Hakimu ajitoa kesi uhalifu Kanisa Kuu Geita

HAKIMU Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Cleofas Waane amejitoa kuendelea kusikiliza kesi ya uvamizi na uhalifu katika Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo Katoliki la Geita.

Waane alikuwa na wajibu wa kusikiliza kesi hiyo namba 62 ya mwaka 2023 inayomkabili Elpidius Edward (22) mkazi wa Mtaa wa Katundu, Kata ya Kalangalala mjini Geita.

Hakimu Waane amesema hawezi kuendelea na shauri hilo kutokana na mgongano wa kimaslahi kwani yeye ni Mkristu na muumini wa Kanisa Katoliki.

Baada ya uamuzi huo, alirejesha shauri hilo kwenda kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Geita, Samwel Maweda.

Hakimu Maweda alichukua uamuzi wa kuhamisha shauri hilo kwenda kwa Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Johari Kijuwile ambaye alitaja shauri la kesi hiyo Aprili 3, mwaka huu.

Hakimu Johari jana aliahirisha kesi hiyo mpaka Aprili 12 mwaka huu wakati mshitakiwa atakapopandishwa kizimbani kusomewa hoja za awali za mashitaka yanayomkabili.

Elpidius alifikishwa mahakamani na kusomewa shauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita kwa mara ya kwanza Machi 6 mwaka huu baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita kumpeleka mahakamani.

Elpidius anadaiwa kufanya makosa mawili likiwamo la kuvunja na kuingia kwenye nyumba ya ibada kinyume na kifungu cha sheria namba 291 (I)a na kifungu kidogo cha sheria ya adhabu.

Mtuhumiwa anadaiwa kukiuka sheria hiyo Februari 26, 2023 katika Parokia ya Maria Malkia wa Amani iliyopo Mtaa wa Jimboni, Kata ya Buhalahala, Halmashauri ya Mji wa Geita mkoani Geita.

Inaelezwa, kosa la pili la mtuhumiwa huyo ni kufanya uharibifu wa mali zenye thamani ya Sh milioni 48.2 ndani ya Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo Katoliki la Geita majira ya saa nane usiku.

Habari Zifananazo

Back to top button