata, kwa kuwa wasanii waliwabana watu wa Baraza hilo kuwa uamuzi wao huo hauna mantiki kwa kuwa vituo hivyo hivyo vya luninga bado vinaonesha video za wasanii wengine wa nje wakiwa wakifanya mambo machafu zaidi.

Msanii Khamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ ni mmoja wa wasanii ambao waliwakumbusha Basata kuwa uwepo wa mitandao ya kijamii, unaweza pia kuendeleza kuonesha video hizo na hivyo inakuwa haijasaidia lolote.

Lakini hata hivyo, Mngereza anafafanua zaidi kuwa maadili ya Ulaya sio kigezo cha kuyaleta nchini kupitia video hizo na msimamo wa Baraza kama msimamizi wa tuzo hizo ni kuhakikisha kuwa wasanii wanarejea kwenye mstari kwa namna yoyote ile.

“Lakini najua kuwa hoja yangu kubwa hapa nataka kusema kuwa kuna umuhimu wa wasanii wenyewe kuwekeza kwenye elimu ili angalau kuwa na mwanga katika kusimamia kazi zenu za sanaa,” anasema. Semina hiyo ya takribani saa tano iliyoshirikisha takribani wasanii 50 kutoka katika bendi mbalimbali za muziki, ngoma za asili, taarab, muziki wa kizazi kipya pamoja na watayarishaji wa muziki.

Mbali na wasanii wengine kulalamikia nyimbo zao kutolewa, lakini pia wapo ambao wamelalamikia nyimbo zao kutoingizwa kabisa kwenye tuzo hizo. George Kavishe, ambaye ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, anasema kuwa wasanii wanatakiwa kujua njia mbadala za kuingiza nyimbo zao sokoni.

Anasema ili kuchaguliwa kwenye tuzo hizo ni vema wasanii wakatambua kuwa ni nyimbo zilizotoka kuanzia mwezi wa kwanza hadi kabla ya mwezi wa 11 ndio zinakuwa kwenye nafasi ya kushirikishwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

“Najua kwa sasa mitaani kumekuwa na baadhi ya wasanii wanasema kuwa nyimbo zao zilikubalika mitaani, lakini hazijachukuliwa kwenye kushiriki katika tuzo za mwaka huu, ni vema wakajua ni muda gani wa kuachia nyimbo zao na ziweze kuchukuliwa kwenye tuzo hizi,” anasema Kavishe.

Kavishe anaongeza kuwa lengo la tuzo hizo sio kutoa fedha kwa washindi isipokuwa ni kuonesha kwa kiasi gani wanapongeza na kutambua kazi nzuri iliyofanywa na wasanii watakaoshinda. Anafafanua kuwa wapo wasanii ambao wamekuwa wakidhania kuwa fedha wanazopewa kwenye bahasha ni kutambua ushindi wao, lakini ukweli ni kwamba hizo ni fedha za matumizi madogomadogo tu.

“Tunatambua hali halisi ya maisha yetu, Watanzania tunatakiwa katika hafla kama hiyo pengine kupitia dukani kupendeza na sasa kwa kuwakatia fedha kidogo ni kurudisha kwenye zile zilizotumika katika maandalizi yenu binafsi ya kuja kwenye tuzo,” anaeleza Kavishe.

Anaongeza kuwa TBL imejipanga kuhakikisha kuwa wasanii wananufaika na tuzo hizo kwa namna nyingine kama vile kwa njia ya ushiriki kwenye matamasha ya muziki ambayo yatakuwa yakifanywa na TBL kwa ajili ya washiriki wa tuzo hizo mahiri kama Kili Tour.

Katika hilo, wasanii wa muziki wa dansi walilalamikia kuachwa katika ziara hizo ambapo walielezea kuwa kwao wanaona kuwa ni sawa na wametengwa. Rapa wa Bendi ya Mapacha Watatu, Khalid Chokoraa anasema kuwa suala la bendi kusafiri kwa pamoja kama inakuwa inahusisha msafara mkubwa zaidi ambapo kunakuwa na vifaa mbalimbali, wasanii wenyewe hadi wachezaji wa muziki (wacheza shoo).

“Ni kweli kuwa hii inakuwa na gharama lakini kwa upande wetu sisi hakuna shida kama Mapacha Watatu tunaweza kutumia CD na kuendelea kuimba kama kawaida,” anasema Chokoraa. Hoja ya uhalali wa wasanii kushinda tuzo hizo nayo imeibuka kati ya wasanii hasa ikizingatiwa na mfumo wa upigaji wa kura ulivyo kwa sasa.

Mfumo unaotumiwa ni kura moja kwa msanii mmoja katika kila kipengele kinachoshindaniwa na namba ya simu iliyotumiwa kwenye upigaji wa kura katika kipengele husika haiwezi kutumiwa mara mbili. Pia wasanii wanaweza kuomba kwa njia zao wenyewe kama vile kwa kutumia mitandao ya kijamii kama vile Twitter, Facebook, Instagram na njia nyingine.

Hoja hiyo ilimgusa msanii wa Kundi la Weusi Asili, Niki wa Pili ambaye ni msemaji wa kundi hili kuonesha wasiwasi wake kuwa wasanii wasiokuwa na marafiki wengine kwenye mitandao hiyo au wasiokuwa na uelewa kabisa wa matumizi ya mitandao hiyo kujikuta wakikosa kura.

“Mimi ninaona kuwa hiyo sio sahihi kwa kuwa wapo wasanii ambao hawana kabisa hiyo mitandao au hata kama wanatumia, lakini sio waelewa sasa hapa ina maana kwa wale wenye marafiki zaidi ya 5,000 au hata elfu kumi kabisa sasa iwapo wakipigiwa kura wanajikuta wamejiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kushinda,” anasema Niki wa Pili.

Kavishe anatumia mwanya huo kuwataka wasanii kujikita zaidi katika matumizi ya mitandao hiyo ikiwa kama wanataka kujitangaza sio tu kwa ajili ya kupata kura za kushinda Tuzo za Kili, ila hata katika maisha yao ya kila siku kama wasanii.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi