HALMASHAURI ya Wilaya ya Meru, imenunua mashine za kisasa za upimaji wa ardhi kwa lengo la kuondoa changamoto za migogoro ya ardhi kwa wananachi.
Vifaa hivyo ni mashine za kisasa zinazohusiana na masuala ya upimaji wa ramani, mashine ya kuprinti ramani za kila saizi, vifaa vya kutunzia ramani, mashine ndogo za upimaji (GPS), ambapo pia kila mtaalamu wa ardhi amewezeshwa kompyuta mpakato zenye uwezo wa kufanya kazi za uchoraji.
Kutokana na halmashauri hiyo kununua vifaa vya kisasa,Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Mwalimu Zainabu Makwinya kwa kununua vifaa hivyo.
Amesema ametembea halmshauri zote nchini, lakini amejionea mabadiliko makubwa katika halmashauri hiyo kupitia kwa Mkurugenzi huyo kuamua kununua vifaa vya kisasa kwa ajili ya upimaji na hatimaye halmashauri kupata mapato na kubuni maeneo mengine ya uwekezaji, ili kujikwamua kiuchumi.
Waziri Mabula alishauri pia wapimaji hao kuwafuata wananchi kwenye maeneo wanayoishi, ili kuwapunguzia gharama za kuleta fomu au kutaka hati za ardhi, au kuwahitaji wapima ardhi katika maeneo husika wanapoishi wananchi.
Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri hiyo, Leonard Mpanju anasema halmashauri hiyo ina changamoto ya migogoro ya ardhi kati ya Halmashauri ya Meru na Arusha Jiji, ikiwemo vijiji na vijiji na kuishukuru serikali kwa kutatua mgogoro wa ardhi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa (KIA).