loader
Dstv Habarileo  Mobile
Yanga imefungwa na mfumo sahihi wa Simba

Yanga imefungwa na mfumo sahihi wa Simba

Kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya hasimu wake mkubwa Simba kimekuja huku timu hiyo yenye maskani yake katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani ikiamini ina kila sababu ya kuwafunga wapinzani wao hao wakubwa.

Yanga ilifungwa na Simba iliyotumia zaidi ya miaka mitatu kuandaa wachezaji chipukizi na kuwaunganisha na wazoefu kadhaa na kuonyesha kandanda safi kwenye mechi hiyo iliyovuta hisia kubwa kutoka kwa mashabiki wa soka nchini.

Amis Tambwe alifunga mabao mawili moja likiwa kwa njia ya penalti kabla ya Awadh Juma ‘Maniche’ chipukizi aliyesajiliwa na Simba wakati wa dirisha dogo akitokea Mtibwa Sugar akifunga bao la tatu, lakini shujaa wa mechi hiyo alikuwa Ramadhani Singano’Messi’.

Singano ama Messi alitokana na kikosi cha pili cha Simba chini ya Jamhuri Kihwelo’Julio’ na baadaye Selemani Matola aliyefanikiwa zaidi katika timu hiyo kwa kutwaa kombe la Uhai na lile la Super8 ambalo sijui limekufia wapi.

Singano, Haruna Chanongo, Saidi Ndemla na Jonas Mkude walitokana na kikosi cha pili cha Simba na ndio walioongoza mauji hayo kwa Yanga kwa namna kama ile walivyofanya walipoongoza mauji dhidi ya Mtibwa Sugar iliyosheheni nyota wenye uzoefu katika mashindano ya kombe la Super8 ambayo Yanga haikushiriki.

Salumu Sued ‘Kussi’, Shaabani Kisiga ‘Malone’, Yusuf Nguya na wakongwe wengine walitolewa nishai na kikosi cha pili cha Simba cha akina Singano, Wiliam Lucian, Ndemla, Edward Christopher, Chanongo na wengineo ambao leo hii ni muhimili wa Simba na wameifunga Yanga katika namna kama ile walivyoifunga Mtibwa Sugar.

Yanga ilikuwa na majina makubwa kama vile Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa, Khamisi Kiiza, Kelvin Yondani, Emmanuel Okwi, Athumani Iddi ‘Chuji’ na wengineo ilidhaniwa kuwa ingeweza kupata ushindi mnono kwenye mechi hiyo. Kwanini imetokea hivyo?

Jibu la swali hili liko wazi ni majibu rahisi kwa maswali magumu yanayoikabili timu hiyo, kwamba haina mshambuliaji wa maana basi ipande ndege na kumnunua kwa gharama kubwa mshambuliaji inayomtaka (Okwi) na sio kuumiza kichwa kutengeneza wa kwao.

Haina beki wa kati jibu ni kwenda kumsajili Mbuyu Twite kwa mbwembwe kutoka Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) na sio kumuanini chipukizi wao Issa Ngao na kumjengea uzoefu na baadaye kuja kuwa na msaada mkubwa katika klabu hiyo.

Hata katika zama hizi ambazo beki wao Nadir Haroub ’Cannavaro’ ambaye akili inataka lakini mwili hautaki Yanga inashindwa kuwaamini akini Ngao, Rajabu Zahir na wengineo?. Kipindi hiki ambacho kiungo Chuji akili yake inataka lakini mwili hautaki Yanga haiamini kama chipukizi Khamis Thabiti anaweza kubeba jukumu la kiungo huyo mkongwe na ambaye ameshapoteza nafasi kwenye kikosi cha Taifa Stars sababu kubwa ikiwa umri.

Yanga ina chipukizi wengi wenye uwezo tena katika uwiano ambao ni kama sawa tu na Simba lakini tofauti yao ni kwamba Simba inawaamini chipukizi wake lakini Yanga yenyewe bado ikiogopa kuwatumia kwa kuogopa lawama kutoka kwa mashabiki wao wenye hulka ya kuucheza mpira kuliko wachezaji wao.

Reliants Lusajo ni mshambuliaji ambaye kama Yanga itaamua kumtumia anaweza kuja kuwa kama Mbwana Samatta kutokana na kipaji alichonacho, ana uwezo wa kumiliki mpira kwa namna ya utulivu, uwezo wa kufunga mabao lakini pia ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi kuanzia namba 8, 9 na 10 lakini bado klabu hiyo inakificha kipaji cha chipukizi huyo kutoka Machava ya Kilimanjaro.

Lini watavifichua vipaji vya akina Abdallah Mguhi ‘Messi wa Yanga’ Relients Lusajo, Issa Ngao, Rajabu Zahir, Khamisi Thabiti ambao wakichanganywa na chipukizi wengine kama akina David Luhende, Frank Domayo timu yao inaweza kuwa moto wa kuotea mbali, ni Bin Kleb, Seif Ahmed ‘Magari’ na wengineo ndio wanajua kwani inategemea zaidi utashi wao.

Kikubwa Yanga imefungwa na mfumo sahihi wa kupata timu wa klabu ya Simba na sio kitu kingine na hadi hapo itakapoamini juu ya mfumo huo uliowahi kuiletea mafanikio makubwa klabu hiyo ndipo itapata mafanikio na kushinda mechi zake nyingi sio kuifunga Simba pekee.

Iliwahi kufanikiwa katika mfumo wa kuamini chipukizi na ikawa inaifunga Simba kama ilivyotaka kipindi cha akina Silvatus Ibrahim ‘Polisi’ Anwar Awadh ’Kaito’ Mzee Abdallah ambao iliwachanganya na chipukizi walioanza kupata uzoefu kama vile Salvatory Edward, Ally Yusuph ‘Tigana’ katika ya miaka ya 1990.

Kama kuna kitu Yanga inakosea basi ni hiki cha kushindwa kuamini chipukizi na kama kuna kitu ambacho Simba imepatia basi ni kuamini chipukizi wao, ifikie mahala itoe nafasi kwa chipukizi wake kama ambavyo mahasimu wao wanafanya kama inataka kufanya vizuri katika medani ya soka.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Clecence Kunambi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi