loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watoto wenye ulemavu waorodhesha changamoto

Inanipa wakati mgumu sana." Hicho ni kilio cha Jerida Godfrey, mwanafunzi mwenye ulemavu wa wa kusikia anayesoma katika shule ya msingi Mugeza Viziwi alichotoa kwa lugha ya alama huku mwalimu wake, John Kahangwa akitafsiri.

Anasema watu wenye ulemavu wa kutosikia na kutoongea wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kuonekana watu wenye ujeuri na wakati mwingine kutopata huduma sahihi pale wanapokwenda kwenye maeneo kama hospitali kwa kuwa hakuna wakalimani.

Anafafanua kwamba kwa vile unakuta daktari haelewi, anapata wakati mgumu na hivyo anaweza kuamua kuandika dawa yoyote ambayo haiendani na ugonjwa aliyonao mlemavu wa kutosikia.

“Hali hiyo ilinikuta wakati fulani. Nilikuwa naumwa koo, nikaenda katika kituo cha afya. Nikajieleza kwa mhudumu niliyemkuta hakuelewa na badala yake alisema huyu kichaa naye ananisumbua.

Alitamani kunifukuza nitoke katika ofisi yake lakini kwa ung'ang'anizi tu nikaambulia kuandikiwa panadol huku akinionesha kwa ishara kuwa nimpishe.

Ingawa sisikii lakini mtu akiongea namtazama mdomo na vitendo, naweza kutambua kuwa anamaanisha nini kwangu. Hali hiyo iliniuma sana na nilijenga hasira hata nikikutana na huyo daktari natamani kumpiga jiwe,” anasema.

Anasema amegundua kwamba watu wenye ulemavu wa kusikia wamekuwa wakionekana kama watu waliojaa ujeuri, jambo ambalo limekuwa linasababisha wengi wao kunyimwa hata nafasi za kazi katika taasisi na ofisi mbalimbali hata kama wamesoma kwa kiwango kinachotakiwa.

Anasema mlemavu wa kutosikia na kuongea anaweza kukosea njia, akapita sehemu isiyoruhusiwa kama jeshini.

Pale anapokamatwa na kuulizwa maswali na yeye anajibu kwa lugha ya alama watu wasiofahamu watadhani ni dharau, wanaweza kumpa kipigo lakini kama kungekuwepo mkalimani kusingekuwa na tatizo kubwa.

Ni kwa mantiki hiyo, Jerida anaiomba Serikali kwa niaba ya wenzake wenye ulemavu kama huo, kuwekewa wakalimani angalau hata mmoja katika kila sehemu inayotoa huduma nyeti kama hospitalini, vituo vya polisi, mahakama, halmashauri za miji, benki na kadhalika.

Mwanafunzi mwingine wa shule ya msingi Mugeza Mseto wanaposoma watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali, Gideon Meshack (14) ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino), anasema tangu kuibuka kwa wimbi la watu wanaosaka viungo vya albino wamekuwa wakiishi katika hali ya wasiwasi.

“Sisi watoto albino kwa kuhofia kuuawa tunapofanikiwa kuletwa katika makambi au shule maalumu kama hii nilipo, tunashindwa kurudi nyumbani wakati wa likizo kwa kuhofia kuuawa, lakini sisi bado tunahitaji kuwa karibu na familia zetu. Hata pale tunapobaki shuleni, mwalimu anayekuwa zamu hupata kazi kubwa kwani hulazimika kufanya kazi masa 18, ikiwa ni pamoja na kusaidiana na mlinzi kuimarisha ulinzi dhidi yetu pamoja na kufundisha," anasema Meshack.

Anaiomba serikali kuimarisha ulinzi zaidi kwa watoto wenye ulemavu kila mahala, ikiwa ni pamoja na kambini ili waishi kwa amani kama watoto wengine.

"Kwa kweli hata sisi watoto tunataka likizo tuwe na wazazi, kwa hiyo ni muhimu serikali ihakikishe amani kwa albino inakuwepo wakati wote na kila mahala," anasema akimaanisha inauma kuona wenzao wanakwenda likizo kuungana na wazazi wao, lakini wao wanabaki shuleni kwa sababu ya hofu tu. Rogas Chachely ni mlemavu wa viungo ambaye pia ni katibu wa baraza la watoto wenye ulemavu mkoani Kagera.

Yeye anasema wao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi mojawapo, ikiwa ni jamii kuwa na mtizamo hasi dhidi ya watoto wenye ulemavu.

Anasema bado kuna wazazi wanaowaficha watoto wenye ulemavu ndani ya nyumba kwa mitazamo potofu tu kwamba ulemavu ni laana, aibu au mikosi katika jamii.

Anasema bado katika jamii kuna watoto wanaotelekezwa na wazazi wao, hasa wazazi wa kiume, pale mama anajifunguapo mtoto mwenye ulemavu kwa kuhofia kuchekwa na kufedheheshwa na jamii.

Anasema kwa mantiki hiyo, watoto kadhaa wenye ulemavu wanakosa haki zao za msingi, ikiwa ni pamoja na haki muhimu ya kupata elimu kutokana na mitazamo potofu ya baadhi ya wazazi.

Anazitaja changamoto nyingine wanazokabiliana nazo watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali kuwa ni uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika shule mbalimbali wanazosoma walemavu.

Anafafanua kwamba namna nzuri ya kumsaidia mtoto mlemavu ni kumpa elimu itakayomsaidia kupambana na changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupata kazi.

Lakini anasema tatizo linakuja kwamba hata unapofika kwenye shule maalumu hakuna vifaa vya kutosha vya kufundishia na kujifunzia.

Walemavu wa macho hawana mashine za kuandikia za kutosha, karatasi na hata fimbo maalumu za kuwasaidia kutembea huku albino wakiwa hawana miwani, kofia maalum za kujikinga na jua pamoja na mafuta yanayosaidia wasishambuliwe na saratani ya ngozi.

Pia anasema kuna changamoto za miundombinu mbalimbali kutofikika kwa urahisi, siyo mashuleni pekee bali hata katika majengo ya umma.

Miundombinu hiyo anaitaja pia kwamba ni pamoja na vyoo, madarasa, ngazi za kuingia kwenye majengo, vyombo vya usafirishaji na kadhalika.

Changamoto nyingine anasema ni watoto wenye ulemavu kutoshirikishwa katika maamuzi kuanzia ngazi ya familia hadi za juu pamoja na uhaba wa walimu wenye taaluma ya kufundisha walemavu.

Kwa mfano anasema, ukiondoa vyuo vikuu viwili vitatu, kwa sasa chuo pekee cha ualimu kinachotoa elimu maalumu kwa walimu ni Patandi kilichoko mkoani Arusha.

Wilfred Wilbard, mwenyekiti wa baraza hilo mkoani Kagera anasema kuwa kupitia baraza lao wamekuwa wakipendekeza na kuiomba Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu endelevu juu ya watoto wenye ulemavu.

Na pia wamekuwa wakiomba kila chuo cha ualimu kutoa elimu maalumu ili kupatikana walimu wengi zaidi. Pendekezo lao lingine anasema ni kuanzishwa kwa shule za watoto wenye ulemavu kila wilaya kama ilivyoanzishwa za kata.

Anasema kama shule hizo zitaanzishwa itasaidia watoto wengi wenye ulemavu kupata huduma ya elimu katika maeneo yao kuliko hivi sasa ambapo kuna shule moja kwa kanda nzima ya ziwa inayohudumia watoto viziwi ya Mugeza.

Anasema mapendekezo yao mengine ni serikali kuwachukulia hatua kali wazazi wanaowaficha watoto wenye ulemavu majumbani na wale wanaowafanyia vitendo vya kinyama, yakiwemo mauuaji ya kikatili kwa albino.

Anasema ni muhimu kwa serikali itenge bajeti ya kutosha kwa kila Halmashauri kwa ajili ya kuwahudumia watoto wenye ulemavu ikiwemo kuyawezesha mabaraza ya watoto hao.

Anasema baraza la watoto wenye ulemavu mkoani Kagera lilianzishwa mwaka 2013 kwa lengo la kuwaunganisha watoto ili kuwa na sauti moja katika kutetea na kulinda haki zao.

Mwalimu John Kahangwa ambaye ni mwalimu wa Shule ya Mugeza Viziwi, anasema kuwa shule hiyo inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini Magharibi ambapo huhudumia wanafunzi kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Simiyu, Geita na Shinyanga.

Hata hivyo, anasema kutokana na uchache wa nafasi huwalazimu kupokea wanafunzi kumi tu kwa mwaka kati ya zaidi ya wanafunzi 50 wanaoshinda kanda nzima, jambo ambalo husababisha walio wengi kukosa nafasi.

Kahangwa anasema hali hiyo inawafanya watoto wengine ambao hawakupata nafasi kurudi nyumbani na kusubiri kuomba mwaka mwingine na pengine hata mwaka unaofuata hawapati nafasi, hivyo wanaendelea kubaki nyumbani na kukosa haki yao hiyo ya msingi.

Anasema shule hiyo inakabiliwa changamoto mbalimbali, ikiwemo upungufu wa walimu ambapo mwalimu mmoja huhudumia watoto 12 tofauti na sheria za kimataifa ambazo zinaelekeza kuwa walimu wawili wafundishe watoto kumi.

Pia anaomba Serikali kwa niaba ya walimu wenzake wanaofundisha katika shule maalum za watu wenye ulemavu kuboresha utaratibu na kupanua miundombinu ya kufundishia na kusomea kwa watoto wenye ulemavu sambamba na kuongeza mishahara kwa walimu hao, kwani hufanya kazi nyingi hata nje ya muda wa kazi.

Anasema wanakabiliwa pia na tatizo la wazazi kuwatelekeza watoto wao mara wanapowaleta shule na kupokewa na uongozi.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Angela Sebastian

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi