loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wivu ulivyochelewesha filamu ya Tito

Wivu ulivyochelewesha filamu ya Tito

Makundi mbalimbali ya sanaa yalianzishwa na kujipatia umaarufu mkubwa, kama ilivyokuwa kwa Fukuto, Kaole, Kidedea na mengine. Hata hivyo, mwisho wake ni mpasuko mkubwa na hata kufa kabisa kwa makundi hayo, na kushindwa kurudi na kufikia malengo waliyopanga mwanzo.

Lakini tofauti kwa waigizaji, Mrisho Zimbwe maarufu kama Tito Carlos na mwigizaji mwenzake Pamela Brown ambaye sasa ni mkewe anayejulikana kwa jina la Shadya Brown.

Walipoamua kuungana kwa ajili ya kufanya kazi pamoja ya filamu, na kujikuta katika vituko na mikasa iliyopelekea hata kutaka kutoa roho ya mmoja wapo, na hatimaye wanatimiza malengo kwa kukamilisha filamu hiyo ingawa kulikuwa na kusuasua kwa muda mrefu. Kukamilika kwa filamu ya Kizazi ambayo mwanzo ilikuwa ikijulikana kama DNA, na nilipoona baadhi ya scene na kugundua ni filamu nzuri na yenye kuvutia, kulinifanya nifanye mahojiano na Tito ambaye ndiye mwenye filamu.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Tito anasema tayari ameshaikamilisha filamu hiyo, ambayo ina zaidi ya miaka mitatu na miezi kadhaa. Anasema kukamilika kwa filamu hiyo ni baada ya misuguano ya muda mrefu na kuamua kuyaweka matatizo yao pembeni.

“Tumepitia misukosuko mingi ya maisha, lakini tumeamua kuikamilisha na sasa inatarajia kuingia sokoni muda si mrefu,” anasema. Miongoni mwa misukosuko ambayo ilitokea wakati wakiifanya filamu hiyo ni Pamela kutingwa na kazi, hivyo akawa sehemu ya uongozi wa filamu na sio mwigizaji.

Hata hivyo baada ya filamu hiyo kuanza miezi kadhaa, ndipo patashika likaibuka baada ya Pamela kutokuwa na imani na mwigizaji wa kike aliyeigiza na mumewe. Maelewano yakawa hayapo ukizingatia yeye pia ni kiongozi, maafikiano yaliyoamuliwa ni kuondoa sehemu zote ‘scene’ alizoigiza yule mwigizaji wa kike, ikawa sababu ya Pamela kuamua kuingia mwenyewe na kushika nafasi hiyo.

Ingawa alishika mwenyewe nafasi zote alizotaka kuigiza yule mwigizaji wa kike, vikaja kuchanganyika na kazi kwani yeye ni muajiriwa wa kampuni ya magazeti ya serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya HabariLeo, HabariLeo Jumapili, SpotiLeo, Daily News na Sunday News. Hali hiyo ilimfanya kukosa muda wa kuigiza na kupelekea filamu kuendelea kubaki kimya.

Tito anasema, wakati wakiendelea na harakati za kucheza filamu hiyo, likatokea tukio lingine kubwa kiasi cha nusura kutoa roho ya mmoja wa wapenzi hao, pale mwaka 2011 Tito kupata ajali mbaya.

Tito anasema baada ya matatizo ya muda mrefu na mpenzi wake kabla ya kuwa mkewe, kipindi hicho akiwa mjamzito, ulitokea ugomvi mkubwa kati yao ambao alishindwa kuvumilia ndipo alipoamua kuondoka nyumbani Magomeni, na kuelekea Bilicanas kwa ajili ya kupunguza mawazo.

Akiwa katika klabu hiyo ya usiku pamoja na Ben Branco, anasema akili zake zilikuwa zikimchanganya zaidi akaamua kujituliza kwa kunywa pombe. Anasema ilipofika saa saba, ndipo walipoamua kubadili klabu na kutaka kwenda Maisha. Ilibidi kutumia usafiri wa pikipiki ambayo mara nyingi alikuwa akiutumia, ingawa wenzake walimkataza lakini hakuweza kusikiliza hata kidogo.

Ilibidi kufuatana na wenzake waliokuwa ndani ya gari, na yeye akiwafuata nyuma kwa pikipiki. Hapo ukichanganya pombe, na mawazo mazito alipofika daraja la Salenda, akajikuta akiwaza zaidi juu ya mpenzi wake na hata kupelekea kushindwa kuidhibiti pikipiki na kujikuta akipata ajali kubwa.

“Kukosa kofia ya kujikinga hatari pindi pikipiki inapopata ajali nilinusurika kupasuka kichwa,” anasema. Katika ajali hiyo, alichubuka vibaya sana na hata kulazwa na baadaye kutolewa huku akiwa bado ana matatizo ya kichwa. Hapo ndipo familia ilipokuja juu na kutaka aachane na huyo mwanamke (Pamela) na mpango wa filamu yao ya DNA ukawa umeishia hapo.

Ilichukua miezi kadhaa kati ya Tito na Pamela kila mmoja akiamini hatoweza kurudiana na mwenzake, lakini kila mmoja alijikuta na wakati wake, wakajilaumu na kurudiana tena. Kuungana kwa mapenzi yao suala la kuiendeleza filamu ya DNA lilirudi tena na kuwa na imani, ipo siku litaisha.

Katika tukio lingine ambalo hawatakuja kulisahau baada ya kujifungua mtoto wao, ambaye pia ni wa kwanza kwao anayeitwa Natalia lilikuwa ni suala la kugombana mpaka kufikishana mahakamani wakati huo wakiwa wameshafunga ndoa tayari. “Lilikuwa tatizo jipya ndani ya familia, lakini likawa kubwa sana kiasi cha kufikishana mahakamani,” anasema.

Wivu wa mapenzi ulizidi kutawala, kiasi cha kipigo kuwa sehemu ya maisha yao na hata kutokuwa na maelewano hadi kufikishana mahakamani. Mwaka 2012 baada ya kufungua kesi na ndipo mambo yalipovunjika tena, na kusitisha filamu ya DNA na ndipo Tito aliamua kutaka kutoa sehemu zote alizomweka mkewe na kumweka mtu mwingine.

Lakini ukubwa wa gharama ulimfanya asubiri, huku akihudhuria mahakamani baada ya kufikishwa na mkewe. Hata hivyo wakati kesi yao ikiendelea mlalamikaji akiwa Pamela na familia yake, juu ya Tito mambo yalikuwa tofauti kwao. Kesi iliendelea na wakati huo wakijisuluhisha wenyewe nyumbani, hadi mwisho wa siku wakawa wanatoka katika chumba kimoja kwenda kwenye kesi, jambo ambalo liliangusha mshangao mkubwa kwa watu wanaowajua.

Kweli mapenzi ya watu usiyaingilie, leo hii Tito anasema tayari wameshamaliza migogoro yao yote na wameshakamilisha filamu ya DNA, ambayo wameamua kuipa jina la Kizazi. “Filamu muda wowote inaweza kuingia sokoni, na tumeona haina haja ya kuendelea kulumbana na kupoteza fedha nyingi”.

Tito jina lake halisi ni Mrisho Salehe Zimbwe akiwa ni mtoto wa tano, mzaliwa wa Tanga pia ni baba wa watoto watatu, Amina, Abdulmajid na Natalia. Baada ya kuingia jijini Dar es Salaam, alijiunga na kundi la sanaa la Kaole mwaka 2002 na kuwa miongoni mwa wasanii wa mwanzo wa kundi hilo.

Filamu yake ya kwanza kuigiza ni Chumba Na 77 ambazo zilikuwa filamu za mwanzo, na kuleta mapinduzi makubwa hadi sasa. Filamu ambazo amekuwa akifanya vizuri ni zile za mapambano, kwa kuwa watu aliokuwa akifuata nyayo zao ni Jimmy Master na Kaini.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Mohamed Mussa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi