loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yanga yaenda Bagamoyo, Simba Kagera

Mabingwa watetezi Yanga, wamefunga safari mpaka Bagamoyo kuweka kambi kwa ajili ya mechi yake ya Jumapili dhidi ya JKT Ruvu ya Pwani kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Yanga ilipoteza hesabu za kutetea taji lake baada ya kufungwa na Mgambo mabao 2-1 mwishoni mwa wiki iliyopita na hivyo ili kujiweka salama katika mbio za taji hilo italazimika kushinda mechi zote nne ilizosaliwa nazo huku ikiomba Azam ipoteze mechi zake.

Yanga imebaki katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 46 nyuma ya Azam yenye pointi 53, nafasi ya tatu iko Mbeya City yenye pointi 45.

Akizungumza na gazeti hili jana Katibu Mkuu wa Yanga Beno Njovu alisema kikosi cha Yanga kilianza kujifua tangu juzi, lengo ni kuhakikisha wanashinda katika michezo iliyobakia.

“Leo (jana) nimewatembelea wachezaji kambini Bagamoyo wote wako vizuri, wana morali naamini baada ya hapo watarudi wakiwa na nguvu ya kufanya vizuri katika mechi zake zote zilizobaki,” alisema Njovu.

Njovu alisema wachezaji wote wako vizuri isipokuwa kwa mshambuliaji wao wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima ndio mgonjwa. Katika michezo 22 iliyocheza Yanga imeshinda michezo 13, sare saba na kupoteza michezo miwili.

Kwa upande wa Simba inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 36, inawania ushindi ili ijiimarishe kwa msimu ujao.

Simba itahuka dimbani keshokutwa kumenyana na Kagera Sugar, mechi inayotarajiwa kuwa ya vuta niku vute itakayochezwa kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Simba Seleman Matola alisema kikosi cha wachezaji 20 wanaondoka asubuhi ya leo kwa basi tayari kwa mchezo huo.

“Wachezaji wote wako vizuri hakuna majeruhi, tunaamini tutafanya vizuri kama ambavyo tumekusudia, sio tu katika mchezo huo tumedhamiria kushinda katika michezo yote,” alisema.

Pamoja na hayo, Matola alisema hawajakata tamaa wana imani watafanya vizuri katika michezo ijayo ili wasizidi kuporomoka.

Alisema kinachohitajika ni wachezaji kuonyesha juhudi uwanjani na kupambana kiume kwa ajili ya kushinda, hatimaye kumaliza Ligi katika mikono salama na kujipanga zaidi kwa msimu ujao.

Katika michezo 23 iliyocheza imeshinda tisa, imepoteza mitano, imetoka sare tisa na imebakiza michezo mitatu dhidi ya Kagera, Ashanti na Yanga.

TIMU ya soka ya Polisi Zanzibar inayoshiriki Ligi Kuu ya ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi