Hakuna visa vya Marburg – Waziri Ummy

MLIPUKO wa virusi hatari vya Marburg katika Mkoa wa Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania- Kagera umedhibitiwa rasmi, lakini mamlaka itaendelea kufuatilia kwa siku 42 zaidi kabla ya kutangaza mwisho wa mlipuko huo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametangaza leo jijini Dar es Salaam “Tunatarajia kutangaza mwisho wa mlipuko wa virusi vya Marburg mwezi ujao (Mei 31, 2023) iwapo hakutakuwa na kisa kipya,” Waziri Ummy aliwaambia waandishi wa habari akiutaja uamuzi huo kama sehemu ya maelekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Takriban watu sita akiwemo mhudumu wa afya na mtoto wa miezi 18 walifariki wakati watu tisa walipoambukizwa ugonjwa huo ambao ulikumba sehemu ya kaskazini-magharibi mwa Tanzania mwezi Machi mwaka huu.

Wagonjwa wawili waliachwa chini ya kituo maalumu kwa ajili ya ufuatiliaji na matibabu. “Hadi Aprili 21, 2023 wagonjwa hao wawili walithibitishwa kimaabara kuwa hawana maambukizi ya Marburg,” Waziri Ummy amesema wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari. “Walionusurika na ugonjwa huo ni pamoja na daktari ambaye alimhudumia mgonjwa wa kwanza wa Marburg.”

“Hii inadhihirisha jinsi hatua za haraka zilizochukuliwa na Serikali zilihakikisha udhibiti kamili wa ugonjwa huu na kwamba hausambai nje ya familia zilizoathiriwa na kwa wafanyikazi wa afya waliohudumia wagonjwa,” Waziri aliongeza.

Ummy amewataka wananchi kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo na magonjwa mengine ya kuambukiza. Aliwashukuru wataalam wa afya hasa walio mstari wa mbele katika Mkoa wa Kagera wakiwemo waliotoa huduma kwa wagonjwa na timu ya ufuatiliaji.

Habari Zifananazo

Back to top button