‘Hakikisheni mnatatua migogoro ya ardhi’

‘Hakikisheni mnatatua migogoro ya ardhi’

MKUU wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba, amewataka wakuu wa wilaya mkoani humo kuhakikisha wanatatua na kumaliza migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao, huku akiwaasa kutumia vyema sheria ya kuwaweka rumande  saa 48 wananchi waliofanya makosa.

Hayo ameyasema leo kwenye kikao kazi na wakuu wa wilaya wote ambao wameteuliwa kuja kwenye wilaya zilizopo mkoani humo.

Amesema mkoa huo una changamoto kadhaa zikiwemo za migogoro ya ardhi, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanaenda kuipatia ufumbuzi, ili wananchi waweze kuishi kwa amani na utulivu.

Advertisement

“Niwatake mkasimamie migogoro ya ardhi kapangeni namna ya kuitatua kila wiki na kila mwezi muwasilishe taarifa kwangu jinsi mlivyoishughulikia, “amesema RC Mgumba.

Amewataka wakuu hao wa wilaya kwenda kusimamia miradi ya maendeleo sambamba na udhibiti wa makusanyo ya ndani kwenye halmashauri zao.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema kuwa ataenda kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa kwenye wilaya yake inakamilika kwa wakati na kuzingatia thamani ya fedha.