DAR ES SALAAM: Wadau wa Uvuvi nchini wamesema tatizo la uchafuzi wa mazingira ya bahari bado ni changamoto kubwa ya uharibifu wa mazalia ya samaki baharini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na HabariLeo jijini Dar es Salaam, baadhi ya wadau wa uvuvi wamesema kumekuwepo na upungufu wa upatikanaji wa samaki baharini kutokana na changamoto za uharibifu wa mazingira ya bahari.
“Wanapotumia uvuvi wa makokoro wanafanya uharibifu wa sakafu ya bahari kwa sababu wanakwangua majani lakini pia samaki wachanga wengi wanazaliwa katika maji machache au madogo kwahiyo uvuvi wa makokoro unafanyika katika maji madogo kwahiyo unaua samaki wachanga na viumbe wengine wa bahari “ alisema Asha
Chande Dadi Ally ambaye ni mvuvi na mfanyabiashara wa samaki katika soko la samaki la kimataifa Feri ameeleza kuna haja ya kujizatiti zaidi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira.
“Tunachotakiwa tuwe na uwelewa na kuwezesha kuheshim bahari kufanya yale tunayoyafanya kwenye matumizi yetu yaki kibinaadam tufanye nje ya fukwe za bahari, waweke sehemu salama zile takataka, tusitupe kwenye bahari” alisema Dadi
Kwa upande wake Mtoka Musa ambaye ni mvuvi katika soko hilo la samaki la Feri ameelezea changamoto wanazopitia kuhusu upatikanaji wa samaki na kushauri serikali kuendelea kushirikiana katika kuelimisha wavuvi ili kupunguza adha na changamoto inayoikumba sekta hiyo.