loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yanga ina kila sababu kuifunga Al Ahly

Ni mechi ya kihistoria na Yanga imepanga kufanya maajabu leo, ikipania kuifunga miamba hiyo ya Afrika. Pengine hilo linawezekana kutokana na matokeo ya Yanga katika mechi kadhaa zilizopita.

Yanga inaingia uwanjani ikiwa katika mwenendo mzuri kuanzia kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara pamoja na michuano hiyo ya kimataifa, ikijivunia ubora wa safu yake ya ushambuliaji ambayo siku za karibuni imekuwa na makali mithili ya kiwembe, kufuatia kufunga idadi kubwa ya mabao.

Tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imevuna pointi 10 kati ya 12, ilizotakiwa kuzipata na imefunga mabao 10 katika mechi hizo nne ilizocheza, rekodi ambayo inaonesha ubora wa kikosi hicho kuelekea katika mchezo huo wa leo dhidi ya Al Ahly.

Katika mechi moja ya mwisho iliyocheza Jumamosi iliyopita Yanga, kabla ya kukutana na Al Ahly leo, safu yake ya ushambuliaji imefunga mabao saba, jambo ambalo linatoa matumaini ya mabingwa hao wa Tanzania huenda ikapata ushindi mnono kutokana na ukali wa safu yake ya ushambuliaji.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga ilionesha umahiri wake wa kufunga idadi kubwa ya mabao katika mechi ya raundi ya awali ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Komorozine ya Comoro. Katika mchezo wa marudiano mabingwa hao wa Tanzania walipata ushindi wa mabao 5-2, na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 12-2 baada ya kushinda mabao 7-0 katika mechi ya kwanza.

Kutokana na mwenendo mzuri na kasi waliyonayo Yanga kwa sasa ukichanganya na maandalizi ambayo wameyafanya ikiwemo kwenda Uturuki kupiga kambi, hakuna shaka timu hiyo ina kila sababu ya kuhakikisha inashinda mchezo huo wa leo bila kujali jina la timu au majina ya wachezaji wa timu pinzani.

Kuongezeka kwa mshambuliaji Emmanuel Okwi kwenye kikosi cha Yanga katika mechi ya leo kunaweza kuwa moja ya faida ambayo vijana wa Jangwani wanatakiwa kuitumia vizuri, ilimradi kuhakikisha wanautumia vizuri uwanja wa nyumbani na wanapokwenda Misri, tayari wawe na uhakika wa kusonga mbele.

Nasema Okwi anaweza kuwa faida kwenye mchezo huo kwa sababu mshambuliaji huyo machachari ni mwepesi wa kufunga mabao. Al Ahly watakuwa wanamjua vizuri winga machachari wa Yanga, Mrisho Ngasa aliyefunga mabao sita, matatu katika kila mechi dhidi ya Komorozine kutokana na kocha wao kumshuhudia mchezaji huyo kwenye mchezo na Wacomoro hao uliofanyika hapa nchini.

Wakati mabeki wa Al Ahly watakuwa wakihangaika na Ngasa, Okwi anaweza kutumia nafasi hiyo kufanya maangamizi kwa sababu kocha wa Al Ahly hakumuona kwenye mchezo dhidi ya Komorozine kutokana na utata uliokuwepo kwenye usajili wake. Kwa upande wa wageni Al Ahly, pamoja na kuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, lakini hawana mwenendo mzuri kwenye ligi ya Misri.

Kuna uwezekano isiweze kutetea ubingwa wake kutokana na nafasi iliyopo. Al Ahly iliyopo kwenye kundi la kwanza kwenye ligi ya Misri, imepoteza michezo yake mitatu iliyocheza hivi karibuni na inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi 16 baada ya kushinda mechi tano na kutoka sare mchezo mmoja.

Faraja pekee kwa Al Ahly ni ushindi wa mabao 3-2, iliyoupata kwenye mchezo wa fainali ya Super Cup, uliochezwa Alhamisi iliyopita Jijini Cairo dhidi ya mabingwa wa Kombe la Shirikisho, CS Sfaxien ya Tunisia. Katika upande wa ufungaji, Al Ahly, inawategemea zaidi washambuliaji wake wawili ambao pia huichezea timu ya taifa ya Misri, Mohamed Afas, maarufu kama Gedo, anayevaa jezi namba 15, na chipukizi Amr Gamal anayevalia jezi namba 17.

Gamal anashika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji katika Ligi ya Misri, akiwa na mabao sita nyuma ya Mghana John Antwi Duku anayeichezea klabu ya Ismailia. Kimaandalizi, Al Ahly inaonekana kutofanya maandalizi makubwa kama yale ya Yanga iliyolazimika kupiga kambi Uturuki kwa ajili ya michuano hiyo, na kutetea ubingwa wao wa Tanzania Bara.

Lakini pia, kwa upande wa upachikaji mabao, Al Ahly kwa sasa hawajaifikia Yanga iliyofungwa mechi moja kati ya 17 ilizocheza mpaka sasa. Baada ya kuligundua hilo ndiyo maana hata Al Ahly, walipogundua watacheza na Yanga kwenye hatua hiyo, wamekuwa wakiwafuatilia kwa karibu kutaka kujua mbinu zao, na walitaka kuja kupiga kambi nchini katika Hosteli za Azam, lengo likiwa ni kuwatoa mashindanoni.

Hata hivyo, hilo halikuwezekana baada ya uongozi wa Azam kukataa ombi hilo. Hizi ni sababu muhimu ambazo zinaifanya Al Ahly, ambazo endapo wachezaji wa Yanga watazingatia vizuri maelekezo ya walimu wao, wanaweza kuipoteza Al Ahly. Wachezaji kama Didier Kavumbagu, Okwi, Ngasa, Kiiza na wengine ambao watapata nafasi leo, hawatakiwi kufanya makosa.

Itakuwa ni furaha kwa viongozi, wanachama na mashabiki wa soka Tanzania kuiona Yanga hatimaye imevunja mwiko wa kunyanyaswa na Waarabu. Wachezaji wa Yanga, wanatakiwa kulichukulia hili kama chanzo cha wao kuhakikisha wanacheza kwa jihadi na kuwavua ubingwa Al Ahly, kama ilivyofanya Simba mwaka 2003, ilipowatoa mabingwa watetezi Zamaleki.

Lakini kufanya vizuri kwa Yanga katika mchezo huo, kutafungua milango kwa wachezaji wa Tanzania kupata soko kimataifa kwani mechi hiyo inafuatiliwa kwa ukaribu kimataifa. Kukua kwa soka la Tanzania, kunatokana na kufanya vizuri kwa klabu zake kwenye michuano ya kimataifa kama hii ambayo Yanga inashiriki.

Al Ahly inapocheza nyumbani, hupata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wake ambao huwa na mchango mkubwa kwa timu hiyo kupata matokeo mazuri. Hali hiyo ijitokeze pia leo kwa mashabiki wa Yanga na Watanzania kwa ujumla kwani Yanga kwa sasa inapeperusha bendera hya taifa. Kila la heri Yanga, hakuna shaka mchezo wa leo mtapambana na kuhakikisha bendera ya Tanzania inapepea vyema.

MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Godwin ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi