“Hakuna kibali kwa wapiga ramli

KIGOMA; Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye amesema hakuna kibali kilichotolewa na Ofisi ya Rais kuruhusu vitendo vya kupiga ramli chonganishi na kutoa uchawi (mizigo) kwenye nyumba za watu kunakofanywa na waganga wa kienyeji maarufu Kamchape.
Andengenye amesema hayo wakati akitoa maelezo kwa Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni, Issa Gavu alipokuwa akizungumza na wajumbe wa baraza la wazee la Chama Cha Mapinduzi Mkoa Kigoma na badala yake alisema kuwa serikali kupitia wakuu wa wilaya na polisi imechukua hatua Madhubuti kupambana na vitendo hivyo.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa katika hatua walizochukua hadi sasa karibu watu 250 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo wamekamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani wakishitakiwa kushiriki katika vitendo hivyo ambapo amesema malalamiko yaliyotolewa na wajumbe wa baraza la wazee kwamba serikali haifanyi lolote kwenye suala hilo siyo kweli.
“Vitendo hivyo vya ramli chonganishi vimeonekana kupendwa na wananchi ambao wanawapokea na kuzunguka nao nyumba kwa nyumba, lakini wenyeviti wa vijiji viongozi wa chama kwenye ngazi ya kata,vijiji na matawi hawajawahi kushirikiana na serikali kwa namna yeyote kukemea kwa kuogopa kulaumiwa na wananchi hao,”Amesema mkuu huyo wa mkoa.
Awali Mzee, Paul Masabo kutoka Kigoma Mjini alimwambia Katibu huyo wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuwa wazee wamekuwa wakidhalilishwa kwa kuitwa wachawi ambapo wananchi wameungana na waganga maarufu kama kamchape kupita kwenye nyumba zao kutoa uchawi na kuwanyoa vipara wazee hao huku kukiwa hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na serikali.
Akizungumzia wajibu wa viongozi, Issa Gavu amesema kuwa ni lazima viongozi wa vijiji na kata kwa ngazi ya serikali za vijiji na chama lazima wasimamie ulinzi na usalama wa watu wao bila kukubali udhalilishaji na mambo yanayotweza utu wa mtu.
 

Habari Zifananazo

Back to top button