SHIRIKA la HakiElimu limetoa mapendekezo tisa, ili kumaliza tatizo la ukatili shuleni ikiwemo mapitio ya Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978.
Pia mapitio ya mwongozo wa elimu juu ya adhabu ya viboko ya mwaka 2002, sheria ya mtoto ya mwaka 2009 vipitiwe upya, ili kukataza kabisa matumizi ya viboko shuleni na kuzuia adhabu nyingine ambazo zinaweza kutoa mwanya wa ukatili kwa watoto.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Januari 26,2023, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, John Kalage amesema serikali iweke mipango endelevu ya kuimarisha mifumo rasmi ya ulinzi na usalama wa watoto shuleni, ikiwa ni pamoja na kuimarisha madawati ya ulinzi na usalama wa watoto shuleni pamoja na mabaraza ya watoto.
” Serikali ichukue hatua kali kwa wote watakaobainika kuhusika na vitengo vya ukatili dhidi ya watoto ili kukomesha vitendo hivyo ndani na nje ya shule,” amesema.
Mapendekezo hayo ya HakiElimu yamekuja ikiwa sambamba na kulaani kitendo cha Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kakanja mkoani Kagera, ambaye katika kipande kifupi cha video anaonekana akiwacharaza bakora wanafunzi wawili kwenye nyayo za miguu huku wakiwa wamevua viatu.
Amesema kitendo hicho kinakiuka sio tu haki za watoto, bali pia ni kinyume na maadili ya kazi ya ualimu na malezi bora ya wanafunzi.
Hata hivyo Kalage ameipongeza serikali kwa kuchukua hatua za awali kwa haraka dhidi ya mwalimu aliyetenda tukio hilo, ikiwemo kumvua nafasi yake ya ualimu mkuu, kumsimamisha kazi na kuunda tume ya kuchunguza tukio hilo ili hatua za kisheria ziweze kufuatwa.
Amesema utafiti uliofanywa na HakiElimu mwaka 2020 unaonesha kuwa asilimia 87.9 ya watoto wa shule waliripotiwa kufanyiwa ukatili wa kimwili, huku asilimia 90 ya ukatili huo ulitokana na viboko shuleni.
“Katika utafiti huu asilimia 54.9 ya watoto walisema walimu wao na walezi wanatumia kupiga ngumi na makofi kama sehemu ya adhabu, ” amesema Kalage.
Amesema programu iliyotangazwa hivi karibuni na serikali ya uanzishwaji wa shule salama 600 nchi nzima, ambayo inalenga kuondoa ukatili wa namna yoyote kwa watoto na kuzifanya shule kuwa mahali salama na rafiki ilenge kwa shule zote 18,000 zikiwemo za msingi 12,000 na sekondari 5,000.
“Kama kuna ufinyu wa bajeti serikali ishirikishe wadau sekta binafsi, asasi za kiraia ili programu hii iwe kwa shule zote isiwe kwa shule 600 tu, wote tunakerwa na ukatili wanaofanyiwa watoto, ” amesema Kalage.
Amesema mapendekezo yao ni kuwa mpango huo uingizwe katika muongozo na kanuni za uendeshaji shule, ili utekelezwe katika shule zote.