loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watupori: Kabila linalong’ang’ania kuishi porini

Ni makazi mapya ya Basarwa - Watupori wa Kalahari, wakazi wa asili wa eneo hilo la Kusini mwa Afrika na bado hawajafurahia heshima hiyo waliyopewa. Madada wawili, Boitumelo Lobelo (25) na Goiotseone Lobelo (21), wanaonekana wameinama kwenye beseni lenye maji machafu, wakifua nguo za watoto wao.

Macho yao yanaonekana kugubikwa na hasira wakati wakizungumzia maisha yao ya hapa, kijiji kilicho umbali wa mwendo wa nusu siku kwa gari kutoka makazi yao ya awali, ambayo hivi sasa ni sehemu ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Kahalari ya Kati (CKGR). “Nakumbuka nyumba yangu na jinsi tulivyokuwa tukiishi.

Maisha yalikuwa rahisi, kulikuwa na matunda mengi, wanyama na hakukuwa na baa wala bia. Hivi sasa tumepotea,” anasema Goiotseone.

Wamekuwa wakirudi kupatembelea tangu walipohamishwa, lakini hivi sasa hawaruhusiwi kukaa huko tena. Walipokuwa na umri wa miaka tisa na mitano, Boitumelo na Goiotseone walihamishiwa New Xade pamoja na wazazi wao. Wanazungumzia maisha waliyoyapenda kwenye hifadhi, ambako walikuwa wakiamka kila asubuhi na kuungana na wanawake kijijini kuokota matunda na kuchimba mizizi kwa ajili ya chakula. Lakini Goiotseone naye anakumbuka siku waliyolazimishwa kuondoka.

Watupori hao ndio wakazi asilia wa Kusini mwa Afrika – walioondolewa na vikundi vya Wabantu waliokuja kutoka Kaskazini na Wakoloni kutoka Ulaya.

Hivi sasa wakiwa wamebaki 100,000 –wengi wakiwa katika nchi za Botswana, Namibia, Afrika Kusini na Zambia, kimila wanaishi kwa kuwinda wanyamapori, kuokota matunda na kuchimba mizizi.

Wakiwa katika makundi tofauti ya kikabila, baadhi wanaliona jina la Watupori kama tusi lakini kundi hili linasema hivyo ndivyo wanavyostahili kuitwa. Pia San, Basarwa na Khoisan – ingawa pia baadhi ya majina ya makabila haya yanachukuliwa kuwa matusi.

“Polisi walikuja, wakavunja nyumba zetu na kututupa nyuma ya malori na mizigo yetu na kutuleta hapa. Walitutelekeza hapa kama si binadamu,” Goiotseone aliliambia Shirika la Habari la Uingereza, BBC.

Wawili hawa ni kizazi kipya cha Basarwa: Wanakwenda shule na wamejifunza Kiingereza na lugha ya Kitswana, ambacho kinazungumzwa kwa upana sana Botswana. Lakini wanasema maisha haya mapya yanawagharimu sana.

“Tunaambukizwa Ukimwi na magonjwa mengine tusiyoyajua; vijana wanakunywa pombe; wasichana wanazaa watoto. Kila kitu hapa ni kibaya,” Boitumelo analalamika.

Maelfu ya Watupori waliishi katika eneo kubwa la jangwa la Kalahari miaka kwa miaka. Lakini leo wengi wao wameondolewa, wengi kwa nguvu, na kuhamishiwa kwenye kambi zilizoandaliwa na Serikali, kutoka porini.

Watupori wa Botswana wamekuwa kwenye mgogoro na serikali kwa zaidi ya miaka 15 sasa, kutokana na masuala ya kisheria juu ya haki zao za kuishi ndani ya hifadhi – na kuendelea na maisha yao ya jadi kama wawindaji waokotaji. Kuna wakati walikataliwa kupata maji kwenye mapori hayo.

Visima vyao vilifunikwa na kupigwa marufuku kuchimba vingine. Mahakama ya Rufaa ya Botswana katika hukumu yake ya mwaka 2011 kuhusu suala hilo, ilielezea hatma ya Watupori hao kama “simulizi ya kutisha juu ya mateso ya binadamu na kukata tamaa” na kuamua waruhusiwe kuchota maji.

Leo wengi wanasema amri za mahakama zilizowatetea wao, zinapuuzwa na maofisa wa serikali. Wanahitaji vibali vya kuingia maporini na kuruhusiwa kuwinda. Bila kibali, wanaokutwa wakiwinda wanakamatwa. Kwa nini walihamishwa?

Serikali inasema hatua ya kuzuia watu kurudi eneo hilo inalenga kuhifadhi wanyamapori na uoto wa asili wa hifadhi hiyo, ambayo ni kubwa kidogo kwa eneo kuliko Denmark.

Lakini vikundi vya haki za binadamu na Watupori hao wanaamini kwamba sababu inayotolewa haina uzito. Uchimbaji madini ni moja ya tasnia muhimu nchini Botswana, huku almasi ikiwa ni chanzo kikubwa cha mapato.

Makazi ya zamani ya Watupori yako katikati mwa eneo lenye madini mengi ya almasi. Watu hao wanaamini kwamba walihamishwa ili kupisha mradi wa mabilioni ya dola wa uchimbaji madini katika eneo hilo.

Kampuni kubwa ya uchimbaji almasi iliyosajiliwa London, Uingereza imeanza mipango ya kuchimba madini hayo umbali wa takriban kilometa 45 kutoka mpaka wa Mashariki wa hifadhi hiyo.

Ujenzi wa awamu ya kwanza wa mradi huo ulianza mwaka 2011. Unatarajiwa kuanza uchimbaji mwaka huu, kwa kuanza na uzalishaji wa tani 70,000 za almasi ghafi. Serikali siku zote imekanusha kuwapo kwa uhusiano kati ya kuhamishwa kwa watu hao na ugunduzi wa akiba ya almasi, iliyogundulika kwa mara ya kwanza katika miaka ya themanini.

Serikali imeshaweka huduma mbalimbali katika kambi: Kuna zahanati, shule na nyumba zilizowekwa uzio – ikiwa ni sehemu ya kubadili eneo hilo kuwa la kisasa zaidi.

Lakini maisha ya kisasa hayamfurahishi kila mtu: Basarwa wamejenga vibanda katika maeneo yao, kama kukumbuka maisha yao ya zamani yenye furaha na ya kimila.

Watupori hao siku zote wamekuwa wawindaji na wanasema hawajawahi kupata ujuzi unaotakiwa katika kufuga ng’ombe. Ukosefu wa ajira ni mkubwa na jamii hii haina ujuzi wa maana, au angalau hata wa kutumika nje ya jamii yao.

Duka la pombe la kijiji halikosi wateja. Si ajabu kuona vijana wanayumba wakitoka kwenye vibanda vya kuuzia pombe katikati ya mchana.

Si tu maisha bali mazingira ya kijamii nayo yanaongeza tatizo. Ni kawaida kukuta mamia ya ng’ombe na wachungaji wao wako chini ya miti ya miba wakijiandaa kwa safari ya kilometa tano kutafuta eneo la karibu la malisho.

Watupori walipohamishwa, kila familia ilipewa ng’ombe au mbuzi watano ili kuwatia moyo wa kuwa wafugaji na wakulima. Lakini kuwa mfugaji kuna changamoto zake pia.

“Ukimlazimisha mtu kuishi maisha fulani asiyoyajua, atakabiliwa na ugumu,” anasema mkulima kutoka jamii ya watupori, Jumanda Galekebone. “Watu wetu hawajui jinsi ya kuhudumia ng’ombe wanapougua, hawajui magonjwa ya mifugo kama ya miguu na midomo,“ anafafanua.

“Maisha haya hayajasaidia kuboresha maisha yao.Bado kuna watu wengi wanaingia msituni kuwinda na kukamatwa. Baadhi yetu hapa tunakabiliwa na adhabu za mahakamani kutokana na kuwinda. Hiyo inathibitisha, kwamba huwezi kulazimisha mabadiliko kwa watu,” anasema Galekebone.

Lakini inaonekana Watupori hao hawana jinsi ila kubadilika, kufuata – angalau kama mipango ya serikali inavyobaini. Baadhi wanaamini kwamba maisha wanayoishi hayako katika jamii ya sasa ya Botswana. Baadhi ya maofisa wa serikali wamekuwa wakiwaita “wakazi wa maeneo ya mbali”, watu wa enzi za mawe, ambao wanatakiwa kuingizwa kwa nguvu katika karne ya 21.

Mwaka 2006, uamuzi mwingine wa Mahakama ulisema uamuzi wa serikali kukataa kuruhusu Basarwa kuingia CKGR ni kinyume cha Katiba.

Wengi wameruhusiwa na maofisa wa Serikali kurudi mbugani, lakini wale tu ambao majina yao yalionekana kwenye nyaraka za Mahakama. Kiongozi wa jumuiya hiyo, Roy Sesana ni mmoja wao. Lakini anasema hafurahii ushindi huo. Hivi sasa anaishi kati ya CKGR na New Xade ili kuwa karibu na familia na watu wake.

“Tumetenganishwa na watoto na wake zetu. Ni aina gani hii ya maisha? Hatukufanya kosa lolote kustahili hali hii,” anasema. Sesana alikuwa mmoja wa walalamikaji wakuu katika kesi kadhaa dhidi ya serikali. Kwa watu ambao wametumia muda mwingi wa maisha yao wakitembea kwa uhuru ndani ya ardhi hii, wakiwinda wanyamapori na kuokota matunda kwa chakula, eneo hili haliwapi fursa ya kuacha ardhi hii.

“Tumezoea kujilisha-hivi sasa tu wategemezi wa misaada ya serikali, tunageuzwa wavivu na wajinga,” anasema Sesana. Tunafanywa kama mbwa. Mbwa ndicho kitu pekee ambacho hakiwezi kujiletea chakula nyumbani. Anatakiwa kusubiri mmiliki wake ampe chakula.”

Vikundi vya kimataifa vya haki za binadamu vinatoa mwito wa kususia tasnia ya utalii ya Botswana, ambayo ni chanzo kikubwa cha pili cha mapato mpaka hapo serikali “itakapoacha kushitaki wakazi hao wa kwanza wa nchi hii.”

Rais Ian Khama, ambaye anaonekana kuelewa sana linapokuja suala la kusimamia hali ya Watupori ameshatangaza kuwa uwindaji katika maeneo yanayodhibitiwa utaharamishwa siku yoyote mwezi huu.

“Uamuzi huo ulilazimishwa na kuwapo taarifa za kisayansi zinazoonesha kuwa aina nyingi za wanyamapori zinapungua,”Khama aliliambia Bunge.

Alisema Watupori watafunzwa jinsi ya kutumia rasilimali zao vizuri. Lakini watu hao wanashikilia kwamba maisha yao ya kuishi kwa amani na mazingira hayo kunathibitisha kuwa hawana athari kimazingira. Wanasema badala yake hatua hiyo ni jaribio la kutaka kuua utamaduni wao.

“Sehemu pekee ambako utamtambua Mtupori hivi sasa ni katika nguo za kijadi zilizozungukwa na nyumba za kitamaduni katika vijiji vya kitalii,” anasema Sesana.

“Tunaogopa kwamba siku zijazo, hakutakuwa na mtu ambaye ataonesha utamaduni wa Watupori isipokuwa kwa kujipanga mbele ya watalii kwa ajili ya kampuni zinazowatumia kwa biashara,” anasema. *Imetafsiriwa kutoka kwenye mitandao.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi