loader
Zanzibar kuondoa sheria zinazokandamiza wanawake

Zanzibar kuondoa sheria zinazokandamiza wanawake

Hatua hiyo ni pamoja na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa mashirika ya kimataifa, wadau na wanaharakati wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary anasema baada ya wadau kujadili na kutoa maoni juu ya Sheria hizo sasa Serikali ya Zanzibar ipo katika katika hatua ya mwisho ya kupelekwa mswada mbele ya Baraza la kutunga sheria la Wawakilishi.

Bakary anasema baadhi ya sheria zinazotumika Zanzibar zinapaswa kufanyiwa marekebisho kwa kuwa ni za muda mrefu na zilizotungwa wakati wa ukoloni wa Muingereza.

Anasema sheria hizo kwa sasa zinahitaji marekebisho kwa kuwa zimepitwa na wakati na kwamba sasa Zanzibar inahitaji sheria zinazoendana na mabadiliko ya mfumo wa maisha ili kujenga jamii yenye usawa.

'Ni kweli tunazo sheria za muda mrefu tulizoachiwa na wakoloni ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho ili ziendane na wakati na kuweza kufanya kazi katika mazingira ya sasa," anasema Bakary.

Mswada wa Sheria ambazo zipo katika hatua ya mwisho tayari kuwasilishwa mbele ya Baraza la Wawakilishi kwa marekebisho na kuwa sheria kamili ni pamoja na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai nambari 7 ya mwaka 2004 na sheria ya ushahidi nambari 5 ya mwaka 1917.

Aidha sheria ya Mahakama ya Kadhi nambari 3 ya mwaka 1985 tayari imepata baraka zote kutoka kwa wadau na kujadiliwa na Baraza la Mapinduzi na sasa inasubiri kuwasilishwa katika vikao vya Baraza la Wawakilishi.

Bakary anasema kuwa Sheria ya ushahidi inayopigiwa kelele na wanaharakati kwa sasa inahitaji marekebisho kwa kuwa imekuwa kikwazo kikubwa na kusababisha kesi nyingi za ubakaji kutupwa katika mahakama baada ya kukosekana kwa ushahidi usiokuwa na shaka.

"Sheria hii tunataka kubainisha upi ushahidi usiokuwa na shaka kwa sababu matukio ya ubakaji yanafanyika katika mazingira ya usiri mkubwa kwa hivyo hapa tunataka kuboresha zaidi aina ya ushahidi utakaokubalika Mahakamani," Bakary anaeleza.

Mwaka 1985 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliunda Tume ya kurekebisha sheria na kuipatia jukumu ya kupitia sheria zote zinazoonekana zimepitwa na wakati na zile zinadhoofisha haki za wananchi.

Kisha kuziwasilisha Serikali Kuu. Mwenyekiti wa Tume ya kurekebisha sheria ya Zanzibar, Jaji Bakari Mshibe, anasema tayari wamegunduwa sheria nne zinahitaji marekebisho makubwa ili kwenda na wakati na kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia katika jamii.

Akitoa mfano, Mshibe anasema sheria ya Mahakama ya Kadhi nambari 3 ya mwaka 1985 ipo katika mchakato wa hatua za mwisho kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kuona Mahakama hiyo inasimamia vizuri majukumu yake.

Marekebisho makubwa katika sheria hiyo ni pamoja na kuiboresha Mahakama hiyo kuwa na uwezo zaidi katika kusimamia mwenendo wa uendeshaji wa kesi na sifa kwa Mahakimu wake.

Mshibe anafahamika kuwa sheria mpya sasa inasema Mahakimu na Majaji watakaoendesha Mahakama ya Kadhi wanapaswa kuwa na kiwango cha elimu kuanzia shahada ya kwanza katika vyuo vikuu vinavyotambuliwa nchini.

Aidha alisema suala la mgawanyo wa mali kwa wanandoa wakati inapovunjika nalo limezungumzwa kwa upana mkubwa kwani ni moja ya sehemu ya malalamiko ya wanaharakati wanaopinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

"Eneo la mgawanyo wa mali kwa wanandoa bado limekuwa na utata kwa sababu Mahakama za kadhi zinafuata sheria za Kiislamu ambazo zimetaja bayana mgawanyo wa mali kwa wanandoa kwa hivyo sisi suala hilo tumeliacha kama lilivyo, Jaji Mshibe anafahamisha.

Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) ni miongoni mwa wadau wanaliochangia kwa kiazi kikubwa kuchambua sheria kandamizi dhidi ya wanawake na madhara yake kwa jamii.

Mkurugenzi Mkuu wa Zafela, Jamila Mahmoud alizitaja baadhi ya sheria zinazohitaji marekebisho haraka ili kupambana na kutokomeza vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ni pamoja na sheria ya Mahakama ya Kadhi namba 3 ya mwaka 1985 ambayo hadi sasa imekwama, licha ya Serikali kuahidi kuiwasilisha mbele ya Baraza la Wawakilishi.

Akifafanua Jamila anasema sheria ya Kadhi iliopo sasa haikidhi mahitaji ya kuyapatia ufumbuzi masuala ya ndoa zaidi katika suala la mgawanyo wa mali kwa wanandoa wakati inapovunjika pamoja na mwenendo mzima wa kuendesha kesi hizo mahakamani.

Sheria hiyo imetoa mamlaka kwa baadhi ya mambo machache tu kushughulikiwa na mahakama hiyo ikiwemo ndoa, talaka pamoja na ulezi wa mtoto na utunzaji wake tu.

“Zafela imegunduwa kwamba sheria ya Mahakama ya Kadhi bado inahitaji marekebisho makubwa ambapo suala la mgawanyo wa mali lishughulikiwe na mahakama hiyo moja kwa moja kwa sababu linatokana na ndoa,” alisema.

Anasema wanawake wanapata matatizo makubwa wakati ndoa inapovunjika kwa kuwa wanakosa mgawo wa mali huku wakiachiwa kazi mkubwa ya kulea watoto jambo linalosababisha ongezeko la kwa watoto wa mitaani na wanaojiingiza katika ajira mbaya kutokana na ukosefu wa malezi bora.

Sheria nyingine zilizofanyiwa kazi na Zafela na kubainika zinahitaji marekebisho makubwa ni sheria ya ajira ya mwaka 2005 ambayo inakataza udhalilishaji wa kingono, lakini haikutoa adhabu kwa atakayefanya kosa hilo.

Zafela ilianzishwa mwaka 2003 na kupata usajili kamili mwaka 2005 kwa ajili ya kusaidia na kutoa huduma za kisheria kwa makundi ya wanawake na watoto kwa lengo la kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Tangu kuanzishwa kwake Zafela imekuwa mkombozi kwa jamii ya wanawake na watoto kuweza kupata haki zao za msingi za kisheria na hivyo kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia katika jamii.

Kufuatia utekelezaji wa mradi wa usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake (GEWE) unaotekelezwa kwa pamoja na chama cha waandishi wa habari wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na Serikali ya Denmark, wamezifanyia uchambuzi wa kina baadhi ya sheria kandamizi na zinazotoa mwanya wa kuchangia ongezeko la vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia nchini.

Wanaharakati wa mradi wa kupambana na udhalilishaji wa kijinsia (GEWE) wanataka kesi za ubakaji zitolewe hukumu yake haraka na kuondowa vikwazo vinavyoshelewesha ushahidi.

Sheha (diwani) wa Makunduchi Tasani, Mwanabaraka Chimbeni Kheir ambaye ni mwanaharakati wa mradi wa mradi wa kupambana na udhalilishaji wa kijinsia anasema wananchi wameanza kukata tamaa kutokana na mahakama kushindwa kuzipatia ufumbuzi haraka kesi za ubakaji.

“Tunazitaka mahakama zetu kuharakisha kutoa hukumu kwa kesi za ubakaji ambazo zinachukuwa zaidi ya miaka mitano bila ya hukumu kwa kisingizio kwamba ushahidi haujakamilika,“ anasema Mwanabaraka.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mwanaidi Saleh, anasema Sheria zinazohusiana na masuala ya jinsia zipo katika mchakato wa kufanyiwa marekebisho ili kujenga mazingira ya kuwa na jamii yenye usawa kati ya mwanaume na mwanamke.

Anasema baadhi ya sheria zimekuwa kikwazo kwa maendeleo ya elimu kwa mtoto wa kike kwa kuwa zinatoa mwanya mkubwa kwa wazazi kuwaachisha shule na kuwaozesha watoto wao wa kike kwa kuwa sheria inataja kiasi kidogo cha fidia kwa wazazi wanapatikana na kosa la kumuozesha mtoto kabla ya kuhitimu masomo.

“Tupo katika mchakato wa kuifanyia marekebisho makubwa Sheria ya Elimu ya mwaka 1982 baada ya kubaini mapungufu mengi katika sheria hiyo, ikiwamo adhabu ndogo kwa mzazi atakayeozesha mtoto wake,“ alisema Mwanaidi.

Kwa mfano, alisema adhabu ya kwanza mzazi akimuozesha mtoto wake atalazimika kulipa faini ya Sh 1,500 au Sh 3,000 fedha ambayo ni kidogo sana ikilinganishwa na gharama halisi za maisha na kubwa zaidi kulinganisha na madhara ya kumuozesha binti mdogo.

Mrajisi wa Elimu Zanzibar, Siajabu Suleiman Pandu, anasema baadhi ya marekebisho ya sheria ya Elimu nambari 6 ya mwaka 1985 yanayotazamiwa kufanywa ni pamoja na kuweka adhabu kali ili kuwabana wazazi wenye tabia ya kuwaozesha watoto kabla hawajamaliza masomo.

Hata hivyo Pandu anasema adhabu pekee haitoshi bali jambo muhimu ni kutoa elimu na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.

"Sheria ya Elimu iliyopo sasa haijawabana wazazi na kuwataka kuacha kuwaozesha watoto wao wakati wakiwa katika masomo hasa elimu ya msingi ambayo ni ya lazima, Pangu anaeleza.

Mwenyekiti wa jumuiya ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanawake (UWAWAZA), Mgeni Hasssan Juma anasema zaidi ya kesi 170 zinazohusu udhalilishaji wa kijinsia zimeripotiwa katika Mahakama zote za Unguja na Pemba katika mwaka 2003, lakini ni kesi tatu tu ndiyo watuhumiwa walitiwa hatiani.

“Mwenendo wa kesi hauridhishi hasa katika suala la ushahidi na tunaitaka Wizara ya Katiba na Sheria kufanya marekebisho katika sheria ambazo zinatoa mwanya kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwamo ubakaji,” alisema Mgeni.

Mgeni amewasilisha hoja binafsi mbele ya Baraza la Wawakilishi ya kutaka ukatili wa kijinsia kushughulikiwa kikamilifu na vyombo vya sheria.

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi