loader
Dstv Habarileo  Mobile
Zanzibar mguu sawa michezo na utalii

Zanzibar mguu sawa michezo na utalii

Mchezo huo maalumu unaojulikana Nani Kama Mtani Jembe tayari umevuta hisia kubwa za wadau wa soka na wanazi wa klabu hizo kubwa na zenye wafuasi wengi hapa nchini. Kwa ufupi soka ni moja ya michezo inayopendwa na kufuatiliwa zaidi duniani. Kwa takwimu zangu binafsi inawezekana, kandanda ni kitu cha pili kuwa na wafuasi wengi zaidi baada ya Facebook.

Kwa hiyo mabalozi wa mchezo huo, au wanasoka kama tunavyowaelewa, hawaangaliwi kwa mengine mengi zaidi ya umahiri wao uwanjani. Miaka nenda miaka rudi mechi kati ya Simba na Yanga zimekuwa za kuvuta watu wengi, hisia na wakati mwingine husababisha hata majeruhi na vifo, mashabiki wa timu moja wakikataa kuburuzwa na nyingine au wakiona bora wajitoe uhai kuliko kushuhudia wakifungwa.

Si kwa Tanzania tu bali nchi mbalimbali duniani kuna upinzani wa jadi na kuna timu zenye uhasama baina mkubwa. Mfano jijini Manchester, jiji la pili kwa ukubwa nchini Uingereza, kuna ushabiki wa kufa mtu, utani wa jadi kati ya Manchester City na Manchester United uliofikia hatua ya uadui na hata kuitana majirani wabaya.

Inawezekana Tanzania tukawa na tofauti kidogo katika ushabiki kwa sababu Simba na Yanga zimeenea maeneo mbalimbali nchini kwamba mtu ama awe Simba au awe Yanga. Inadaiwa ni nadra sana kuwa nje ya machaguo hayo mawili. Lakini ipo orodha ya klabu zilizo na upinzani wa jadi ambazo zipo katika jiji moja.

Tuachane na Ulaya, tuangalie za hapa Afrika japo kwa uchache, mfano Misri katika jiji la Cairo kuna klabu pinzani mbili Al-Ahly na Zamalek. Kinachovutia zaidi kwenye mchezo unaozikutanisha klabu hizi ni kwamba, mwamuzi huwa anatoka nje ya Misri ili kuweza kuchezesha mechi kwa haki, kwa sababu hawaaminiani.

Nchini Afrika Kusini, klabu pinzani za jadi ni Kaizer Chiefs na Orlando Pirates. Hizi ni klabu za Jiji moja la Johannesburg na pia zinatoka katika kitongoji kimoja cha Soweto chenye wakazi wengi zaidi wa maisha ya kawaida. Mchezo unaozikutanisha timu hizi, huwa ndiyo wenye mahudhurio makubwa zaidi nchini Afrika Kusini na mara nyingi huchezewa kwenye uwanja wa FNB ambao una uwezo wa kuchukua watazamaji 90,000.

Nchini Tunisia katika jiji la Tunis, timu pinzani ni Club Africain na ES Tunis. Mara zote mchezo baina ya timu hizi hupigwa mjini Rades katika uwanja wa 7 Novembre ambao una uwezo wa kuchukua watazamaji 65,000. Hii ni mada inayohitaji nafasi kuzungumzia upinzani wa timu mbalimbali.

Dhamira yangu si kutaka kujadili kuhusu mechi ya Simba na Yanga leo, au upinzani wa timu mbalimbali Afrika na kwingineko, bali nilitaka kuwaweka sawa wasomaji wangu ili twende pamoja wajue jinsi gani kwenye michezo kulivyo na nguvu. Pengine kwa kutambua nguvu iliyopo kwenye soka na michezo mingine hapa nchini, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeandaa mpango kabambe mwaka 2014 wa kukuza sekta ya utalii kwa kutumia michezo.

Ofisa Mipango wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk Miraji Ukuti Ussi anasema wanaamini kwa njia ya michezo wanaweza kuitumia kwa kiasi kikubwa kuitangaza nchi, ikiwa ni hatua mojawapo ya kuhamasisha utalii na hilo watalifanya kwa kutoa kalenda maalumu ya matukio ya michezo kwa mwaka mzima.

“Zamani tulikuwa na mashindano ya mpira wa miguu kwa kualika timu mbalimbali za ndani na nje zinacheza na hiyo inakuwa hatua mojawapo ya kuitangaza nchi. “Tumefikiria hilo tulifanye na pengine kuboresha zaidi na ndiyo tupo katika mchakato, naamini mwakani mambo yatakuwa mazuri mkakati huo utakapokamilika. “Pia katika kuimarisha masuala ya utalii licha ya kuhusisha vyama vya michezo husika pia tutashirikiana na waandaaji wa matamasha mbalimbali kama vile Sauti za Busara na yale ya Nchi za Jahazi kuona namna yatakavyoweza kusaidia kuhamasisha utalii wa Zanzibar,” anasema Dk Ussi.

Anasema anaamini wakishirikiana na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kile cha netiboli (Chaneza), mpira wa wavu (Zava) na vyama vingine vya michezo ikiwemo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), vikitumiwa ipasavyo vinaweza kusaidia kuitangaza nchi na hivyo kuwa kichocheo cha watalii kufika na kujionea mambo mbalimbali ya Zanzibar.

Dk Ussi anasema hivi sasa mchango wa sekta ya utalii kwa Pato la Taifa (GDP) Zanzibar umefikia asilimia 27 na unachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni. “Kwa hiyo utaona jinsi gani utalii ulivyo muhimu kama tutautumia ipasavyo na hiyo ndiyo dhamira yetu kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Anasema utalii ni sekta muhimu sana kwani nchi zote duniani zinajihusisha kwa njia moja au nyingine na biashara hiyo ambayo hufanywa kwa malengo mbalimbali yakiwemo ya kujifurahisha kwa kutembelea mandhari za kuvutia. Anasema kwa upande wa Zanzibar malengo ya kuendeleza sekta ya utalii yamekuwa yakibadilika kwa awamu na historia inaonesha kabla ya mapinduzi sekta hiyo ililenga zaidi kujenga uhusiano na urafiki.

“Zanzibar imejaaliwa kuwa na hali ya hewa mwanana, mandhari na fukwe nzuri pamoja na tamaduni ambazo si aghlabu kuzikuta katika eneo lolote jingine katika maeneo ya mwambao na nchi zilizomo katika bahari ya hindi,” anasema Dk Ussi.

Kamishina huyo anasema sekta hiyo sasa imetoa mchango wa ajira ya moja kwa moja kwa vijana 13,017 na zaidi ya ajira 45,000 kwa zile nafasi zisizo na uhusiano wa moja kwa moja na kwamba matarajio ni kuwa zaidi ya asilimia 50 ya waajiriwa Zanzibar watatokana na sekta ya utalii ifikapo mwaka 2020.

Anasema serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dk Ali Mohammed Shein inatilia mkazo sana mambo ya utalii, hivyo wanaamini watapiga hatua kubwa kwa jambo hilo. “Rais pia ni mpenzi wa michezo, tunaamini mkakati wetu wa kutangaza vivutio vya utalii kwa njia ya michezo utapata matokeo mazuri na ile dhamira yetu ya kuitangaza Zanzibar itatimia,” anasema.

Anasema dira ya mwaka 2020 na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupungunza Umaskini Zanzibar (Mkuza) kwa pamoja vinalenga kufikia ukuaji wa uchumi utakaowajali wananchi na zaidi masikini. Kwa upande wake Meneja wa Hifadhi ya Msitu wa Jozani, Ally Ally anasema kuna vitu vingi ambavyo watalii wanaweza kwenda kuviona Zanzibar ikiwemo kima wekundu ambao hawapatikani sehemu yoyote duniani.

Naye Fakhi Suleimani Juma, ambaye ni muongoza watalii anaipongeza serikali kwa juhudi hizo za kutaka kutangaza vivutio vya utalii kwa njia ya michezo.

“Michezo ina nguvu sana, tukiitumia vizuri tutafanikiwa,” anasema na kutolea mfano kuwa hata mwaka jana wakati wa michezo ya Olimpiki iliyofanyika London, Uingereza kulikuwa na fursa nzuri ya kutangaza vivutio vilivyopo Zanzibar. “Nilikuwepo London, Uingereza waliandaa kitu kilichoitwa Kijiji cha Afrika, eneo walimotaka timu zote kutoka Afrika na kukaa kama ndugu. “Ni hapa sasa wapenda nyama choma, kongoro, mishikaki na labda hata supu ya ngozi za ng’ombe na mbuzi vilipatikana. Vyakula ya aina zote vya Kiafrika vilipatikana. Ilikuwa sehemu nzuri nasi kujitangaza, lakini kilichowakutanisha ni michezo,” anasema.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Amir Mhando

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi