Halmashauri, shirika wazungumza kupunguza hewa ukaa

MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, George Mbilinyi amesema halmashauri hiyo itaendelea na mazungumzo na Shirika la Maendeleo ya Mpingo (MCDI) juu ya namna ya kuendesha Mkakati wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa kupitia Utunzaji wa Misitu (Mkuhumi).
Alisema hayo katika kikao maalumu kati ya MCDI na halmashauri hiyo kilichofanyika Mtama kikilenga kuwa na makubaliano ya kuanzishwa kwa mradi wa Mkuhumi katika halmashauri hiyo.
Katika kikao hicho, Mbilinyi alishukuru shirika kwa kuwa tayari kuanzisha mradi huo katika halmashauri yake na kuahidi kukaa vikao endelevu na kamati yake waone jinsi ya kutekeleza mradi huo kwa maendeleo ya jamii.
MCDI ni shirika lisilo la kiserikali lililopo Kilwa Masoko Mkoa wa Lindi linalofanya kazi kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya kusaidia vijiji vinavyomiliki misitu ya asili kuwa na hifadhi endelevu zenye uvunaji endelevu kwa ajili ya maendeleo ya jamii.
Husaidia vijiji kuvitafutia masoko ya mazao ya misitu na wanajihusisha na upandaji wa miti katika vijiji.