Bahati huwapenda wenye ujasiri. Muulize Achraf Hakimi atakupa majibu.
UTAMBULISHO WAKE
Achraf Hakimi mwenye miaka 24 alizaliwa November 8,1998 katika jiji la Madrid nchini Hispania..
Achraf Hakimi (24) ameoa Mwigizaji wa Kihispania, Hiba Abouk (36). Walianza kuchumbiana Julai, 2018. Hiba Abouk ana asili ya Libya na Tunisia. Wana watoto wawili; wa kwanza alizaliwa 2020 na wa pili 2022.
UTAMBULISHO WA MKE WAKE
Hiba Abouk ni nani?
Jina lake kamili ni Hiba Aboukhris Benslimane. Alizaliwa Oktoba 30,1986 huko Madrid, Uhispania. Yeye ndiye mdogo kati ya ndugu zake wanne. Wazazi wake walihama kutoka Tunisia na kuishi Uhispania.
Alisoma ‘French Lycée’ huko Madrid hadi umri wa miaka 18. Baadaye alisoma falsafa ya Kiarabu na akapata shahada ya leseni ya mchezo wa kuigiza kutoka The Real Escuela Superior de Arte Dramatico ni shule ya maigizo huko Madrid, Uhispania. Pamoja na Kihispania na Kiarabu, anazungumza Kifaransa, Kiingereza na Kiitaliano.
SAFARI YA SOKA
Maisha yake ya soka yalianza akiwa na umri wa miaka saba ambapo alijiunga na timu ya soka ya Getafe iitwayo Colonia Ofigevi. Kutoka Colonia Ofigevi, alijiunga na timu ya vijana ya Real Madrid akiwa na umri wa miaka minane.
Alijiunga na Real Madrid Castila mwaka 2016 na alijumuishwa katika kikosi cha kwanza cha Madrid mwaka 2017, kutokana na ugumu wa nafasi ya kucheza, alitolewa kwa mkopo katika klabu ya Borrusia Dortmund.
Klabu ya Serie A Inter Milan ilimsaini Hakimi kwa mkataba wa miaka mitano tarehe 2 Julai 2020 kwa Euro milioni 40. Baada ya msimu mmoja akiwa na Inter Milan, PSG ilimsajili kwa mkataba wa miaka mitano kwa ada ya awali ya uhamisho ya Euro milioni 60, ambayo huenda ikapanda kwa euro milioni 11 katika nyongeza.
UGUMU WA MAISHA
Baba yake Hakimi alikuwa mfanyabiashara wa mataani, tena wakati mwingine ni wale wafanyabishara ambao hawatakiwi, ugumu wa maisha ulimfanya Hakimi kuingia kwenye soka akiamini atakamilisha ndoto zake na kuwasaindia ndugu zake na mama yake alikuwa mfanyausafi.
Moja ya mahojiano Hakimi aliwahi kusema “Mama yangu alikuwa mwanamke wa kufanya usafi tu na baba yangu alikuwa mitaani,” alisema kwenye kipindi cha TV cha Uhispania, El Chiringuito. Anaseme “Ndugu zangu walitoa maisha yao kwa ajili yangu. Walichukua vitu vingi kutoka kwa ndugu zangu ili nifanikiwe. Leo nacheza kwa ajili yao.”
HAKIMI AKIWA MOROCCO
Hakimi aliiwakilisha Morocco katika mashindano ya U-17, U-20 na U-23. Alikuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji 26 kwa Kombe la Dunia la Urusi 2018. Pia aliitwa kwa ajili ya Kombe la Mataifa ya Afrika la Cameroon 2021. Ni sehemu ya kikosi cha wachezaji 26 kwenye Kombe la Dunia la FIFA la 2022 Qatar.
Awali Hakimi alitakiwa kucheza Morocco kama anavyosema ““Utamaduni wangu ni wa Morocco. Nyumbani, sikulazimika kufikiria sana jambo hilo,” alisema katika mahojiano na jarida la L’Equipe. “Nilikuwa nikitazama mechi za Morocco na baba yangu ambaye aliniambia kila mara kuhusu wachezaji mashuhuri wa zamani.”
Mnamo mwaka wa 2017, akiwa tayari kuingia kwenye timu ya wakubwa, Real Madrid walikuwa katikati ya mbio za kihistoria za UEFA Champions League ambazo zingewafanya kushinda mataji matatu mfululizo.
Chini ya ukufunzi wa Zinedine Zidane, alicheza mechi tisa za La Liga na kufunga mabao mawili, na hiyo ilimtosha kupata timu ya taifa kwenye Kombe la Dunia la 2018. Mashindano hayo nchini Urusi yalikuwa ya kukatisha tamaa kwa Hakimi.
TURUDI QATAR
Baada ya Morocco na Uhispania kwenda dakika 120 bila bao katika mechi ya Kombe la Dunia 2022 hatua ya 16 bora, beki huyo wa kulia wa Paris Saint-Germain aliitwa kupiga mkwaju wa penalti, mkwaju ambao umeandika upya historia ya soka ya Morocco.
Huku taifa zima likiwa na presha na mashabiki wasioegemea upande wowote, Hakimi alisimama, akainama kushoto, akamwangalia kipa wa Uhispania Unai Simon, na kumwambia wewe, mimi naitwa Hakimi daka nikuone…ilinyongwa Panenka ya hatari kipa akabaki anaangalia mpira unavyoingia.
Unaweza kusema kwamba Hakim ni kiongozi halisi wa timu ya taifa, lakini uchezaji bora wa mara kwa mara wa Hakimi umekuwa mojawapo ya mambo machache ambayo wafuasi wa Morocco wanaweza kujinufaisha nayo kwa muda wa miaka mitatu iliyopita.
ROBO FAINALI
Kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo imeingia robo fainali ya Kombe la Dunia kwa kuifunga Hispania mabao 3-0 kwa mikwaju ya penalty. Morocco sasa inasubiri siku ya Jumamosi ambapo itacheza na Ureno katika hatua hiyo.
Bado Afrika ina matumaini na Morocco, kutokana na ubora walionao na hata aina ya mchezo wanaoonyesha katika kila mchezo.
Mungu ibariki Afrika, Morocco pia.