loader
Dstv Habarileo  Mobile
Yesu Kristo anavyofananishwa na mwanakondoo

Yesu Kristo anavyofananishwa na mwanakondoo

Sikukuu ya Krismasi husherehekewa Desemba 25 kila mwaka ambapo watu wa mataifa mbalimbali hufanya ibada zinazoambatana na shamrashamra za kila aina kwa lengo la kumkumbuka Yesu Kristo ambaye hufananishwa na mwanakondoo aliyekuja ulimwenguni kuokoa wale wanaomwamini.

Kondoo ni miongoni mwa wanyama wanaotumiwa na mataifa mbalimbali katika ibada za kijadi na zile za dini zilizoendea sehemu mbalimbali ikiwamo dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislamu.

Katika dini ya Kikristo, Yesu anafananishwa na mwanakondoo pia mchunga kondoo ambaye alitumwa ulimwenguni kuwaokoa binadamu. Katika maandiko mbalimbali ya dini hiyo, Yesu ametajwa kuwa mwana kondoo kutokana na tabia yake ya upendo na jitihada zake za kukusanya watu kutoka sehemu mbalimbali kuishi pamoja na kondoo.

Katika dini ya Kikristo, Yesu anafananishwa na kondoo kwa sababu, alijitolea uhai wake kwa ajili ya kuukomboa ulimwengu kama ilivyoandikwa katika Biblia Takatifu, “Tazama, Mwana- Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” (Yohana 1:29). Katika kitabu hicho hicho, pia katika (Yohana 10:9) Yesu amenukuliwa akisema, “Mimi ndimi mlango wa kondoo; aingiaye kupitia mimi ataokolewa. Ataingia na kutoka na kupata malisho.”

Pia Yesu anafananishwa na mchungaji wa kondoo kwa kuwa Wakristo anapaswa kukaa katika kundi pamoja na kupendana kama ilivyo kwa wanakondoo kama ailivyoandikwa katika (Yohana 10: 11,14) ambapo Yesu anasema, “Mimi ndimi mchungaji mwema; Ninawajua kondoo wangu na kondoo walio wangu wananijua.”

Tabia ya kondoo ndio inayosababisha mnyama huyo kupewa utukufu na kutumika kama alama ya kuwaweka watu pamoja ili waweze kuishi kwa upendo, amani na utulivu. Kondoo ni mnyama ambaye kwa jina la kitaalamu anaitwa Ovis aries. Kondoo anayefugwa ametokana na kondoo mwitu aliyeishi miaka zaidi ya 2000 Kabla ya Kristo.

Kondoo ana manyoya mengi, mwili mkubwa wastani, miguu minne yenye kwato, mkia mnene na macho makubwa kiasi. Ni mnyama anayekula majani lakini pia anaweza kula vyakula vya wanyama wengine vilivyotengenezwa kwa kutumia mbinu za kisasa. Manyoya ya kondoo hutumika katika kutengeneza nguo za sufi zinazotumika hasa katika nchi za baridi kwa kuwa ni kinga nzuri dhidi baridi.

Kondoo jike huwa na kilo kati ya 45 hadi 100 ila dume huwa mkubwa zaidi na huwa na kilo 45 hadi 160. Kondoo ambaye hajakomaa huwa na meno 20 ila aliyekomaa ana meno 32. Wataalamu wanasema ni rahisi kujua umri wa kondoo kwa kuangalia meno yake kwa kuwa meno ya mbele hung’oka na kuota mapya makubwa na yenye nguvu zaidi.

Kondoo hukamilika kuota meno akiwa na umri wa miaka minne. Anapoanza kuzeeka meno hung’ooka na kusababisha kushindwa kula na wengine hufa kutokana na matatizo ya meno. Kondoo ambaye hawapati matatizo ya meno katika umri mkubwa huweza kuishi hadi miaka 32.

Kondoo ana mkia mrefu, mnene, mpana wenye manyoya mengi ukilinganisha na ya wanyama wengine kama mbuzi. Hivi sasa kondoo wanafugwa na binadamu kwa ajili ya nyama, maziwa na sufi, pia kwa ajili ya kufanya matambiko mbalimbali kulingana na mila na desturi za eneo husika.

Inaelezwa kwamba kuna jumla kondoo bilioni moja wanaofugwa duniani, ambapo asilimia 40 wako bara la Asia nchini China, India, Uajemi. Asilimia 20 ya kondoo wako katika bara la Afrika hasa Afrika Kusini na Sudani. Wakati nchi za Australia na New Zealand zina asilimia 15 ya kondoo hao na asilimia tano wanafugwa maeneo ya Uingereza na Amerika.

Chakula cha asili cha kondoo ni nyasi ila pia anaweza kula majani ya miti, magome na nafaka mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mahindi au pumba inayotokana na nafaka mbalimbali. Kondoo hutumia midomo yake kuchagua majani kisha kuyakata kwa meno. Kondoo ana tumbo moja kubwa lililogawanyika katika vyumba vinne; ambapo chumba kimoja hutumika kama ghala la kuhifadhia chakula ambacho hakijalainika vizuri.

Hivyo akisha kula nyasi hucheua na kuanza upya kutafuna nyasi hizo na anapomeza kwa mara ya pili huingia sehemu nyingine ya tumbo lake na kumeng’enyuliwa kwa ajili ya lishe. Kondoo hula chakula kingi anapokuwa malishoni, anaporudi kwenye banda hucheua kisha kutafuna upya na kukiingiza kwenye chumba kingine kinachoruhusu mmeng’eno.

Tumbo lake kubwa huruhusu chakula kumeng’enyuliwa vizuri. Inasemekana kwamba kondoo ni miongoni mwa wanyama wachache wenye uwezo wa kula vitu ambayo haviwezi kumeng’enyuliwa kwenye tumbo la wanyama wengine. Kondoo anabeba mimba kwa siku 152 sawa na miezi mitano. Mtoto anaweza kusimama na kunyonya muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Kondoo asipochinjwa anaweza kuishi kati ya miaka 10 hadi 12. Kondoo dume hupevuja wakiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu hadi miaka miwili na dume hupevuka akiwa na miaka miwili na nusu hadi miaka mitatu. Dume anaweza kupanda majike kati ya 30 hadi 35 katika kundi. Dume kutafuta jike aliyepo kwenye joto na kuanza kumpapasa.

Ikiwa jike atavutiwa na dume huyo husimama ila kama hajavutiwa naye kukimbia. Dume anaweza kumkimbilia na kumshawishi ila asipokubali huondoka na kutafuta jike lingine. Kwa kawaida kondoo hupandana alfajiri au jioni kwani ni nadra kukuta kondoo wakipandana wakati wa mchana. Hata hivyo, kitendo hicho kutegemea hali ya hewa na mazingira.

Kondoo ni wanyama wataratibu wanaopenda kukaa katika makundi. Kondoo hukaa katika makundi ambapo kundi moja linaweza kuwa na kondoo zaidi ya 1,000. Kondoo mmoja akipotea au kujitenga na wengine huchanganyikiwa. Hupita huku na kule akiita kwa nguvu na hawezi kula hadi atakapounganika na wenzake.

Inadaiwa kuwa kondoo ana uwezo wa kuzungusha macho yake na kuona pande zote, hivyo huwezo kuona vitu vilivyopo nyuma yake bila kugeuza kichwa. Uwezo wake wa kuona humuwezesha kujihami dhidi ya maadui. Pia wana uwezo mkubwa wa kunusa na wanapohisi harufu isiyo ya kawaida kukimbia au ili kuepuka kula vitu vyenye sumu.

Kuna uhusiano wa karibu kati ya mbuzi na kondoo kwa kuwa wanyama hao wako katika nasaba ya Caprinae. Utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa kondoo jike anaweza kuzaa anapopandwa na dume la mbuzi. Mchanganyiko huo maalumu huzaa kiumbe anaitwa kondoombuzi. Huitwa hivyo kwa kuwa hufanana zaidi na kondoo hasa kwa tabia ingawa anaweza kuwa na kichwa kama mbuzi.

Kondoombuzi huwa na tabia tofauti hasa anapopata joto. Huwa na harufu kali kuliko mbuzi au kondoo halisi. Wataalamu wanasema nyama yake huwa tamu kuliko ya kondoo au mbuzi wa kawaida.

Kondoo anatumika katika utamaduni mbalimbali na katika dini mbalimbali pia katika imani za dini ikiwa ni pamoja na dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislamu ambapo kondoo ametumika kama sadaka muhimu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. Makala haya yameandaliwa kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya habari.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi