loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yanga, Simba imebaki utamaduni

Hata waweza kusema ni miaka ya soka ya Tanzania, Yanga na Simba. Mchezo huu ulitakiwa kuchezwa Jumapili iliyopita ila kutokana na mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa timu ya Taifa, Taifa Stars dhidi ya Benin, ulisogezwa mbele hadi leo, Jumamosi Oktoba 18, 2014.

Upinzani wa Simba na Yanga upo tangu enzi na enzi, hata kabla ya Uhuru na bado unaendelea na watu bado wanaudumisha utamaduni huu ambao wameurithi tangu enzi hizo. Hapa cha kujiuliza je, upinzani ule wa Simba na Yanga wa enzi zile bado upo hadi leo? Na utaendelea kudumu milele na milele?

Jibu ni kwamba kweli upinzani upo ila hauna hadhi ile na utaendelea kwa ajili ya tamaduni zetu tu za kupenda kuishi kwa mapokeo au mazoea. Swali jingine kama utaendelea ni kwa faida ya nani hasa? Na utaendelea kwa faida ipi hasa? Kwa faida ya kutunisha matumbo ya watu na kujipatia fedha lukuki kila unapochezwa mchezo wa Simba na Yanga au kwa faida ya soka la Tanzania? Hilo ni swali gumu ambalo linahitaji majibu sahihi.

Jibu ni jepesi mno hapo utamaduni wa Simba na Yanga utadumu kwa faida ya watu wachache ambao wapo tayari kuwalipa mamilioni ya fedha waganga ili kujitengenezea majina labda ya kuingia kwenye siasa na kujipatia fedha lukuki na si kwa maendeleo ya soka la Tanznaia, hilo ninakataa tena.

Kuna baadhi ya watu wao wanaomba tu mechi ya Simba na Yanga ifike ili wavune fedha na wengine ili waendeleze biashara zao ambazo zilianza kuyumba au wengine wapate fedha waende wakamalizie kujenga nyumba zao ambazo zilisimama kwa kukosa fedha za kuwalipa mafundi.

Mechi ya Simba na Yanga ni mipango ya watu ambao wameshajiweka sawa tangu ratiba ya Ligi Kuu ilivyotoka ili kujipatia manoti siku hiyo na kutunisha matumbo yao na kuwafilisi wavuja jasho ambao ni wachezaji.

Usione watu wapo tayari kuipeleka hata timu nje ya nchi kwa ajili ya kuweka kambi kwa kujiandaa na mechi hiyo ya upinzani wa jadi, bali ni kwa faida yao tu, maana wanajua baada ya mchezo, kuna kitu kizuri kinakuja mbele yake nacho sio kingine, bali ni noti au fedha kwa lugha sahihi.

Wana imani mashabiki wakiona moja ya timu hiyo imeenda kuweka kambi sehemu nzuri, basi itawavutia mashabiki kujazana uwanjani siku ya mchezo na wao hiyo ndio furaha yao maana baada ya mchezo, mambo lazima yawe mazuri. Wakati ninyi mashabiki na wapenzi wa hizo mkizimia uwanjani kwa presha ya mchezo husika wao, wanaomba mchezo umalizike haraka ili wakahesabu mapato ili wajue wamepata nini na wagawane vipi hakuna kingine kwao, hayo mengine ni kazi kwenu.

Hivi sasa najua baadhi ya watu wameshatengeza vitabu kibao tu vya tiketi bandia kwa ajili ya kuziuza kimagendo na kujipatia fedha kwa maana hii leo ni siku ya mavuno kwao hakuna tena mchezo wa faida kama huu kwenye Ligi Kuu. Watu wa aina hii wapo kote kote kuanzia kwenye timu hizo mbili yaani Simba na Yanga na pale kwenye Shirikisho la Soka (TFF), tena wamejipanga kweli kweli na cha kushangaza hata vigogo wakubwa wanahusika katika hili.

Ninarudia upinzani wa Simba na Yanga hivi sasa haupo kwenye faida ya soka la Tanzania, bali upo kwa faida ya wachache ambao wameugeuza mchezo huo kama siku ya mavuno kwao kwa michezo yote ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Kama hauamini haya ninayosema, hebu jiulize kwa nini timu hizi ambazo zipo kwa zaidi ya miongo saba sasa, lakini hazina hata viwanja vya kufanyia mazoezi, hazina kitegauchumi cha maana.

Hapo unaweza ukakubaliana nami. Hivi sasa Simba na Yanga ni mitaji ya watu kutoka kimaisha na njia ya kujijenga kisiasa na tena Uchaguzi Mkuu ni mwakani, basi watu hivi sasa utaona wapo karibu sana na hizo timu maana wanajua hiyo ni njia ya kuwapeleka ‘mjengoni’ mjini Dodoma.

Walafi na majangili wa soka wameiharibu ladha ya Simba na Yanga kwa ajili ya manufaa yao na wameifanya mechi hii kuwa mtaji wao na waganga wa kienyeji ambao nao siku ya leo mifuko yao inanona kwa kuwabebesha matunguli wachezaji na watu wa benchi la ufundi wakiwaaminisha kuwa mchezo huo huwezi kushinda bila ndumba.

Tafiti zisizo rasmi zinasema mechi hii ya Simba na Yanga ndio mechi inayoongoza kwa ndumba nyingi kuliko mechi nyingine yoyote ya Ligi Kuu Tanzania Bara na huu ndio ujinga mwingine ambao unaliharibu soka la Tanzania.

Mechi ya Simba na Yanga ni moja ya mechi kubwa sana ya wapinzani wa jadi barani Afrika, ila kwa sasa imepoteza mvuto ingawa watu hawataki kukubali na imefika hapa kwa uzembe wetu hasa kwa kutotaka kuwa wa kweli. Pia inadaiwa mechi hizi za hawa watani wa jadi zinaongoza kwa udanganyifu hasa rushwa inayopenyezwa kwa waamuzi hadi wachezaji wenyewe.

Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi Mtanzania anayesoma China na anapatikana kwa anuani za evancemhando@ gmail.com, +8615180191494.

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya ...

foto
Mwandishi: Mo van der Mhando

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi