loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watumishi changieni ndugu zenu mfuko wa CHF

Pamoja na kupenda kwetu iongezwe, huenda hilo likawa ni tatizo kwa upande wa serikali ingawa ipo namna nyingine ya kuzidi kuimarisha bajeti ya afya nchini.

Tunasema hivyo kwa kuwa ni ukweli ulio wazi kwamba hali yetu ya kutegemea zaidi washiriki wetu wa maendeleo kutusaidia pengine katika bajeti hii hata kuliko ushiriki wetu wa ndani unaweza kuwa chanjo kikuu cha matatizo yetu kwa sasa.

Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa kwa kuwategemea sana, wakati wakijiondoa au kuchelewa kutekeleza ahadi zao washirika wetu wa maendeleo katika mfuko wa pamoja ndio kumesababisha athari za moja kwa moja katika miradi ya afya, ambayo ilijadiliwa na kuelezwa kwamba itatekelezwa.

Kutokana na ukweli huo ipo haja ya kuanza polepole kujenga uwezo na utamaduni wa ndani wa kuchangia sekta ya afya ambayo inamhusu kila mmoja wetu.

Tunaipongeza Serikali kwa kuongeza mchango wake katika bajeti ya sekta ya afya ya mwaka huu kama mchango wa ndani. Tunaamini kuwa majadiliano yanayoendelea sasa bungeni yatatoa kipaumbele kwa sekta hii ili angalau ipewe fedha kama zilizotengwa katika mwaka wa fedha uliopita.

Tunaungana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Selemani Rashid kuwaomba wananchi wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kuwa na uhakika wa huduma za matibabu maeneo wanayoishi.

Tunajua wapo watumishi wengi wa umma ambao ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wanaonufaika na huduma za mfuko huo, wakati ndugu zao wengi walio vijijini hawana utaratibu wowote wa uhakika wa matibabu.

Sisi tunaona ipo haja kwa watumishi hawa kuwachangia ndugu zao katika mfuko wa afya ya jamii ambao mchango wake ni kati ya shilingi elfu tano hadi elfu ishirini kwa mwaka kwa kaya.

Tunaamini kama watumishi hawa wanaokadiriwa kuwa laki tatu walio serikalini na wengineo wakiamua kwa dhati kuwachangia walio vijijini, hatua hiyo mbali ya kuwaondolea usumbufu wa kuombwa fedha za matibabu kila mara, italiwezesha taifa kuwa na vyanzo imara vya ugharamiaji wa huduma za afya kupitia uchangiaji.

Hakuna muarobaini mwingine au muujiza wowote wa kulikwamua taifa katika suala hili, tuanze sasa kuhimizana kushiriki kwa staili hiyo ili tuwaokoe ndugu zetu lakini pia kuanzisha utamaduni wa kutumia vyanzo vya ndani kuimarisha sekta ya afya na hasa tiba.

Pamoja na kutoa rai hiyo, pia tunawaomba wanaohusika waendelee kuchukua hatua za dhati za kukabiliana na changamoto zinazoikabili mifuko ya uchangiaji afya tukiamini kwamba elimu zaidi iendelee kutolewa ili watu wahamasike katika makundi, mtu mmoja mmoja kujiunga katika mfumo wa tiba wa CHF.

Aidha tunawaomba wadau wetu wa maendeleo mnaoendelea kutuunga mkono katika sekta ya afya muendelee na ukarimu wenu kwani tunathamini sana mchango wenu ambao unatuwezesha kupiga hatua mbele katika juhudi za kuimarisha sekta ya afya na jamii.

Wakati tukiwaomba muendelee kutushika mkono na sisi tunajipapasa kuweza kujizatiti katika kuimarisha huduma za matibabu na afya hapa nchini.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi