loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wawekezaji waanza kusaidia ujenzi wa miundombinu Kahama

Kampuni ya African Barrick inayonamiliki migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi imeanza ujenzi wa miundombinu ya barabara ambayo itakuwa chachu ya maendeleo wilayani hapa.

Hatua ya Barrick pia inatoa changamoto kwa makampuni mengine yaliyowekeza Kahama kufuata nyayo kwa kurudisha faida katika jamii kwa kuchangia huduma mbalimbali.

Kabla ya hatua ya sasa, wananchi wa Kahama walikuwa wakilalamika kuhusu ushiriki wa wawekezaji katika kusaidia shughuli za maendeleo dhana ikiwa kwamba wawekezaji wamekalia kuvuna bila kuchangia maendeleo ya maeneo husika.

Malalamiko ya chini chini na hata ya wazi yalikuwepo licha ya wawekezaji wa madini kusaidia katika baadhi ya huduma za jamii kama vile afya, elimu na maji lakini sasa imedhihirika kuwa kiu kubwa ya wana-Kahama ilikuwa barabara za mji ambazo zilikuwa mbovu.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, anasema hapo nyuma kulikuwa na mahusiano mabaya baina ya wawekezaji wanaowekeza katika Wilaya ya Kahama pamoja na uongozi wa Serikali ya Wilaya.

Anasema alichokuja kugundua baadaye ni kwamba wawekezaji hawana matatizo bali wanachohitaji ni mahusiano mazuri baina yao na wananchi waliopo katika eneo husika, hususani maeneo yanayopakana na miradi yao.

“Mimi nilikwenda moja kwa moja kwa mwekezaji wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi na kuongea naye kuhusu hali ya barabara mjini ilivyo mbaya. Akaahidi kunisaidia katika kuhakikisha barabara hizo zinajengwa,” anasema Mpesya.

"Nilipeleka ombi langu hilo kwa niaba ya Wanakahama. Mwekezaji alikubali kutoa kiasi cha Sh bilioni 4.6 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami mjini Kahama zenye urefu wa kilometa 5," anasema.

Katika kuhakikisha kuwa ahadi hiyo inatekelezeka Mkuu huyo wa Wilaya ya Kahama anasena aliwaita wazee wa mji huo na kuwashirikisha katika kuchagua ni maeneo yapi yanayopaswa kujengwa barabara hizo kwanza na kufikia muafaka baina yao. Kadhalika alitumia mwanya huo kujenga mahusiano mema baina ya wawekezaji na wananchi.

Mbali na mwekezaji huyo kusaidia katika suala zima la miundombinu ya barabara katika Mji wa Kahama, Kampuni Barrick imeahidi pia kuendelea kusaidia juhudi za serikali katika huduma mbalimbali za kijamii kama vile afya, elimu pamoja na maji kwa wananchi wa Mji wa Kahama.

Mkuu wa Wilaya anasema katika mchakato wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo, Kampuni ya CHICO kutoka China ndio iliyoshinda na kwamba ndiyo inayoendelea na ujenzi.

“Tunaomba ushirikiano wenu wananchi kwa wawekezaji kwani watu hao hawana shida katika suala zima la maendeleo. Jitahidini kuwapa ushirikiano ili Kahama yetu iweze kupata maendeleo kwa kuwatumia wawekezaji hawa,” anasema Mpesya.

Kwa upande wa mgodi wa Bulyanhulu, Mkuu huyo wa Wilaya anasema tayari ameshafanya mazungumzo na uongozi wa mgodi ambapo pia umeahidi kusaidia huduma za jamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu.

Aidha Mpesya anasema kuwa wawekezaji hao wameahidi kuweka mtandao wa maji kutoka katika mgodi huo hadi katika Kata ya Lunguya, hatua ambayo itapunguza tatizo la maji katika eneo hilo na kwamba pia wameahidi kusaidia katika ujenzi wa shule za sekondari pamoja na zahanati katika kata za Bugarama na Bulyanhulu.

Baadhi ya wadau wa maendeleo katika Wilaya ya Kahama wametoa shukrani zao kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama na kumtaka aongeze bidii katika kuhakikisha kila mwenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya Kahama anafanya hivyo.

Paul Ntelya, mmoja wazee katika Mji wa Kahama amesifia juhudi zinazofanywa na Mpesya na kuahidi kumpa ushirikiano pale panapohitajika akisifia namna alivyowashirikisha wazee wa Kahama katika mchakato mzima wa kuamua ni barabara zipi zipewe kipaumbele kwanza.

“Sisi wazee tunajua kila kiongozi ana mapungufu yake lakini Mkuu huyu wa Wilaya yuko katika msitari sahihi wa kuibadilisha Kahama," anasema Paul Ntelya na kudokeza kwamba baadhi ya viongozi waliopita walikuwa wazuri lakini walikuwa wakiharibiwa na baadhi ya watendaji walio chini yao pamoja na kushindwa kuwashirikisha walengwa katika maendeleo yao.

Mzee Ntelya anamtaka Mkuu wa Wilaya kutokata tamaa katika kuwasaidia wananchi wa Kahama na kumuomba kuwashauri wawekezaji hao kutokata tamaa katika kuwasaidia wananchi wa Mji wa Kahama hasa katika sekta za miundombinu ambayo bado ni mibaya isiyoendana na na namna mji huu unavyokuwa kwa kasi.

“Unajua Mji wa Kahama unakuwa kwa kiwango kikubwa na hivyo unahitaji barabara za uhakika hasa katika kipindi kama hiki cha masika,” anasema Ntelya.

Anasema kuwa unaweza kuona kwa sasa barabara zinatengenezwa mjini kwa kiwango cha lami lakini kuna baadhi ya wanasiasa watajitokeza na kusema wao ndio wameweka nguvu kubwa katika kufanikisha ujenzi huo kumbe hizo zote ni nguvu za Mkuu wa Wilaya, Benson Mpesya.

Wilaya ya Kahama pamoja na kuwa na vyanzo vingi vya mapato lakini miundombinu yake hususani ya barabara hazifanani na sifa inayopewa wilaya hiyo.

Baadhi ya watu wameshauri kwamba wakati mwekezaji anasaidia ujenzi wa barabara za Kahama, Serikali pia isijibweteke, bali iongeze juhudi kuifanya Kahama iwe na barabara nzuri kuliko ilivyo sasa.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Raymond Mihayo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi