loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Zonga: Ushindi siri ya udhamini

Wengine wamekuwa wakisema sababu kubwa ya kufanya vibaya kwenye mashindano ni kikosa kuungwa mkono na wadau na hujitegemea wenyewe kwa nauli, posho za wachezaji na mahitaji mengine. Aidha, timu nyingine hushindwa kabisa kushiriki kwa sababu ya kukosa fedha za kuwatoa sehemu moja kwenda nyingine.

Pengine, kuna sababu nyingi zinazochangia kuhangaika bila mafanikio. Lakini Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Salehe Zonga anasema dawa ya wadhamini kujileta wenyewe, ni klabu husika kufanya vizuri kuanzia kwenye timu anazozisimamia, na uongozi kufanya kazi kwa juhudi.

Anasema jambo aliloligundua ni kwamba vyama vingi vya michezo havipati ufadhili wa mashindano kutokana na mfumo uliopo. Kwanza vingi vina migogoro isiyokwisha. Kwa klabu inayoongozwa na migogoro kamwe hakiwezi kufanikiwa wala kupata baraka kutoka kwa wadau. Siku zote wadhamini hupenda kitu kizuri ili na wao bidhaa zao ziweze kuuzika.

Zonga ambaye amekuwa akiongoza mpira wa kikapu kwa miaka mingi, ana uzoefu mkubwa na masuala hayo. Anasema siri kubwa ni chama au timu kuhakikisha inafanya vizuri kabla ya kujitokeza kuomba udhamini.

Anasema kuanzia mwaka 2005 kurudi nyuma ambako alikuwa ni kiongozi wakati huo kabla ya kurudi tena mwaka jana, mchezo wa kikapu ulikuwa na hamasa kubwa ya kuwavutia wafadhili tofauti na hapo katikati yaani kuanzia mwaka 2006 ambako udhamini ulishuka.

“Zamani kulikuwa na hamasa na wadau kuunga mkono, baadaye mgogoro ulijitokeza. Kwa mfano, TBF kuliwahi kutokea mgogoro mdogo wa baadhi ya viongozi kutokuelewana, na vyama vingine pia, lakini hiyo haiwezi kujenga zaidi ni kubomoa, kwa hiyo tunahitaji kubadilika na kujifunza,” anasema Zonga.

TBF kwa sasa wanaandaa mashindano ya kikapu na kushirikisha klabu zaidi ya 30 yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam. Zonga anasema hawajapata wadau wa kuwaunga mkono, lakini anataka kurudisha imani kwa wadau kwa kuhakikisha timu zilizopo zinafanya vizuri ili kuwavutia wadau na wakati mwingine watakapoomba ufadhili kuwa rahisi kupata.

“Sina wasiwasi na suala la wadhamini, kwanza tujitahidi tufanye vizuri na kutangaza mchezo wetu kwa kuwaalika wadau mbambali kuja kututembelea wakati mashindano yanaendelea, wakiona tunafanya vizuri watakuja tu,” anasema mwanamichezo huyo mkongwe.

Anasema wamejipanga kwa nguvu zao hivyo wataendesha kama walivyopanga na kuhakikisha washindi wanapata zawadi za vikombe ili kuwapa hamasa wakati mwingine waweze kujitokeza.

Mashindano hayo yatafanyika kuanzia leo Jumamosi na baadhi ya timu ambazo zitashiriki kwenye mashindano hayo ni Bandari, Kings United za Tanga, timu kutoka Lindi, Mtwara, Shinyanga, Morogoro, Dodoma, Dar es Salaam na baadhi ya mikoa mingine inaendelea kuthibitisha.

Matarajio makubwa ya TBF katika kuzialika timu nyingi za mikoani ni kuibua vipaji vipya ambavyo vitaendelezwa na kuonekana kwenye timu za Taifa. Anasema ana imani kubwa siku moja mchezo huo utawavutia mashabiki wengi na kwenda kuangalia kama ilivyo katika mchezo wa soka, hivyo, wadau watajitokeza kwa kujiamini kwamba wakishirikiana bidhaa zao zitahuzika.

Malengo makubwa ya TBF katika kuendeleza mchezo huo nchini kwanza ni kuunda timu za vijana kuanzia umri chini ya miaka 12 hadi 20 na kushiriki kwenye michuano ya Afrika Mashariki na ikiwezekana hata Afrika. Hiyo ni njia ya kuwatafutia vijana ajira kwani watakapoonekana wakicheza kwa juhudi katika nchi mbalimbali, kuna uwezekano wa kupata nafasi katika nchi zinazothamini michezo hiyo kama Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Afrika.

Kwa kuanzia, tayari wamepata mwaliko wa ushiriki kwenye mashindano ya Kanda ya Vijana chini ya umri wa miaka 18 yatakayofanyika nchini Uganda kuanzia Aprili 18, mwaka huu. Kupitia mashindano ya klabu bingwa watachagua wachezaji watakaounda kikosi kwa ajili ya michuano hiyo, lakini ushiriki wao utategemea kama watapata ufadhili kwa vile huhitajika kujilipia kwa kila kitu.

“Ni gharama kubwa kusafirisha timu, kwa kila kichwa kimoja ni dola za Marekani 40 (Sh 64,000) kwa mchezaji, wakati kiongozi mmoja ni dola 60, hivyo, tunahitaji kujipanga,” anasema Zonga. Anasema watajitahidi wawezavyo kuhakikisha kunakuwa na mwakilishi wa Tanzania kwenye michuano hiyo kwani ndio sifa mojawapo ya kutangaza mchezo huo na ikiwa watafanya vizuri wataijengea sifa kubwa Tanzania.

Aidha, sio kwa wanaume peke yao ambao hupewa nafasi hiyo, zipo timu za wanawake wanaopenda mchezo huo ambao pia watashiriki kwenye mashindano hayo ya Klabu Bingwa. Anasema atahakikisha katika michuano hiyo klabu za wanawake zinashiriki kikamilifu ili kuonesha vipaji vyao.

Wakati anazungumzia mikakati ya kuboresha mchezo huo na kurudisha hamasa kwa mashabiki, anasema suala lingine atakalotilia mkazo ni viwanja kwa ajili ya mchezo huo. “Kuna upungufu wa viwanja kwa ajili ya mchezo wetu, lakini tuko kwenye mkakati ili tuchangishe fedha, lengo letu liweze kutimia, siku siyo nyingi tutatangaza,” anaeleza mtendaji huyo wa TBF.

Yote yanawezekana kama yanayosemwa yatafanyiwa kazi kwa vitendo. Lakini pia vyama vizingatie ushauri wa Zonga kwa kujitahidi kufanya vizuri, kuwaalika wadau kwenye michuano, kuepukana migogoro isiyokuwa na tija, ndipo mafanikio yatakapoonekana.

Jambo lingine ni ushirikiano wa viongozi katika kuendeleza mchezo wenyewe, unaweza ukasaidia kuleta matunda kwa wakati ujao, ikiwa wanapishana kwa kauli na vitisho hakika mchezo utarudi nyuma. Tujifunze kwa maendeleo.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi