Hakuna mgonjwa mpya wa kipindupindu Dar
MPAKA sasa hakuna mgonjwa mpya wa kipindupindu aliyeripotiwa baada ya kutangazwa kulipuka kwa ugonjwa huo Aprili 25 mwaka huu na Wizara ya Afya, ambapo watu 15 walibainika kuugua, 13 wakitokea Wilaya ya Ilala na wawili Wilaya ya Kinondoni.
Aidha wagonjwa wawili ambao walikuwa wamelazwa hospitalini kwa ugonjwa huo wameruhusiwa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume amesema hayo kwenye mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo wanahabari wa mkoa huo kuhusu ugonjwa wa kipindupindu na kusema kuwa kati ya wagonjwa hao wanawake walikuwa tisa na wanaume sita.
Akifafanua amesema kutopata maambukizi mapya kumesababishwa na hatua mbalimbali za dharura zilizochukuliwa na serikali za kuwafuatilia watu wa karibu, ambapo wagonjwa walitokea, kutoa elimu na kuchukua sampuli za maji na kutibu maji kwenye visima shughuli ambayo bado inaendelea.
Dk Mfaume alisema asilimia 90 ya sababu ya mtu kupata ugonjwa huu ni maji yasiyo safi na salama, hivyo wamekuwa wakishirikiana na dawasa kutoa elimu na kutibu maji hatua ambayo ilifanyika hadi kwa wauza maji ya visima.
Amesema wametoa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ikiwa ni jitihada za kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali, kwani wanahabari ni kundi muhimu kwa kuwa ndio wanasaidia kutoa taarifa maeneo ambayo serikali huenda haijaweza kuyafikia.
Naye Mtaalam kutoka Idara ya Kinga Wizara ya Afya, Dk Fredrick Jacob, amesema kipindupindu ni ugonjwa unaoathiri zaidi nchi zinazoendele, ambapo kila mwaka watu milioni 2.8 huugua na watu 95,000 hufariki kwa ugonjwa huo duniani.
“Idadi hii ni kubwa kwa kuwa mgonjwa hawezi kushiriki shughuli zake binafsi, hivyo jamii tuna kila sababu ya kujikinga na visababishi vyake,”amesema.
Ili kukabiliana nao amesema jamii inatakiwa kuepuka visababishi vyake ambavyo vingi vinatokana na tabia ya mtu kuwa mchafu, ikiwemo kula kinyesi kibichi kwa kutonawa mikono anapotoka chooni,kula vyakula bila kunawa mikono na kutotumia vyoo na kunywa maji yaliyochanganyikana na kinyesi.
Kwa upande wake Ofisa Afya Mkoa wa Dar es Salaam, Enezael Ayo amesema pamoja na kutokuwa na maambukizi mapya, lakini bado wapo katika siku 21 za uangalizi ndio ijulikane kuwa hakuna kabisa mgonjwa kwani hapo katikati anaweza akatokea.