MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kutokana na utabiri walioutoa ya kwamba ongezeko la mvua linatarajia zaidi katika kipindi cha mwezi Mei hadi Juni mwaka huu.
Kaimu Meneja wa Ofisi Kuu ya Utabiri TMA, Dk Mafuru Kantamla amesema hayo Aprili 4, 2023 katika mahojiano maalumu katika siku ya pili ya kikao cha baraza la wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) mjini Morogoro.
Kaimu Meneja wa Ofisi Kuu ya Utabiri TMA, amesema hayo kuhusiana na utabiri, ambao Mamlaka hiyo ilitoa ikihusisha mvua za masika Februari 22, 2023.
Utabiri huo ulitolewa kwa umma kupitia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo , Dk Ladislaus Chang’a.
Amesema wanategemea msimu wa masika, mvua zinatarajia kuwa za wastani na hadi chini ya wastani katika maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka nchini.
Lakini katika baadhi ya maeneo ya upande wa Kaskazini hususani ya Mkoa wa Morogoro, baadhi ya maeneo ya mkoa wa Pwani na kisiwa cha Unguja , mvua hizo zilitarajia kuwa za wastani hadi juu ya wastani na mtawanyiko wake ulitarajia kuanza wiki ya mbili na ya tatu ya mwezi wa Machi mwaka huu.
Amesema mwanzoni mwa Aprili mvua hizo hazitakuwa na mtawanyiko mzuri katika maeneo ya ukanda wa Pwani ya Kaskazini.
“Mwezi huu wa nne kutakuwa na vipindi vidogo vya ukavu usiozidi siku 10, lakini mvua hizi zinatarajia kuimarika zaidi tunapoelekea mwezi wa tano, “ amesema Dk Kantamla.
Amesema kuimarika huko kunatokana na kuonesha viashiria vya mfumo wa mvua vinaonesha joto la bahari Magharibi mwa bahari ya hindi linatarajia kuongezeka na vile vile joto la bahari katika tropiki ya bahari ya pasific linatarajiwa kuongezeka.
“ Hali hii inatarajia kuongeza wigo mkubwa wa mvua za masika katika maeneo haya ya Pwani ya Kaskazini, ukiwamo na Mkoa wa Morogoro,” amesema Dk Kantamla.
Amesem kuwa mvua za masika kwa kawaida huwa zinatarajia kuanza mwezi Machi na zinaisha mwezi Mei kila mwaka, lakini msimu huu wa 2023, wataalamu walifuatilia mifumo ya hali ya hewa na kujiridhisha kwa kiwango cha juu ya kwamba mvua hizo zitakuwa na mwendelezo na zitaendelea mpaka Juni .
“ Pamoja na kwamba kutakuwa na ongezeko la mvua katika kipindi cha mwezi Mei, lakini mvua hizi zinatarajiwa kuendelea kwenda mpaka kati kati ama kuelekea mwishoni mwa mwezi Juni,” amesema Dk Kantamla
Kutokana na hali hiyo amesema ni vyema sasa kwa jamii kuweza kuzitumia fursa hizo za mvua ambazo zinatarajia kuongezeka, kwa kujua ni nini wanaweza kufanya kwa kuhusisha wataalamu maofisa ugani.