loader
Watumishi wa Afya Rukwa wachangia benki ya damu salama

Watumishi wa Afya Rukwa wachangia benki ya damu salama

Takwimu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, zinaonesha kuwa asilimia 95 ya damu inayopatiakana katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa inatumika kwa kuokoa maisha ya akina mama na watoto lakini upatikanaji wa damu hiyo ni duni sana.

Mathalani kwa mwaka uliopita kiwango cha mahitaji wa damu hospitalini hapo ilikuwa chupa 3,000 lakini iliyoweza kupatikana na kutumika zilikuwa chupa 1,1164..

Kutokana na hospitali hii ya mkoa wa Rukwa kukabiliwa na upungufu mkubwa wa damu, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa , Dk John Gurisha alihamasisha watumishi wa afya , watumishi kutoka Ofisi ya Katibu Tawala mkoani hapa, Manispaa, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, magereza askari polisi kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ili kuweza kunusuru maisha ya wagonjwa hususani wajawazito na watoto.

Ingawa Dk Gurisha alitoa tangazo kuhamasisha uchangiaji wa damu katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa inayofanyika Julai 25 kila mwaka, mwitikio ulikuwa mdogo.

Watu waliofika katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa kuchangia damu ni wachache wa sekta ya afya wakiwamo wauguzi, mafamasia, daktari wa meno wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa Dk Gurisha ambapo ni chupa 100 za damu zilikusanywa katika.

Dk Gurisha anawahimiza wakazi wa mkoa wa Rukwa kujitolea kutoa damu kwa kuwa mahitaji ya damu hospitalini hapo ni makubwa na hakuna njia nyingine ya kupata damu zaidi ya kuchangiwa na jamii.

Gurisha amewataka watumishi na viongozi kuwa mstari wa mbele kujitolea kutoa damu kama njia ya kuhamasisha wananchi kuunga mkono kampeni ya kuchangia damu salama ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu hasa wanawake na watoto.

“Wakati tukiwa majukwaani tunakuwa mstari wa mbele kuwalalamikia wananchi hawajitokezi kuchangia damu ili kunusuru maisha ya wagonjwa hususani wajawazito na watoto wachanga lakini leo ni viongozi wachache tu waliojitokeza kutoa damu….jamani tujitokeze na kuonesha mfano bora,” Gurisha anahimiza.

Gurisha anasema licha ya kuwataarifu watumishi wa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa, Manispaa, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga pia Mkuu wa Magereza, Kamanda wa Polisi wa Mkoa kwamba kujitokeze kuchangia damu hawakujitokeza kuungana na watumishi wa sekta ya afya kuchangia damu.

Anasisitiza kuwa ili damu ipatikane lazima jamii wakiwemo watumishi wa umma na viongozi mbalimbali wajitokeze na wachangie damu ili kunusuru maisha ya watu wanaokufa kwa kukosa damu.

Shirika la Msalaba Mwekundu na kikundi cha hamasa kilitoa matangazo na kupita nyumba hadi nyumba pia walipita katika taasisi za watu binafsi na za umma, lakini mwitikio bado hauridhishi kwani walitegemea kupata watu wengi tofauti na idadi iliyojitokeza.

Dk Gurisha anasema upungufu wa damu unasababisha wagonjwa wanaohitaji damu kupata tiba pungufu madhalani, mgonjwa anayehitaji kuongezewa chupa tatu za damu anapewa chupa moja au nusu chupa na kuruhusiwa kurejea nyumbani kwa kuwa hakuna damu ya kumuongezea.

“Wagonjwa wengi wanaohitaji damu wanakufa ili hali Tanzania ina watu wengi wenye damu safi na salama….Jamani tujitahidi kujenga utamaduni wa kujitolea damu ili kuokoa maisha ya wenzetu maana ukitoa damu hupati madhara yeyote,” anaeleza Dk Gurisha.

Anasema wapo watu wanaosita kutoa damu kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamioja na imani potofu, imani za kidini ambapo baadhi ya ya madehebu ya dini yanazuia waumini wake kuchangia damu au kuongezea damu pindi wapougua .

Gurisha anasema amewahi kushuhudia muumini wa moja ya madhehebu ya kidini alikataa katakata mtoto wake mwenye upungufu wa damu asiongezewe damu na hatimaye yule mtoto alikufa.

Baada ya kifo cha cha mwanawe yule mzazi alisema ni bora afe kwa sababu imani ya dini yake haimruhusu kuchangia wala kuongezewa damu kwa sababu damu ni kitu chenye thamani kubwa na hakistahili kuchezewa ovyo ovyo.

Sababu nyingine anabainisha kuwa ni kuwepo kwa baadhi ya makundi ya watu wanasita kujitokeza kuchangia damu wakihofia kupimwa kwanza afya zao.

“Bila shaka ni elimu tu imekosekana kwani ni jambo jema na la busara kwa mtu kujua afya yake”, anasema Dk Gurisha.

Anafahamisha kuwa mtu unapojitolea kuchangia damu kwanza anapimwa afya yake kujua kama ana maambukizi ya magonjwa ya homa ya ini, magonjwa ya zinaa kama kaswende na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

“Isitoshe kabla ya mtu kupimwa damu yake lazima kwanza apatowe ushauri nasaha ili aweze kukubaliana na matokeo pia ni njia mojawapo ya kujikinga na maambukizi ya Ukimwi," anasisitiza Gurisha.

Anasema sababu nyingine inayowafanya watu kusita kuchangia damu ni hofu kuwa damu hiyo itaibiwa na watumishi wa afya na kuuzwa jambo ambalo sio kweli.

“Nikiri kuwa hospitalini hapa bado sijaripotiwa visa vya wataalamu wa afya kuiba damu na kuiuza lakini ule usemi usemao kwa samaki mmoja akioza wote waliomo dengani wameoza mimi nasema kama akibainika mtumishi yeyote mwenye tabia kama hiyo hakika ataadhibiwa mara moja…kama samaki mmoja ameoza basi aondolewe mara moja kwenye tenga ili asisambaze harufu mbaya kwa wengine “ anasisitiza.

Anasema kutokana na dhana kwamba damu inaibiwa na wauguzi kumekuwa na tabia kwa baadhi ya watu wanaojitolea damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya ndugu zao kulazimisha warudishiwe damu inayobaki ili waondoke nayo, jambo ambalo haliwezekani kwa kuwa kuna utaratibu wa kutunza na kuharibu damu kwa kuichoma.

“Naiasa jamii itoe taarifa mara moja ikimbaini mtumishi yeyote wa afya mwenye tabia ya kuuiba na kuuza damu isitoshe wasiinunue damu hiyo bali watoe taarifa katika vyombo vya dola ikiwemo Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa,“ anasisitiza .

Kwa upande wake, Meneja wa Maabara Hospitali ya Mkoa wa Rukwa, Oliva Nguma anakiri kuwa uchangiaji wa damu ni changamoto kubwa kutokana na muitikio mdogo.

Watu wenye sifa za kujitolea kuchangia damu ni wenye umri wa miaka kati ya 18 na 60 lakini hawajitokezi ipasavyo.

Watu wanaostahili kuchangia damu ni wenye umri kati ya miaka 18 hadi 60 lakini kwa kukwepa kuchangia damu jamii sasa imekuja na mbinu mpya ….ndugu wanapobaini kuwa mgonjwa wao atalazimika kuongezewa damu, basi mgonjwa huyo husindikizwa na ‘bibi’ au ‘babu’ wenye umri wa miaka zaidi ya 80.

“Au wasindikizaji wanakuwa akina mama wanaonyonyesha au wajawazito ambao hawana sifa hiyo ya kuchangia damu…hali hii inasikitisha na ni aibu kwa wale wanaofanya hivyo,“ Nguma anaeleza.

Hata hivyo, anasisitza kuwa hamasa ya uchangiaji wa damu lazima ianzie vijijini kwani idadi kubwa ya wakazi mkoani humo hawana mwamko kabisa wa kuchangia isitoshe hawaoni umuhimu wa kujitolea damu, jambo linalosababisha kutokana wajawazito na watoto kupoteza maisha yao.

Alibainisha kuwa tatizo la upungufu wa damu hospitalini hapo ni changamoto kubwa hasa wakati wanafunzi wa vyuo na shule wanapoendeka makwao kwa likizo kwa kuwa ndio wenye muamko wa kuchangia damu.

Mchangiaji damu ambae pia ni mganga wa meno, katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa, Dk Emanuel Mtika anaeleza kuwa amehamasika kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wengine.

Mtika anasema ni vyema kujenga tabia ya kuchangia damu kwa kuwa leo unaweza kuchangia mwingine na wewe ukachangiwa kesho hivyo ni vyema kuonesha upendo na kusaidiana.

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Peti Siyame,Sumbawanga

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi