loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watanzania tujifunze kutoka fainali za Brazil

Yapo mengi ambayo Tanzania tunahitaji kujifunza kutoka kwenye mashindano haya ambayo macho na masikio yote duniani yameelekezwa huko. Tuanze na uzalendo.

Kwa wanaofuatilia mashindano haya baada Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kuipitisha Brazil kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia 2014, wananchi wa nchi hiyo waliingia mitaani kupinga kuteuliwa kwake.

Haikuwa rahisi kwa Serikali ya Brazil kwa kuwa wananchi nao walikuwa na hoja ya kupinga mchakato mzima kutokana na hali ya maisha ilivyo nchini humo.

Walichodai ni kwamba taifa lina hali mbaya kiuchumi hivyo gharama hizo zingeelekezwa kwenye mahitaji ya moja kwa moja ya wananchi badala ya kujenga viwanja ambavyo vinatumia fedha nyingi, lakini havitumiki ipasavyo baada ya mashindano.

Pamoja na maandamano ya hapa na pale, Serikali ilitumia busara kubwa na hatimaye kuwezesha mashindano hayo kufanyika na kuwaunganisha tena raia wa nchi hiyo wanaozidi milioni 200.

Tumeona kupitia luninga na vyombo mbalimbali vinavyoripoti michuano hiyo moja kwa moja, mshikamano ulipo sasa kutoka kwa mashabiki waliojitokeza kuipa sapoti timu yao na kuwashangilia muda wote.

Kitendo cha kushikamana, kimeiwezesha nchi hiyo kuanza vyema. Hili la uzalendo kwa hapa Tanzania ni la muhimu sana kujifunza kwani, mara ngapi mashabiki wanagawanyika uwanjani pale timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ ikiwa mwenyeji wa timu za nje.

Tumeshuhudia mashabiki wakiwazomea, kuwalaumu wachezaji kila wafanyapo makosa madogo madogo na wakati mwingine kuingiza ushabiki wa klabu mbili kongwe nchini, Simba na Yanga.

Matokeo, badala ya kuwapa moyo wachezaji ili wawe na morali wakiwa nchini mwao, huwakatisha tamaa na mwisho ni kuharibu zaidi uwanjani kwa kukosa sapoti ya Watanzania kuwa nyuma yao.

Tunaamini Watanzania walio wengi wanapenda soka na watatumia muda wao mwingi katika mashindano haya kuangalia mechi mbalimbali nchini Brazil.

Pamoja na kufurahia ushindi wa timu wanazozipenda, lakini ni wakati muafaka kuangalia mambo mengine muhimu ili mwisho wa mashindano haya, tujifunze kitu fulani, kwa ajili ya maendeleo ya soka letu.

Ukiachana na suala la uzalendo, lakini kuna mambo mengi yakiwemo ya nidhamu na uvumilivu kwa wachezaji na mashabiki. Nidhamu na uvumilivu kwa wachezaji uwanjani ni vitu muhimu sana, hasa pale panapotokea utata wa maamuzi kutoka kwa refa na wasaidizi wake.

Kwa kuwa mashindano haya yanaangaliwa na watu wa kada mbalimbali hapa nchini, tunaamini kila kada, kuanzia kwa mashabiki wa kawaida, viongozi wa vyama vya michezo, viongozi wa klabu, waamuzi, makamisaa na wadau wengine wa soka, watumie fainali hizi kujifunza jambo fulani.

Ni kwa pamoja, mwisho wa siku, kila kada ikiunganisha nguvu ya kile ilichoona kinahitaji kuigwa Brazil, tutaweza kurekebisha kasoro zilizopo hivi sasa zinazotukwaza kushiriki katika mashindano mbalimbali.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi