loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Wezi wa fedha za wakulima wakishikishwa adabu nitalipa deni’

Kwa nyakati tofauti, Rais Kikwete ametumia muda mrefu mkoani humo kuzungumzia wizi huo na anasema jambo hilo limemchosha, hayupo tayari kuendelea kulivumilia, lazima wezi wakamatwe na washitakiwe mahakamani ili wizi huo ukome. Rais anasema, amekuwa akibeba madeni ya vyama vya ushirika ili vifanye kazi lakini sasa anataka kufahamu si tu namna vyama hivyo vilivyopata hasara lakini pia uhalali wa madeni husika, na hatalipa fedha zilizoibwa.

“Siwezi kufanya biashara hii ikawa ya kudumu nataka kujua mmepataje hasara, kama ni uzembe au michongo hapana, silipi,” anasema Rais mjini Tunduru wakati anazungumza na viongozi wa mkoa wa Ruvuma.

“Haiwezekani Serikali ikawa inafidia watu walioiba, hata mwanao akiwa hivyo ataendelea,” anasema na kubainisha kwamba, baadhi ya wakulima ni mawakala wa wanunuzi wa mazao, kuna watumishi wa Serikali wanazunguka kununua mazao, na pia baadhi yao ni mawakala wa wafanyabiashara. “Na nitashangaa kama hawafanyi,” anasema.

“Vyama vya ushirika vimeingiliwa na wezi, sasa vyama vya ushirika vimekuwa mawakala wa kampuni hii, kampuni ile,” anasema Rais Kikwete na kutoa msimamo kuwa hawezi kuendelea kutumia fedha za Serikali kulipa madeni yaliyotokana na wizi. “Vyama vya ushirika kazi yake ni kumkomboa mkulima…nithibitishieni kwanza uhalali wa serikali kulipa hiyo bilioni 2.6,” anasema na kuagiza kuwa, kwanza walioiba wakamatwe, washitakiwe, washikishwe adabu, yeye atalipa deni.

“Hatuwezi kuviacha viendelee, watu watakuwa hawana woga, watakuwa wanasema we kula tu Serikali italipa…wanateseka wananchi ambao hawana hatia,” anasema na kuongeza kuwa, wakati wa uchaguzi kwenye vyama vya ushirika, kuna watu wanahonga wachaguliwe.

Wakati anazungumza na wananchi mjini Namtumbo, Rais Kikwete alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu, awakamate wote walioshiriki na kuiba fedha za wakulima wa tumbaku wilayani Namtumbo, akishindwa amuambie yeye.

Anamweleza Mwambungu kuwa, Mkuu wa Mkoa ana mamlaka ya kufanya hivyo na kwa kuwa aliunda tume (Mwambungu) na imeshampa matokeo ya uchunguzi hana sababu ya kuendelea kunyamaza kwa kuwa watuhumiwa wapo hivyo wakamatwe haraka, na washitakiwe mahakamani.

Ameagiza kuwa, wezi wote walioibia wakulima wa tumbaku katika wilaya hiyo wakabidhiwe polisi, na hata kama ni watumishi wa Serikali wasimamishwe kazi, washitakiwe. Anasema, maofisa wa ushirika waliowaibia wananchi wamefanya kosa la jinai, wanastahili kukamatwa na kushitakiwe ili wasiibe tena.

“Hili jambo ndugu zangu, baya, baya, baya sana,” anasema Rais Kikwete na kumwelekeza Mwambungu kuwa, asikubali wananchi wailaumu Serikali kwa makosa ya watu wengine, na amewataka wananchi waache kuchagua viongozi wezi, kwa kuwa wakati mwingine wanailamu Serikali na Chama cha Mapinduzi(CCM) wakati makosa ni yao. “Mkuu wa Mkoa uliunda Tume, umepata majibu, una mamlaka kamili… Kesho wapelekwe Polisi, ukishindwa niambie mimi,” anasema.

“Halafu mnailaumu Serikali kwani tulishirikiana kuchagua?” anauliza Rais Kikwete. “Wakulima wamechagua wenyewe kiongozi wao, kawaibia wenyewe halafu wanailaumu Serikali,” anasema. “Washitakiwe tuondokane na tabia hii, vinginevyo tabia hii itakuwa haiishi,” anasema Rais. “Vyama vya ushirika si vyama vya Serikali, kazi ya serikali ni ukaguzi,” anasema Rais Kikwete mjini Tunduru na kubainisha kuwa, maofisa ushirika wana wajibu wa kusimamia utendaji wa vyama hivyo.

Anaagiza Polisi wawakamate wote waliowaibia fedha wananchi hao, wawekwe ndani ili sheria ichukue mkondo wake. ”Safari nyingine msijaribu kuchagua viongozi wezi,” aliwaeleza wananchi. “Hawa wameiba, ni kosa la jinai, na kosa la jinai Serikali ndiyo inayoshitaki…kuna ukame wa viongozi waaminifu, na kwenye vyama vya ushirika kuna ukame wa viongozi waaminifu,” anasema Rais Kikwete.

“Naomba hili deni liwe halali… mkiendelea na watu wa aina hii, tukaendelea kuwafuga hatufiki… sasa nalipa deni kumbe mwenzangu anaenda kuoa, usajili wa dirisha dogo,” anasema.

Anasema, kwa kuwa Serikali ni mdhamini wa vyama vya ushirika, ina wajibu wa kulipa deni lakini liwe halali. “Serikali lazima ilipe deni kwa haki, isilipe deni la walioiba…lakini tunataka tulipe kwa halali baada ya kujiridhisha,” anasema Rais na kutamka kwamba, wakimridhisha atalipa, wakishindwa halipi.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi