HakiElimu watoa mapendekezo 6
WAKATI bajeti ya Wizara ya Elimu imepangwa kusomwa wiki ijayo, Shirika la HakiElimu limetoa mapendekezo sita yakupewa kipaumbele katika bajeti ijayo ili kuboresha sekta ya elimu nchini.
Mkurugenzi wa HakiElimu, Dk John Kalage akizungumza leo Mei 9,2023 jijini Dar es Salaam, amesema wanatambua juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu katika vipindi viwili vilivyopita, kiwango cha bajeti kuongezeka.
Pia wanatambua wigo uliotanuliwa na serikali katika utoaji wa elimu bila ada kwa kidato cha tano na cha sita, hivyo takribani Sh bilioni 10.
3 zinapaswa kutengwa kila mwaka kama fidia ya ada kwa wanafunzi wa vidato hivyo.
Pia kidato cha kwanza hadi cha nne bajeti imeongezeka kutoka Sh bilioni 364.2 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh bilioni 390 kwa mwaka 2022/2023 huku bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ikiongezeka kwa asilimia 14.7 kutoka Sh bilioni 570 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh billioni 654 kwa mwaka 2022/2023.
“Fedha za kujikimu kwa mwanafunzi elimu ya juu imeongezeka pia kutoka sh 8500 hadi sh 10,000, tunaipongeza serikali kwa uwekezaji huu kwenye sekta ya elimu,” amesema Dk Kalage na kuongeza:
“Hata hivyo, tunapendekeza upangaji wa bajeti, katika sekta ya elimu iongezwe kwa kuwa kiwango ambacho serikali imekuwa ikitenga hakiwiani na viwango vinavyopendekezwa kimataifa juu ya upangaji wa bajeti ya sekta ya elimu.
“Azimio la Incheon la mwaka 2015 ambalo serikali iliridhia, linazitaka nchi zilizo ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kutenga walau asilimia 20 ya bajeti kuu ya serikali katika sekta ya elimu, lakini serikali imekuwa ikitenga asilimia 14 pekee.
“Iwapo ingetenga asilimia 20 ni wazi ingeweza kutatua changamoto kubwa katika sekta ya elimu,” amesema Kalage
Pili wamependekeza serikali ipange bajeti ya mpango wa tatu wa maendeleo ya elimu (ESDP111) wa mwaka 2021/2022-2025/26 na kwamba tangu kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo serikali haijaweza kutenga bajeti inayoainishwa katika mpango huo.
“Ni rai yetu kwa serikali na wabunge kupanga baejti ya sekta ya elimu inayoendana na Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Elimu,” amesema.
Aidha wamependekeza pia kuboresha miundombinu ya shule kwa kujenga madarasa angalau 25,000 kwa mwaka, ambapo shule ya msingi madarasa 20,000 na sekondari madarasa 5,000, ili kuweza kutatua tatizo la upungufu wa madarasa ndani ya miaka mitano.
“Ikiwa ujenzi wa darasa moja linagharimu Sh milioni 15 basi katika mwaka wa fedha 2023/24 serikali itahitaji kutenga Sh bilioni 375 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 20,00 ya shule ya msingi tu,” amesema.
Mapendekezo mengine waliotoa ni kuboresha ruzuku kwa mwanafunzi hadi kufikia sh 25,000 kwa shule za msingi kwa mwanafunzi na sh 50,000 kwa shule za sekondari.
“Serikali pia ipitie upya mwongozo wa utoaji ruzuku ili kuruhusu matumizi ya fedha za ruzuku katika kutoa huduma za chakula shuleni pamoja na ununuzi wa sodo kwa watoto wa kike wanaohitaji kujihifadhi nyakati za hedhi,” amesema.
Mapendekezo mengine ni kuweka mpango wa muda mrefu kwa miaka mitano mfululizo, kuajiri walimu angalau 40,000 kwa mwaka ambapo msingi walimu 25,000 na sekondari 15,000.
Amesema mpango huo utamaliza kabisa tatizo la uhaba wa walimu wa shule za msingi na sekondari kwa miaka mitano ijayo.
“Ni mapendekezo yetu serikali iongeze idadi ya walimu wanaoajiriwa hadi kufikia 40,000 kwa mwaka wa fedha 2023/24,” amesema Dk Kalage