loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wasomi, lugha za Ulaya na Afrika: kati ya kujiweza na kuwezwa - 2

Wasomi, lugha za Ulaya na Afrika: kati ya kujiweza na kuwezwa - 2

Endelea.. MIAKA kadhaa iliyopita, nafikiri miaka mitatu iliyopita, bunge la Kenya huru lilipiga kura kuzipiga marufuku lugha za Kiafrika zisizungumzwe katika maeneo rasmi, kwa mfano maofisini. Kichekesho ni kwamba bunge hilo halingekuwako kama si kwa sababu ya wafanyakazi na wakulima wadogo wadogo wanaozungumza lugha hizo za Kiafrika kuingia msituni na barabarani ili kupambana dhidi ya serikali ya kikoloni.

Bila shaka bunge hilo halikuona kwamba mizizi yake inatokana na lugha za Kiafrika, bali inatokana na lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo za Ulaya. Sheria hiyo haijapitishwa kwa sababu tu Rais hakuitia sahihi. Lugha imekuwa ni medani ya mapambano ya fikra. Lakini ninalotaka kulizungumzia hapa ni kwamba lugha ni uwanja wa mapambano baina ya utumwa na harakati za kujikomboa na kujipa uwezo.

Historia ya lugha, ameandika Tom Paulin, mara nyingi huwa ni hadithi ya kutamalaki na kupora; ni hadithi ya kuziteka ardhi na kuziweka katika mamlaka ya walioziteka; au kuwalazimisha watu kufuata utamaduni fulani. Lugha, haidhuru iwe inatumiwa ndani au nje ya maeneo ya taaluma, imekuwa ni uwanja wa vitakatika hali zote-baina ya mtawala na mtawaliwa, hasa katika enzi za ukoloni.

Katika hali kama hizo, lugha imekuwa ni silaha ya kutamalaki au ni silaha ya kupinga kutamalakiwa, sawa na silaha kama upanga. Kwa hakika, vita vikali zaidi vimepiganwa, na vinaendelea kupiganwa katika eneo hili. Mshairi mmoja wa Kiingereza, Spencer, aliyeishi zama moja na Shakespeare, na ambaye aliandika kitabu maarufu, Fairie Queen, aliueleza vizuri umuhimu wa kutumia silaha ya lugha katika kutamalaki.

Katika mwaka 1599, aliandika kwamba; “Imekuwa ni kawaida kwa anayetamalaki kuidharau lugha ya anayemtamalaki na kumlazimisha kwa kila njia huyo anayemtamalaki kujifunza lugha yake (mtamalaki).” Spencer aliyaandika maneno haya katika kitabu chake A View of the Present State of Ireland.

Katika kitabu hicho alitetea kupigwa marufuku mfumo wa majina ya watu wa taifa la Ireland-kitendo ambacho lengo lake lilikuwa ni kuzifuta kabisa kumbukumbu za taifa hilo. Udhibiti wa mfumo wa majina ya Wananchi wa Ireland ulikuwa ni njia kuu iliyotumiwa na Waingereza kuitamalaki Ireland.

Kama alivyoeleza Tiny Crowley katika kitabu chake, War of Words: The Politics of Languages in Ireland -1537-2004, wavamizi mbalimbali wa Ufalme wa Uingereza walipitisha sheria kadhaa zilizokuwa na madhumuni ya kuilinda lugha ya Kiingereza isiingiliwe na kuathiriwa na lugha ya Ki-Ireland, Ki-Gaeli (Gaelic).

Moja ya mfululizo wa sheria hizo ni sheria ya Kilkenny ya mwaka 1369, baada ya Uingereza kuiteka na kuikalia Ireland. Kwa mfano, amri mojawapo ya sheria hiyo ilitishia kwamba serikali itamnyang’anya ardhi yake Mwingereza yeyote au mwananchi yeyote wa Ireland ambaye atazungumza na mwenzake kwa lugha ya kwao, kinyume na sheria hiyo.

Kwa hiyo Spencer aliyaandika maneno yake hayo kutokana na sheria hiyo, ambayo inaonyesha haikufaulu kama ilivyotarajiwa. Kwani kama ingekuwa na athari yoyote, Spencer asingekuwa na haja ya kutaka sheria hiyo itekelezwe baada ya zaidi ya miaka mia mbili kupita. Yeye Spencer mwenyewe alikuwa ni Mwingereza mlowezi (au setla) katika sehemu ya Munster.

Mmojawapo wa majirani zake alikuwa ni mlowezi mwenzake kutoka Uingereza, Walter Raleigh-ambaye ndiye aliyeanzisha makao ya walowezi Virginia, Amerika.

Inawezekana kwamba hakukuwapo na uhusiano wa moja kwa moja baina ya yaliyotokea Ireland wakati huo na yale yaliyowakumba Waafrika waliochukuliwa kwa nguvu kutoka Afrika na kwenda kufanywa watumwa katika mashamba ya Marekani yaliyomilikiwa na walowezi waliokuja baada ya kina Walter Raleigh.

Hata hivyo, katika mashamba hayo Waafrika waliotiwa utumwani hawakuruhusiwa kuzungumza kwa lugha zao. Hata mawasiliano ya kutumia ngoma pia yalikatazwa. Vilevile, hawakuwa na ruhusa ya kutumia majina yao ya Kiafrika. Na Waafrika waliopatikana wakizungumza lugha zao waliadhibiwa na hata wengine kuuliwa.

Lengo la yote hayo lilikuwa ni lile lile: kuwasahaulisha uhusiano wao na kwao walikotoka. Japan nayo ilifanya kama hivyo baada ya kuitamalaki Korea: iliwalazimisha Wakorea kutumia lugha ya Kijapani na mfumo wa Kijapani wa kupeana majina. Sera hiyo ilitupiliwa mbali baada ya Japani kushindwa vita ya pili ya dunia.

Lakini athari ya sera hiyo ingali ipo: Mpaka hivi karibuni, ndani ya Japan kwenyewe, wenye asili ya Korea walilazimika kuwa na majina ya Kijapani. (Shahidi wa hili ni Esther W. Dungumano, Mkurugenzi wa uhusiano wa kimataifa wa Chuo hiki cha Dar es Salaam. Yeye anakichapa Kijapani kama yuko Tokyo!) Katika bara la Afrika, baada ya kulivamia na kulitamalaki, Wafaransa, Waingereza na Wareno, walifuata sera kama hizo.

Ingawa wakoloni hao hawakuzipiga marufuku lugha za Kiafrika, lakini waliziteremshia hadhi yake ya kuwa lugha zenye uwezo, maarifa na kuwa ni kitambulisho cha wenye lugha hizo. Hata kama waliziruhusu lugha hizo kutumiwa katika mfumo wa elimu, ilikuwa ni katika hatua za mwanzo mwanzo tu kabla ya wanafunzi kugeuzwa na kuwa wasemaji wa Kiingereza au Kifaransa.

Siijui sheria yoyote ya utawala wa kikoloni iliyopiga marufuku majina ya Kiafrika. lakini kutokana na athari za mamlaka ya kiutamaduni karibu kila Mwafrika aliyepata elimu ya kisiasa ameliambatanisha jina la kizungu katika jina lake la kiafrika. Sera za kikoloni kuhusu lugha zilikuwa zinaendeleza sera za vita ya kutamalaki kwa kutumia mbinu za kilugha.

Kulikuwa na muingereza mmoja: jina lake ni Macauley. Yeye alikuwa ameajiriwa katika kampuni ya British East India ambayo ndiyo ilikuwa inatawala India. Yeye ndiye aliyependekeza sera za kutumia kiingereza kwa kuwasomesha badala ya kihindi au Sanskrit. Yeye alisema, “lazima tuwe na kikundi cha wahindi ambao kwa rangi ya ngozi ni Wahindi lakini kwa akili ni Waingereza.

Kikundi hiki kitakuwa kati yetu na umma tunaoutawala. Fikra kama hizi ndizo zilipelekwa kwa makoloni mengine ya waingereza. Kikundi au tabaka ambalo kwa ngozi ni Waafrika, kwa ubongo ni waingereza. Tazama kitabu chake, Empires of the World

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Ngudi Wa Thiong'o

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi